` TANZANIA IKO SHWARI: POLISI WAONYA KUHUSU MBINU MPYA ZA UCHOCHEZI

TANZANIA IKO SHWARI: POLISI WAONYA KUHUSU MBINU MPYA ZA UCHOCHEZI



Jeshi la Polisi Tanzania limetoa wito kwa umma kuendelea kudumisha amani na utulivu, huku likisisitiza kuwa linashuhudia juhudi za mara kwa mara za kubadilisha mbinu za uchochezi zenye lengo la kuingiza vurugu na chuki nchini.

Taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Jeshi la Polisi, Makao Makuu, Jijini Dodoma, David Misime imesisitiza umuhimu wa kushirikiana na kukataa uchochezi huo.

“Tukatae yale yote yanayohamasishwa kwa njia mbalimbali na katika maneno ya kubadilisha mbinu kila mara ili kutaka kutuchonganisha na kutujengea chuki kati yetu.”

Taarifa hiyo iliongeza kuwa lengo la vitendo hivyo vya uchochezi ni “kutuuingiza katika vurugu ambazo matokeo yake siyo mazuri kama tunavyo shuhudia katika maeneo mengine duniani.”

Hali ya Usalama Nchini Iko Shwari

Wito huo wa Polisi unakuja siku moja baada ya kutoa taarifa ya kuhakikisha Watanzania hali ya usalama. Jeshi la Polisi, kupitia taarifa yake, limewajulisha wananchi kuwa, “kwa ushirikiano wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama pamoja na ninyi wananchi na wadau wengine katika kutimiza jukumu la kulinda amani, utulivu na usalama nchini, hadi sasa nchi yetu kiusalama ni shwari na shughuli za kiuchumi na za kijamii ziliendelea vizuri katika mazingira ya amani kwa kipindi hicho cha masaa 24.”

Jeshi hilo limeeleza kuwa wanapoendelea kuelekea siku ya mwisho wa wiki, wanatoa wito kwa kila mmoja kuendelea kutii sheria, kushirikiana na kila mmoja na kutekeleza wajibu wake katika kulinda na kuimarisha amani ambayo kila mmoja anaihitaji katika maisha na shughuli zake za kila siku.

Jeshi la Polisi limeahidi kuwa, kwa kushirikiana na Vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama, litaendelea kulinda usalama wa nchi yote, maisha na mali za kila mmoja, pamoja na Taifa zima la Tanzania.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464