Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Zanzibar (TAMWA-ZNZ) kimefanya mkutano wa kutoa mrejesho wa utekelezaji wa programu ya mapitio ya sheria za habari na uhuru wa habari, kwa kuwashirikisha wadau mbalimbali wa sekta ya habari visiwani Zanzibar.
Mkutano huo umefanyika katika ofisi za TAMWA-ZNZ zilizopo Mkanjuni, Chake Chake -Pemba, na uliwaleta pamoja waandishi wa habari, wanaharakati wa vyombo vya habari, wawakilishi wa asasi za kiraia, na wadau wa maendeleo kwa lengo la kujadili mafanikio na changamoto zilizojitokeza katika utekelezaji wa programu hiyo kwa kipindi cha mwaka 2024-2025.
Akizungumza wakati wa kufungua mkutano huo, Afisa Ufuatiliaji na Tathmini kutoka TAMWA, ZNZ, Mohammed Khatib, alisema kuwa mkutano huu ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha uwazi, ushirikishwaji na kuimarisha sauti ya wanahabari katika mchakato wa mabadiliko ya sheria za habari.
“Kwa kipindi chote cha utekelezaji wa programu hii, tumeweza kufikia hatua muhimu katika kuhamasisha majadiliano ya kina kati ya waandishi na wadau wa habari na watoa maamuzi. Ripoti tunayowasilisha leo inaonesha hali halisi, mafanikio, lakini pia maeneo yanayohitaji maboresho,” alisema Mohammed Khatib, Afisa Ufuatiliaji na Tathmini.
Akiwasilisha ripoti hiyo, afisa program wa mapitio ya sheria za habari na uhuru wa habari kutoka TAMWA-ZNZ Zaina Mzee, ilieleza kuwa juhudi za ushawishi zilizofanywa, ikiwa ni pamoja na mikutano na baadhi ya Wawakilishi wa Baraza la Wawakilishi, mafunzo kwa wanahabari kuhusu sheria za habari, na kampeni za uelimishaji kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.
Sambamba na hilo, programu hii iliwawezesha waandishi 25 kutoka Unguja na Pemba kupata mafunzo ya kina juu ya namna ya kuchambua na kuripoti sheria za habari, hasa zile zenye vifungu vinavyobinya uhuru wa vyombo vya habari.
Nao washiriki wa mkutano huo walitoa maoni na mapendekezo ya kuboresha ripoti, huku wengi wakisisitiza umuhimu wa kuwa na sheria mpya ya habari inayolinda uhuru wa vyombo vya habari, haki za waandishi, na uwajibikaji wa kitaaluma.
Pia walieleza jinsi mafunzo hayo yalivyowawezesha kubadili mitazamo yao kiuandishi. “Kwa mara ya kwanza tumeelewa kwa undani jinsi sheria za habari zinavyoweza kuathiri uhuru wetu wa kuripoti. Mafunzo haya yametupa ujasiri wa kuuliza maswali mbalimbali kwa viongozi bila woga, kwa sababu sasa tumeelewa haki zetu kama mwanahabari,” .
Aidha walisisitiza pia umuhimu wa kuendelea kushirikiana kama wadau na kuendeleza uchechemuzi ili kuharakisha mchakato wa upatikanaji wa sheria mpya, kwa kuzingatia mazingira ya sasa ya kidijitali na changamoto zinazowakumba waandishi wa habari Zanzibar.
Kwa ujumla, mkutano huo umeonesha dhamira ya pamoja kati ya wanahabari na wadau wa maendeleo katika kuendeleza mchakato wa kupata sheria mpya ya habari Zanzibar. Kupitia ushirikiano endelevu na mijadala ya wazi, sekta ya habari inaendelea kuchukua nafasi muhimu katika kulinda haki ya kupata taarifa na kuhimiza uwajibikaji katika jamii.