
Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga amabaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya lishe Wilayani humo Bw. Tano John Malele akizungumza Julai 16, 2025 katika kikao maalum cha kujadili Taarifa za utekelezaji wa afua za lishe kwa kipindi cha robo ya nne (Aprili - Juni) mwaka wa fedha 2024/2025, kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo
Na Sumai Salum, Kishapu
Msimamo wa Wilaya ya Kishapu kuhusu umuhimu wa lishe Shuleni umeendelea kuimarika, huku viongozi wakihimiza usimamizi madhubuti wa afua za lishe kama silaha ya kupambana na utoro na kuongeza ufaulu kwa wanafunzi wa Shule za Msingi na Sekondari.
Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga Bw. Tano John Malele, ambaye pia ni Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Kamati ya Lishe ya Wilaya hiyo amesema wakati wa kikao cha tathmini ya utekelezaji wa afua za lishe kilichofanyika Julai 16, 2025 Katika ukumbi wa Halmashauri ya Kishapu amesema lishe si jambo la hiari bali ni msingi wa maendeleo ya elimu.
“Serikali ya awamu ya sita imetoa kipaumbele kwa watoto kupata chakula mashuleni. Hatutarajii kuona shule yoyote haina uji au chakula cha mchana kwa wanafunzi wa sekondari katika robo ijayo,” ameisitiza Malele mbele ya wajumbe wa kikao hicho.
Katika hotuba yake, Bw. Malele amewakumbusha Watendaji wa Kata na Vijiji kuwa wao ni kielelezo kwa jamii, hivyo ni muhimu wakajitokeza mbele kwa kuhamasisha wananchi kuchangia chakula cha wanafunzi huku wakianza wao kutoa.
Amewataka wasimamizi wa chakula shuleni kuwa waaminifu katika utekelezaji wa majukumu yao kama sehemu ya kuthamini juhudi za serikali na wananchi.
Mtendaji wa Kata ya Mwamashele ametunukiwa zawadi ya fedha taslimu kutokana na utekelezaji mzuri wa afua za lishe, pamoja na mwandishi wa vikao na mtumishi kutoka shirika la World Vision kwa mchango wao muhimu.
Afisa Maendeleo ya Jamii wa Wilaya ya Kishapu, Bw. Joseph Swalala, amewahimiza watendaji kuendelea kutoa elimu kuhusu lishe bora katika ngazi ya jamii akisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya watendaji, jamii na wadau wa maendeleo kama nguzo ya mafanikio ya afua za lishe.
Naye Afisa Lishe wa Wilaya, Bi. Hadija Ahmed Nchakwi, ameeleza kuwa jitihada za serikali zimeanza kuzaa matunda hasa katika kupunguza viwango vya udumavu kwa watoto walio na umri chini ya miaka mitano pamoja na wajawazito.
“Jamii imeanza kuelewa umuhimu wa lishe. Hata wajawazito wanaokuja kliniki, hali zao zinaonyesha mabadiliko chanya. Changamoto kubwa iliyobaki ni kuhakikisha kila shule inatekeleza kikamilifu mpango wa lishe,” amesema Bi. Nchakwi.
Kwa mujibu wa taarifa za kikao hicho, Wilaya ya Kishapu ina jumla ya shule 168 za msingi na sekondari. Katika robo ya tatu, shule 152 (sawa na asilimia 90.5%) zilikuwa zinatoa chakula kwa wanafunzi, na robo ya nne idadi hiyo ilipanda hadi asilimia 97.62%.
Jumla ya taarifa tisa zimewasilishwa kutoka Idara mbalimbali ikiwemo Afya, Elimu Awali na Msingi, Elimu Sekondari, Kilimo,Mifugo na Uvuvi,Maendeleo ya Jamii, RUWASA, na Redeso, pamoja na wawakilishi wa madhehebu ya Kiislamu.
Taarifa hizo zimeeleza hatua zilizopigwa na mapendekezo ya kuimarisha zaidi utekelezaji wa afua za lishe.
Kikao hicho kimedhihirisha kuwa mafanikio katika elimu hayategemei tu vitabu na walimu, bali pia hali ya lishe ya wanafunzi. Hivyo, kuweka mkazo katika lishe bora si tu kuongeza ufaulu, bali pia ni hatua muhimu ya kulinda afya, kupunguza udumavu katika jamii.
Afisa lishe Wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga Hadija Nchakwi akizungumza Julai 16, 2025 katika kikao maalum cha kujadili taarifa za utekelezaji wa afua za lishe kwa kipindi cha robo ya nne (Aprili - Juni) mwaka wa fedha 2024/2025, kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo
Afisa Maendeleo ya Jamii Wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga Joseph Swalala akizungumza Julai 16, 2025 katika kikao maalum cha kujadili taarifa za utekelezaji wa afua za lishe kwa kipindi cha robo ya nne (Aprili - Juni) mwaka wa fedha 2024/2025, kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo




















Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464






















