` TAASISI YA JOSEPH MUHUNDA NYERERE FOUNDATION YAPANDA MITI SHINYANGA KUMUUNGA MKONO RAIS SAMIA KUTUNZA MAZINGIRA

TAASISI YA JOSEPH MUHUNDA NYERERE FOUNDATION YAPANDA MITI SHINYANGA KUMUUNGA MKONO RAIS SAMIA KUTUNZA MAZINGIRA



Na Marco Maduhu, SHINYANGA

Taasisi ya Joseph Muhunda Nyerere Foundation, imepanda miti katika Chuo cha Ualimu Shinyanga (SHYCOM), kwa lengo la kutunza mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
Zoezi hilo limefanyika leo Februari 2, 2026 katika maeneo mbalimbali ya chuo hicho, likiwa na lengo la kuhamasisha wananchi wa mkoa huo kupanda miti kwa wingi na kuhifadhi mazingira.

Mkurugenzi wa Taasisi hiyo Chief Muhunda Nyerere, akizungumza kwenye upandaji huo wa miti, amesema siku ya kuzaliwa kwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, katika hotuba yake aliutaja mkoa wa Shinyanga na Dodoma, kuwa inakabiliwa na hali ya ukame.
Amesema kutokana na hali hiyo, taasisi yake imeona umuhimu wa kumuunga mkono Rais kwa kuhamasisha upandaji miti katika mkoa wa Shinyaga, ili kusaidia kupunguza athari za ukame na mabadiliko ya tabia nchi kwa kutunza mazingira.

“Nimeamua kuhamasisha upandaji miti kwa vitendo hapa mkoani Shinyanga, ili kutunza mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi yanayosababisha pia hali ya ukame na leo tumepanda miti zaidi ya 100 katika Chuo cha Ualimu Shinyanga,” amesema Nyerere.
Ameongeza kuwa taasisi hiyo inajishughulisha na masuala ya utunzaji wa mazingira nchini, na kwamba kwa mkoa wa Shinyanga itashirikiana na Serikali, taasisi za mazingira pamoja na wadau mbalimbali kwa kuhakikisha miti inapandwa kwa wingi, ili kuufanya mkoa huo kuwa wa kijani.

Aidha, ametoa wito kwa wananchi mkoani humo, kupanda miti kwa wingi, kutunza vyanzo vya maji pamoja na misitu, kwa kuacha ukataji wa miti hovyo, ili kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabia nchi.
Nao baadhi ya wananchi wa Shinyanga walioshiriki zoezi hilo la upandaji miti akiwamo Sonda Kabeshi, wamesema elimu bado inahitaji kwa wananchi kupanda miti kwa wingi na kuacha kuikata hovyo, ili kuondokana na hali ya ukame.

Amesema, historia ya Shinyanga ni mkoa wenye ukame, na kwamba Serikali na wadau mbalimbali wa mazingira wamejitahidi kuubadilisha kwa kupanda miti, lakini juhudi zaidi bado zinahitajika ili kuufanya mkoa huo uwe wa kijani.

TAZAMA PICHA👇👇
Mkurugenzi wa Taasisi ya Joseph Muhunda Nyerere Foundation, Chief Muhunda Nyerere akipanda mti.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464