
Wakati Taifa linashuhudia upepo mpya wa mageuzi katika sekta ya utalii, unaoongozwa na hotuba yenye dira pana ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, imedhihirika wazi kuwa amani na maridhiano ndio msingi imara unaobeba ndoto hizi za kiuchumi.
Wananchi kutoka kila pembe ya nchi wamepokea kwa furaha na matumaini makubwa mwelekeo wa Serikali wa kulifanya taifa kuwa kitovu cha utalii wa kimataifa ifikapo mwaka 2030.
Kuridhishwa huku kunaashiria safari ya mafanikio ambayo Taifa limeanzia katika kujenga upya umoja na utulivu baada ya kipindi cha siasa kali.
Hotuba ya Rais Samia imeonyesha wazi kwamba mageuzi makubwa ya kiuchumi hutegemea utulivu wa kijamii na kisiasa. Wananchi wanasema hotuba hiyo imerejesha matumaini mapya, si tu katika uchumi, bali pia katika imani kwa uongozi.
Kauli za Rais Samia za kuongeza idadi ya watalii, kuboresha bustani za wanyama, na kuimarisha huduma za ndani zinazounga mkono sekta ya utalii, zote zinategemea hali ya amani.
“Rais Samia amekuwa mfano wa uongozi unaojenga, sio unaogawa.” Kauli hii inadhihirisha jinsi uongozi unaoegemea kwenye maridhiano unavyotoa fursa kwa kila mwananchi, bila kujali tofauti zao, kushiriki kikamilifu katika ustawi wa taifa.
Katika muktadha huu wa kujenga upya, ni muhimu kuangazia maneno ya Rais mwenyewe kuhusu amani:"Tanzania imebarikiwa kuwa kisiwa cha Amani na Utulivu. Tuna wajibu wa kuhakikisha moto huu wa amani unawaka daima. Amani si tu kukosekana kwa vita, bali ni umoja, mshikamano, na heshima kati yetu sote."
Kauli hii inatoa msisitizo wa kipekee. Utalii wa kimataifa hauwezi kustawi katika nchi yenye vurugu au migawanyiko. Amani huleta miundombinu safi na husaidia ongezeko la watalii. Utulivu huvutia wawekezaji wa kudumu, ambao huwezesha ujenzi wa hoteli na kambi za watalii zinazotoa ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja kwa maelfu ya vijana na wanawake.
Aidha, wananchi wamepongeza juhudi za Rais za kutumia matukio makubwa ya kimataifa, kama vile filamu na makongamano, kuitangaza Tanzania. Mafanikio haya yote yanapimwa kwa jinsi gani nchi inavyoonekana kuwa salama na yenye kukaribisha wageni – matunda halisi ya maridhiano na amani.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464