Mkurugenzi Mtendaji wa TMF, Dastan Kamanzi
Meneja Uendeshaji kutoka Shirika lisilo la kiserikali Climate Action Network Tanzania (CAN), Boniventure Mchomvu.
Na Kadama Malunde - Morogoro
Waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya redio, magazeti na mitandao ya kijamii wamepata mafunzo maalum kuhusu mabadiliko ya tabianchi kuelekea Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP30) unaotarajiwa kufanyika Novemba 2025 mjini Belem, Brazil.
Mafunzo hayo ya siku tatu yamefanyika kuanzia Oktoba 22 hadi 24, 2025 mkoani Morogoro, yakilenga kuongeza uelewa na ujuzi wa waandishi wa habari kuhusu namna bora ya kuripoti masuala ya mabadiliko ya tabianchi na kuhusisha ajenda za kitaifa na kijamii katika mijadala inayoelekea mkutano wa COP30.
Mafunzo hayo yameandaliwa na Tanzania Media Foundation (TMF) kwa kushirikiana na Oxford Policy Management (OPM), kwa ufadhili wa Ubalozi wa Uingereza na Uswisi.
Lengo kuu la mafunzo ni kuwawezesha waandishi wa habari kuelewa dhana muhimu za mabadiliko ya tabianchi, sera husika, vipaumbele vya kitaifa kwenye mkutano huo, pamoja na mbinu za kuwasilisha taarifa sahihi, zenye ushawishi, na zinazochochea hatua za kijamii na kisera.
Wakufunzi wa mafunzo hayo walikuwa Mkurugenzi Mtendaji wa TMF ,Dastan Kamanzi na Meneja Uendeshaji kutoka Shirika lisilo la kiserikali Climate Action Network Tanzania (CAN), Boniventure Mchomvu
Jumla ya waandishi 20 kutoka mikoa 13 ya Tanzania walishiriki katika mafunzo hayo, wakiwemo wanaume 12 (60%) na wanawake 8 (40%). Washiriki walitoka kwenye aina tatu za vyombo vya habari: mitandao ya kijamii 10 (50%), redio 6 (30%), na magazeti 4 (20%).
Kupitia mafunzo hayo, washiriki wamepata fursa ya kujifunza kutoka kwa wataalamu wa mazingira, wahariri, na wanahabari wabobezi katika uandishi wa habari za tabianchi.
Mkutano wa COP (Conference of the Parties) ni jukwaa kuu la kimataifa linaloleta pamoja nchi wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (UNFCCC) kujadili na kukubaliana hatua za pamoja za kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi duniani.
Mkutano wa mwisho, COP29, ulifanyika mjini Baku, Azerbaijan mwaka 2024, ambapo washiriki walijadili masuala muhimu kuhusu fedha za tabianchi, utekelezaji wa ahadi za kupunguza hewa ukaa, na ushirikiano wa kimataifa katika kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.







































