
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Mbunge wa Kilosa, Profesa Palamagamba Kabudi, amesema hotuba aliyoitoa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati wa uzinduzi wa Bunge la 13 imewapa Watanzania mwanga mpya na kuongeza imani juu ya safari ya maendeleo kwa miaka mitano ijayo.
Akichambua hotuba hiyo, Prof. Kabudi alibainisha kuwa uthabiti wa Rais Samia na namna anavyowajali wananchi ndivyo vimeleta faraja kubwa nchini.
Profesa Kabudi alinukuu kitabu cha hayati Shaban Robert cha ‘Kusadikika’ akisema: "katika nyakati ngumu huzaa viongozi thabiti." Alieleza kuwa katika kipindi hiki cha changamoto, Rais Samia ameonesha ujasiri na uthabiti wake wa kipekee.
'Uthabiti huu sio tu wa kuomboleza na kutambua msukosuko uliokuwepo nchini, bali pia ameonesha matumaini na nyenzo za kutimiza matumaini hayo,' alisema Prof. Kabudi.
Aliongeza kuwa ahadi za Rais Samia za kuanzisha Madirisha ya Uwekezaji na kutenga shilingi bilioni 200 kwa ajili ya mitaji kwa vijana zitabadili maisha yao.
Kwa mujibu wa Profesa Kabudi, hotuba ya Rais Samia ilikuwa ni mfariji mkubwa kwa Taifa hasa pale alipozungumzia kaulimbiu ya Serikali ya 'Kazi na Utu'.
Rais Samia alisema anatamani Awamu yake ya Sita ikimalizika, ikumbukwe si kwa sababu ya ujenzi wa miundombinu mikubwa pekee, bali kwa sababu utu wa Mtanzania uliendelezwa na kupewa thamani kubwa.
"Msisitizo aliouweka Rais katika kushughulikia changamoto za watu wa kawaida umeleta faraja. Alizungumzia kwa ujasiri kuhusu uponyaji wa Taifa, akitangaza Tume ya Uchunguzi na kutoa msamaha kwa vijana wa mkumbo. Hii inaonyesha kiongozi ambaye anajali utu zaidi ya siasa," alimalizia Prof. Kabudi.
Maneno haya ya Mbunge huyo yanathibitisha kuwa, hotuba ya Dkt. Samia ilikuwa na lengo la kuunganisha Taifa, kulipa faraja, na kuliweka kwenye njia thabiti ya maendeleo yenye utu.