
.jpg)

Kijana anayetambulika kwa jina la Tegemeo akitengeneza jiko maalumu la kutumia mkaa mbadala.
"Dunia yetu haiwezi kuwa salama kama mazingira hayako salama, hewa tunayovuta haiwezi kuwa salama kama mazingira yetu hayako salama."
Nukuu hii inalenga kuonyesha umuhimu wa kutunza Mazingira tunayoishi kwa manufaa ya watu na viumbe hai wengine duniani.
Ni muhimu tutambue kuwa Mazingira yakiangamia na binadamu tutaangamia, Mazingira yakipotea na binadamu tutapotea, na iwapo nchi itakuwa jangwa tutalima wapi.
Aidha, nchini Tanzania inakadiriwa kuwa zaidi ya watu 33,024 hufariki kila mwaka kutokana na magonjwa ya mfumo wa hewa na moyo yanayosababishwa na matumizi ya nishati hafifu ya kupikia kama vile kuni na mkaa.
Huu siyo wakati wa kulaumiana tena kuwa nani katufikisha hapa kwa kukata miti ovyo,bali ni muda wa kuchukua hatua kwa kukubali mabadiliko chanya kwa kuwa bado inawezekana.
Tishio hilo linatokana na kasi kubwa ya watu kukata miti ovyo kwa lengo la kuandaa kuni,kuchoma mkaa,kupasua mbao,kuweka nguzo kwenye machimbo ya dhahabu (matimba) na kilimo cha kuhama hama hasa vijijini.
Kwa shughuli hizo Tanzania inapoteza hekta 372,000 za miti kwa mwaka kutokana na shughuli za kibinadamu ikiwemo matumizi ya nishati hafifu ya mkaa na kuni kama nishati mbadala wa kupikia.
MKAKATI WA MATUMIZI YA NISHATI SAFI YA KUPIKIA
Zipo sheria zetu nzuri, ikiwemo ya Sheria ya Usimamizi wa mazingira sura 191 kifungu cha 58 (2) kinaelekeza kuhusu hifadhi ya mazingira na ulinzi wa milima,vilima na miinuko na Sera ya Misitu ya mwaka 1998 imeelekeza utaratibu wa kutunza na kuhifadhi.
Vile vile Sheria ya Ardhi ya Vijiji namba 5 ya mwaka 1999 na Sheria ya Misitu Sura 323, zimeweka utaratibu wa kisheria kudhibiti uharibifu wa mazingira hususani ukataji miti holela katika maeneo mbalimbali yakiwemo ya milima na miinuko.
Aidha, zipo jitihada mbalimbali zinafanyika za kukabiliana na changamoto hiyo jitihada hizo zimesababisha Rais wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kuwa kinara wa ajenda ya Nishati Safi ya kupikia nchini na Afrika.
Rais bado anaendelea kuipeleka ajenda hiyo Kimataifa ili kuhakikisha watu wanapika katika mazingira salama kiafya na kimazingira kwa kutumia nishati salama inayopatikana na kutumika kwa urahisi..
Jitihada za serikali zinazopaswa kupongezwa katika suala hili ikiwemo maelekezo ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan,kupiga marufuku taasisi zote zenye idadi ya kuanzia watu 100 kuacha kutumia kuni katika kuandaa chakula badala yake zitumie nishati safi ya kupikia ikiwemo, gesi, umeme na makaa ya mawe.
Msingi huo umekolezwa na maboresho makubwa yaliyofanywa na Jeshi la magereza, ambalo limekuwa likitumia kuni kwa kipindi chote tangu kuanzishwa kwake hapa nchini.
Mkuu wa Jeshi la Magereza mkoa wa Geita,ACP Jonam Mwakasagule amesema, nia ya serikali kuzitaka taasisi za umma kutumia nishati safi ya kupikia inapaswa kuungwa mkono na jamii nzima.
"Wakati mwingine tulikuwa katika hatari kubwa ya usalama wa maisha yetu kutokana na wanyama pori wakali kama vile nyoka na wanyama wengine" amesema ACP Mwakasagule.
Amesema kuwa matumizi ya nishati safi katika jeshi hilo sasa yamepewa kipaumbe mkoani humo ili kujenga afya bora na kupunguza magonjwa ya macho pamoja na kifua kutokana na matumizi ya kuni wakati wa kupika chakula.
UJIO WA KIWANDA CHA MKAA MBADALA
Kutokana na ukweli huo,Wakala wa Nishati Vijijini(Rea) kwa kushirikiana na Shirika la Madini nchini(Stamico) wanakuja na mpango wa kujenga kiwanda cha kuzalisha mkaa mbadala mkoani Geita ili kuokoa mazingira na afya za watu zinaimarika.
