` MWENYE ULEMAVU ABUNI UTENGENEZAJI MIKEKA KWA CHUPA ZA PLASTIKI KUJIPATIA KIPATO,KUTUNZA MAZINGIRA

MWENYE ULEMAVU ABUNI UTENGENEZAJI MIKEKA KWA CHUPA ZA PLASTIKI KUJIPATIA KIPATO,KUTUNZA MAZINGIRA

Mwenye ulemavu abuni utengenezaji mikeka kwa chupa za plastiki kujipatia kipato,kutunza mazingira

Na Marco Maduhu,SHINYANGA

Katika maisha ya kila siku,taka za plastiki zimekuwa tatizo kubwa kwa jamii nyingi nchini,

Kwa mujibu wa taarifa ya Tovuti ya Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira),kwamba Tanzania kama zilivyo nchi nyingi kusini mwa Jangwa la Sahara,bado huduma ya kudhibiti taka ngumu si ya kuridhisha.

Inakadiriwa kuwa chini ya asilimia 50 ya taka zinazozalishwa ndizo hukusanywa kila siku,takribani asilimia 3 huchomwa kiholela, asilimia 30 hufukiwa, huku asilimia 17 hutupwa hovyo katika maeneo ya wazi, mifereji ya maji ya mvua na hata kwenye vyanzo vya maji.
Chupa za Plastiki.

Ripoti mbalimbali,ikiwemo ya jarida la The Lancet,zinasema kwamba Plastiki inakadiriwa kuchangia asilimia 80 ya taka ngumu zinazomwaga baharini, lakini ni asilimia 10 pekee ndiyo huchakatwa kila mwaka.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP), Inger Andersen, amesema bila hatua za haraka, dunia yote itazama kwenye uchafuzi wa plastiki na kutabiri taka hizo kuongezeka mara tatu ifikapo mwaka 2060.
Mzee Mbunifu.

Kufuatia changamoto hiyo ya uchafuzi wa mazingira kutokana na plastiki,Mzee Sief Mahanji (67)mwenye ulemavu wa mguu mkazi wa Ndala Manispaa ya Shinyanga,mwaka 2023 aliamua kubuni kutengeneza bidhaa za mikeka kwa kutumia chupa za plastiki ambazo hutupwa hovyo mitaani.

Anasimulia kuwa yenye baada ya kukatwa mguu wa kulia kutokana na ugonjwa wa kisukari mwaka huo 2023 na kutokana na kukabiliwa na ugumu wa maisha ndipo akaja na wazo la kutengeneza bidhaa hizo za mikeka kwa kutumia chupa za plastiki ili ajipatie kipato na kutunza mazingira.

Anasema,hua anakusanya chupa hizo za Plastiki katika maeneo mbalimbali yenye mikusanyiko ya watu ikiwamo stendi za mabasi ambazo hutupwa hovyo, na kutumia malighafi hiyo kutengeneza bidhaa hizo za mikeka na kumpatia kipato.

“Mimi nina familia ya watoto tisa,kwa sasa maisha yangu naendesha kupitia kutengeneza mikeka kwa kutumia chupa za plastiki, sababu malighafi hii inapatikana kwa urahisi na pia inasaidia kutunza mazingira kwa kupunguza taka ngumu mitaani,” anasema Mahanji.

Anasema soko la mikeka hiyo lipo kwa wingi na hua anaiuza kwenye taasisi mbalimbali zikiwamo shule binafsi na misikiti, ambapo huuza kwa bei ya shilingi 40,000 kwa mkeka mmoja.

Anaongeza kuwa biashara hiyo imekuwa ikimsaidia kuendesha maisha yake pamoja na kuwatumizia mahitaji ya shule watoto wake pamoja na wajukuu.

Mke wa Seif

Lemida Hussein,ambaye ni mke wa Seif, anasema kwamba mradi huo wa utengenezaji mikeka, umesaidia kubadilisha hali ya maisha yao baada ya mumewe kukatwa mguu na kuacha kufanya biashara katika soko kuu.

