` JWTZ YARIDHISHWA NA HALI YA USALAMA KUELEKEA UCHAGUZI MKUU, YAONYA WANAHARAKATI NA WANAOHUSISHA JESHI NA SIASA

JWTZ YARIDHISHWA NA HALI YA USALAMA KUELEKEA UCHAGUZI MKUU, YAONYA WANAHARAKATI NA WANAOHUSISHA JESHI NA SIASA

                


          Na Mwandishi Wetu

Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limeridhishwa na hali ya usalama iliyopo nchini huku taifa likielekea kwenye Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika tarehe 28 na 29 Oktoba, 2025. Jeshi limehakikishia Watanzania wote hali ya Amani, Usalama na Utulivu katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu, wakati wa uchaguzi na baada ya uchaguzi.

Kupitia taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Uhusiano wa JWTZ, Kanali Bernard Masala Mlunga , Jeshi lilitangaza kuwa linaendelea kufuatilia kwa karibu na kutathmini hali ya Ulinzi na Usalama nchini.

Msemaji huyo alisema kwamba JWTZ linaridhishwa na jinsi Vyama vya Siasa vinavyoendesha kampeni zao kwa kuzingatia matakwa ya kisheria, kuheshimiana na kuvumiliana kunakooneshwa kupitia kwa wagombea wao wa ngazi za Uraisi, Ubunge na Udiwani. Jeshi limetoa ombi kwa vyama vya siasa kuendeleza hali ya amani na utulivu wakati wote wa kampeni, kupiga kura na baada ya kupiga kura.

Aidha, Jeshi lililipongeza Jeshi la Polisi na Vyombo vingine vya Usalama kwa jinsi vinavyoendelea kusimamia hali ya usalama katika kipindi hiki. Pia limewapongeza wananchi kwa kuendelea kutumia haki yao ya msingi ya kushiriki kwa amani na utulivu katika kusikiliza sera za vyama mbalimbali.

Onyo kwa Wachochezi

Pamoja na hali ya amani iliyopo, Kanali Mlunga alisema kuwa kumeendelea kujitokeza baadhi ya watu wanaojiita wanaharakati kutoka ndani na nje ya nchi kutumia mitandao ya kijamii kupotosha Umma kwa kuweka maudhui yenye kuleta uchochezi. Wachochezi hao wanajaribu kulihusisha Jeshi na siasa ili kutimiza azma yao ya uvunjifu wa amani.

Jeshi linauomba Umma wa Watanzania kupuuza machapisho au taarifa ambazo zimekua zikionekana kwenye mitandao ya kijamii. Wananchi wanakumbushwa kuwa taarifa zote zinazolihusu Jeshi zitatolewa na Makao Makuu ya Jeshi kwa utaratibu rasmi wa mawasiliano ya Jeshi na Umma.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464