RAS HAMDUNI AKUTANA NA TUME YA TAIFA YA MIPANGO KUKAGUA MIRADI YA KIMKAKATI SHINYANGA
Na. Johnson James, Shinyanga
Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga, CP Salum Hamduni, amekutana na kufanya mazungumzo na ujumbe kutoka Tume ya Taifa ya Mipango iliyopo chini ya Wizara ya Mipango na Uwekezaji, uliowasili mkoani humo kwa lengo la kutembelea na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa katika Mkoa wa Shinyanga.
Akizungumza leo Februari 11,2026 katika kikao kilichofanyika Ofisini kwa Katibu Tawala, Meneja wa Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathmini kutoka Tume ya Taifa ya Mipango, Bw. Royal Lyanga, amesema kuwa ziara hiyo inalenga kujionea hatua za utekelezaji wa miradi ya kimkakati pamoja na kutathmini mchango wake katika kukuza uchumi wa mkoa na Taifa kwa ujumla.
Ametaja baadhi ya miradi itakayotembelewa kuwa ni pamoja na Uwanja wa Ndege wa Shinyanga (Ibadakuli) na Mradi wa Umeme wa Jua wa Kishapu, ambayo ni miradi muhimu katika kuimarisha miundombinu na upatikanaji wa nishati safi na ya uhakika.
Kwa upande wake, CP Hamduni amesema miradi hiyo imetekelezwa kwa viwango vya kuridhisha na iko katika hatua za mwisho kuelekea kuanza kutumika rasmi, jambo litakalowawezesha wananchi wa Shinyanga kunufaika na matunda ya uwekezaji huo wa kimkakati.
Amesisitiza kuwa Serikali ya Mkoa itaendelea kushirikiana kwa karibu na taasisi za kitaifa kuhakikisha miradi yote inakamilika kwa wakati na kuleta tija iliyokusudiwa kwa maendeleo ya wananchi.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464



