` TUSIWE "MAZOMBI" KWA KUSALITI UTALII NA RASILIMALI ZA TAIFA

TUSIWE "MAZOMBI" KWA KUSALITI UTALII NA RASILIMALI ZA TAIFA

Katika hali inayoonyesha kuamka kwa ari mpya ya uzalendo, Watanzania wametahadharishwa kutokubali kutumika kama silaha ya kuangamiza uchumi wa nchi yao kupitia kampeni za kigeni zinazolenga kuua sekta ya utalii. 

Ujumbe mzito uliosambaa kwa kasi mtandaoni na kuungwa mkono na maelfu ya wazalendo, umebainisha kuwa mapambano yanayoendelea kwa sasa si ya kisiasa tu, bali ni "Vita vya Kiuchumi" ambapo maadui wa ndani na nje wanatumia hashtag zenye sumu kupandikiza hofu kwa watalii.

"Watanzania wenzangu, huu ni usaliti. Msidanganywe na watu wachache walioko nje ya nchi na nchi jirani ambao wanatushawishi tuibomoe nchi yetu kwa faida zao," ulisomeka ujumbe huo wa kizalendo uliopokelewa kwa hisia kali. 

Imefahamika kuwa wakati mataifa hayo jirani yakitoa viza za bure kwa nchi za Afrika na kutangaza utalii wao kwa nguvu, kwa upande mwingine wanachochea hashtag zinazosema "Tanzania siyo salama" ili watalii wakimbie kwenda kwao. Huu ni mkakati wa makusudi wa kutaka kuua soko letu la utalii, migodi, na rasilimali ili wao wanufaike wakati Tanzania ikiingia kwenye giza la machafuko.

Utalii ni Maisha, siyo Anasa Wananchi wametafsiri kampeni za "Kataa Utalii" kama shambulizi dhidi ya mkate wa kila siku wa Mtanzania. Mmoja wa wazalendo hao alikumbusha kuwa utalii ndio msingi wa ajira kwa kundi kubwa la watu: "Kuna wafanyabiashara wanauza mboga, kuku, mayai, na vinyago kwenye mahoteli ya kitalii. Ukikataa utalii, unaua maisha ya hawa watu wote." 

Sauti hizi za kishujaa zimewataka vijana kuacha kuwa "mabongo lala" na kutokubali kutumiwa kufanya fujo barabarani kwa ajili ya senti ndogo wanazolipwa na wasaliti.

Msimamo kuelekea Desemba 25 Kufuatia mjadala huo, Wananchi wametoa msimamo kuwa, kama ambavyo mipango ya kuvuruga maadhimisho ya Uhuru ya Desemba 9 ilivyoshindwa, ndivyo ambavyo msimu wa Krismasi Desemba 25 utakuwa wa amani tele.

"Tunakataa maandamano, tunalinda amani. Tanzania ni salama na itabaki kuwa salama," ni kauli iliyoshamiri, ikiwataka Watanzania kuzinduka na kutoiga mifano ya nchi zilizoharibika kama Libya, ambazo sasa zinatamani amani.

 Ujumbe ni mmoja: Uzalendo kwanza, na msaliti yeyote anayehujumu utalii na amani ya nchi hana nafasi katika nyumba yetu salama ya Tanzania.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464