Mjumbe wa Bodi ya Nishati Vijijini,Ahmed Chinemba, amesema serikali ipo kwenye maandalizi ya kujenga kiwanda hicho kwa ajili ya kuongeza ufanisi wa jamii kutumia nishati mbadala hasa vijijini.
Hatua hiyo itasaidia kunusuru ukataji wa miti ovyo na badala yake jamii itapaswa kuendelea kutunza Mazingira ili yawe endelevu kwa sasa na vizazi vijavyo.
"Tukumbuke kuwa maelekezo ya Rais ni kuwa taasisi zinazohudumia watu zaidi ya 100 ziachane na matumizi ya kuni na mkaa, na kwamba zinapaswa kuanza kutumia nishati safi ya kupikia ikiwemo gesi asilia, umeme, bayogesi na makaa ya mawe yaliyoboreshwa, “
"Matumizi ya nishati safi ya kupikia ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais Samia katika mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati safi ya kupikia (2024 - 2034)."amesema Chinemba.
Naye kamishna wa Umeme na Nishati Jadilifu nchini,Mhandisi Innocent Luoga, amesema, Tanzania ndiyo nchi kinara wa matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa nchi za Afrika mashariki kutokana na sera na miongozo iliyojiwekea ili kufikia malengo.
"Kwa Tanzania safari ya nishati safi ya kupikia tuliianza rasmi mwaka 2022 ambapo Rais Dkt. Samia alianzisha mjadala wa nishati hii kupitia wadau mbalimbali na kutoa maelekezo ya utekelezaji ikiwemo ya kuanzishwa mkakati wa nishati safi ya kupikia ambao ulizinduliwa mwaka 2024 ukiwa unaelekeza kuwa aslimia 80 ya watanzania wanapaswa kutumia nishati hiyo ifikapo mwaka 2034."
Amesema ii kufikia malengo ya mpango huo,serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali kwa lengo la kuhakikisha wananchi wote wanatumia nishati safi ya kupikia ikiwemo kugawa mitungi ya gesi kwa bei ya ruzuku,kutoa elimu kwa makundi mbalimbali na kusambaza gesi asilia kwa njia ya bomba hasa kwa baadhi ya mikoa ya Lindi,Mtwara na Dar es salaam.
"Hatua nyingine ni kuweka unafuu wa Kodi kwa baadhi ya vifaa vya nishati safi ya kupikia vinavyoingia nchini pamoja na kupitia Sheria,kanuni na Sera ili kuangalia maeneo yatakayo rahisisha upatikanaji wa nishati hiyo.
Kwa mujibu wa Luoga, takribani watu bilioni 2.1 duniani hawatumii nishati safi ya kupikia huku nchi za ukanda wa Jangwa la Sahara zikiwa ni watu milioni 990 wasio tumia nishati hiyo safi.
Kadhalika kwa Tanzania watu wanaotumia nishati safi ya kupikia ni takribani aslimia 16 pekee huku malengo ya serikali yakiwa ni wananchi wote kutumia nishati hiyo muhimu.
SHIRIKA LA UNDP
Mwakilishi mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP) Shigeki Komatsubara, anaipongeza Tanzania kwa kutekeleza ajenda ya nishati safi ya kupikia kupitia jitihada mbalimbali.
Amedai kuwa, kielelezo kikuu ni uwepo wa mkakati wa taifa wa matumizi ya nishati safi ya kupikia ambao ni Dira katika kufikia lengo la aslimia 80 ya watanzania wanaopaswa kutumia nishati hiyo.
NINI KIFANYIKE
Baadhi ya wadau wa mazingira akiwemo Hadija Omari na Rethisia Kaswahili wanaishauri serikali kuendelea kutoa elimu kwa umma ili watu watambue umuhimu wa kuhifadhi misitu na kupanda miti.
Wazee wa mila washirikishwe katika vikao mbalimbali hasa vijijini ili kutoa uzoefu wao katika kuhifadhi mazingira.
Wakala wa huduma za misitu nchini (TFS) waoteshe miche ya kutosha na kuigawa kwa watu ili kila mwananchi ashiriki katika kupanda na kutunza miche isiyopungua 10.
"Sheria zilizopo zisimamiwe kikamilifu na zile ambazo zinakinzana na uhifadhi wa mazingira zifumuliwe na kufanyiwa maboresho mapya kulingana na hali halisi wa sasa,"
"Serikali iweke ruzuku kwenye nishati safi ya kupikia ili ipatikane kwa wepesi na gharama nafuu hasa kwa wananchi waishio vijijini, wachimba Madini watumie vyuma badala ya matimba na vijiji viheshimu matumizi bora ya ardhi ili kudhibiti wakulima kuhamia maeneo mengine na kukata miti ovyo." anahitimisha Kaswahili.