

NA EUNICE KANUMBA
Taasisi za elimu nchini zimeshauriwa kuanza mchakato wa kutoa elimu kuhusu Dira ya Taifa ya 2050 ili kusaidia maandalizi ya rasilimali watu watakaoweza kukabiliana na mabadiliko ya kijamii na kiuchumi katika miaka ijayo.
Wito huo umetolewa oktoba 17,2025 na Wakili msomi Ipilinga Panya, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mahafali ya 32 ya Shule ya Sekondari Uhuru iliyopo katika Manispaa ya Shinyanga ambapo wakili huyo katika safari yake ya elimu alisoma katika shule hiyo kwa elimu ya kati
Wakili Panya amesema ni muhimu taasisi za elimu kuanza mapema kufundisha wanafunzi kuhusu dira hiyo, kwani ndani ya miaka 25 ijayo kundi la vijana waliopo mashuleni ndilo litakuwa na jukumu kubwa la kuleta maendeleo ya Taifa.
“Shule ya Sekondari Uhuru iwe mfano wa kwanza nchini kuanzisha somo au mafunzo kuhusu Dira ya Taifa ya 2050, ili kuepusha kizazi kijacho kuingia kwenye changamoto bila maandalizi, kana kwamba kinaelea mtoni huku mikono na miguu vikiwa vimefungwa kamba,” amesema wakili Panya.
Aidha akizungumzia mapambano dhidi ya rushwa wakili Panya amesema kuwa ni muhimu elimu dhidi ya rushwa pia ikatiliwe mkazo mashuleni, ili kujenga misingi ya haki, uwajibikaji na maendeleo endelevu katika jamii.
Katika kuchangia maendeleo ya shule hiyo, Wakili Panya ametoa mashine mbili za kunakilia (photocopy) pamoja na fedha taslimu kiasi cha shilingi milioni moja kwa ajili ya ujenzi wa jiko la shule,ambalo lipo mbioni kukamilika.
Akitoa shukrani, Afisa Elimu wa Sekondari -Manispaa ya Shinyanga, John Musa, amesema mgeni rasmi ni zao halisi la shule hiyo na amejitokeza kwa moyo wa kizalendo kusaidia uboreshaji wa miundombinu ya shule hiyo ikiwemo jiko la kupikia kama sehemu ya mchango wake katika sekta ya elimu ya manispaa ya Shinyanga.
“Serikali itachukua hatua kukamilisha sehemu iliyosalia, lakini tunatoa wito kwa watu wengine wenye nafasi kama hizi kuunga mkono shule walizosoma ili kuongeza ubora wa elimu,” amesema Musa.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Afisa Elimu ya watu wazima Manispaa ya Shinyanga Betrice Mbonea, alitoa wito kwa jamii kuhamasisha watoto wao kuendelea na masomo hata kama walisitisha kutokana na changamoto mbalimbali kama vile mimba za utotoni au hali duni ya uchumi na kuanisha kuwa serikali imeweka utaratibu wa elimu mbadala kwa wanafunzi waliokatishwa masomo ili kuhakikisha hakuna anayekosa fursa ya elimu.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Shule ya Sekondari Uhuru, Kanali Mstaafu John Kayoka, amewasihi wazazi na walezi kuendeleza jukumu la kuwasimamia watoto wao ili kuwaepusha na mwenendo usiofaa.
“Wanafunzi wanapaswa kujitunza na kufuata maadili mema ili wasizimishe ndoto zao, kwani wao ndiyo viongozi wa baadaye wa Taifa,” amesema Kanali Kayoka.
Kwa upande wake, Mkuu wa Shule hiyo, Mwalimu Victoria Nakuyaumu, amesema shule hiyo imekuwa ikifanya vizuri kitaaluma kila mwaka, ambapo kwa mwaka 2025 imefanikiwa kufikisha wastani wa asilimia 75 ya wanafunzi wanaoendelea kidato cha tano.
“Mwaka huu tunawahitimu wanafunzi 226, kati yao wasichana 113 na wavulana 113, na tunatarajia matokeo mazuri kutokana na nidhamu na juhudi kubwa za walimu,” amesema Nakuyaumu.
Shule ya Sekondari Uhuru imeanzishwa mwaka 1990 ikiwa na mikondo miwili tu na hadi sasa (mwaka 2025) ina jumla ya wanafunzi 1,020. Wanaosoma katika shule hiyo.
MWISHO