Anasema, baada ya mumewake kukatwa mguu maisha yao yalibadilika na kuwa magumu,na hivyo kuishi kwa kutengemea kibanda chake cha kuuza matunda soko ambacho kilikuwa hakikidhi mahitaji yote ya nyumbani.

"utengezaji huu wa mikeka umesaidia kuongeza kipato na kuboresha maisha yetu na hata kusomesha watoto,"anasema Lemida.

Mtoto wa Seif.

Farihia Seif Mahanji ni miongoni mwa watoto wa mzee huyo, anasema kuwa biashara hiyo ya mikeka imewasaidia katika kuwatimizia mahitaji yao ya shule na mahitaji ya nyumbani.

Anasema yeye kwa sasa ana soma kidato cha nne katika shule ya sekondari Ndala, na kwamba Baba yake licha ya kupata ulemavu na kubuni biashara hiyo ya utengenezaji wa mikeka kwa kutumia chupa za Plastiki maisha yao hayajateteleka bali wanaisha kama hapo awali.

Mteja.

Shaban Ally ambaye ni miongoni mwa wateja ambao wamewahi kununua mkeka kwa mzee Seif,anasema bidhaa mikeka hiyo ni imara na haiozi,na kumpongeza mzee huyo kwa kujishughulisha na kwamba ingekuwa mtu mwingine amepata ulemavu ange anza kuwa omba omba.

Mkurugenzi wa Manispaa.

Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga Alexius Kagunze, anampongeza mzee Seif ambaye ni mlemavu kwa ubunifu huo, akisisitiza kuwa ni mfano wa kuigwa katika kulinda mazingira kupitia urejelezaji wa taka.

Anasema kuwa, uongozi wa manispaa utaendelea kushirikiana na wananchi wabunifu kama Mahanji, kwa kuhakikisha wanasimamiwa na kuunganishwa na masoko ili kunufaika zaidi, huku akiwasisitiza wananchi wengine kuiga mfano huo wa ubunifu kwa maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla.

Anaongeza kuwa ,kutokana na ubunifu huo wa utunzaji wa Mazingira, umesababisha hata Manispaa ya Shinyanga kushika nafasi ya pili Kitaifa kati ya Halmashauri 20 za Manispaa nchini, kwenye mashindano ya Afya na Usafi wa Mazingira kupitia Wizara ya Afya mwaka jana 2024.
“Ushindi huu wa usafi wa mazingira,unatokana na juhudi za wananchi kwa kutuunga mkono kutunza mazingira, akiwamo na huyu mzee kwa kubuni utengenezaji wa mikeka kwa kutumia chupa za plastiki,chupa ambazo mara nyingi huzagaa mitaani na kuchafua mazingira,”anasema Kagunze.

Anasema, mikakati ya Serikali ni kuendelea kutunza Mazingira na kwamba wameweka Wakala ambaye hua anazunguka na gari kwa ajili ya kukusanya taka mitaani, na kuwasihi wananchi waache kutupa taka hovyo bali waweke kwenye vyombo maalumu ambavyo vimeweka barabarani na maeneo yote yenye mikusanyiko ya watu.

Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ukurasa 39, inasema kwamba ilikukabiliana na uchafuzi wa mazingira, Tanzania imechukua hatua kwa kutunga sera, sheria na mikakati mbalimbali ili kupambana na uchafuzi huo wa mazingira na kwamba Hatua hizo zinajumuisha kushirikisha jamii, sekta binafsi, na taasisi za serikali katika kulinda mazingira kwa kizazi cha sasa na kijacho.

Matarajio ya Dira hiyo kwa upande wa Mazingiira inasema, ni kuwa na Jamii yenye uelewa mkubwa wa athari za uchafuzi wa mazingira ili kuwa na mazingira salama na endelevu kwa wote, Majiji na miji yenye miundombinu na usimamizi bora wa taka na ujenzi unaozingatia uhifadhi wa mazingira.

Matarajio mengine ni kuwa na taifa kinara katika matumizi endelevu ya rasilimali na linalotumia taka kama malighafi kwa manufaa ya kiuchumi na taifa lenye mazingira stahimilivu linalosimamia vyema maliasili kwa maendeleo.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464