RC Mhita Atoa Maelekezo ya Maendeleo kwa Watumishi wa Halmashauri ya Msalala
Na RS Shinyanga
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita,amefanya ziara ya kikazi katika Halmashauri ya Wilaya ya Msalala, ambapo amekutana na kuzungumza na watumishi wa halmashauri hiyo ambapo ametoa maelekezo mahsusi ya namna wanavyopaswa kuwahudumia wananchi ili kuharakisha maendeleo ya mkoa huo.
Katika kikao hicho, Mhe. Mhita amesisitiza kwamba maendeleo ya mkoa wa Shinyanga hayawezi kupatikana bila watumishi kuwajibika kwa uadilifu, kutekeleza majukumu kwa kufuata sheria na miongozo ya serikali, pamoja na kusikiliza na kutatua kero za wananchi kwa wakati.
Ameeleza kuwa ni muhimu kwa halmashauri kuepuka matumizi mabaya ya mapato ya ndani, kuhakikisha upatikanaji sahihi wa taarifa za mapato na matumizi, na kuweka mikakati madhubuti ya kuziba mianya ya upotevu wa mapato. Kadhalika, amehimiza uongozi wa halmashauri kuongeza ubunifu wa kutafuta vyanzo vipya vya mapato ili kuongeza uwezo wa kifedha wa halmashauri katika kutekeleza miradi ya maendeleo.
Katika kikao hicho, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Msalala, Bi Rose Manumba, amempongeza Mhe. Mhita kwa kuteuliwa na Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, huku akiahidi kutekeleza kwa vitendo maelekezo yote yaliyotolewa kwa kushirikiana na watumishi wa halmashauri hiyo.
Aidha, Mhe. Mhita alitumia fursa hiyo kuwataka viongozi wote wa halmashauri hiyo kuendeleza hamasa kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura kwenye uchaguzi mkuu ujao, akisema hamasa hiyo inapaswa kuwa sawa na ilivyokuwa wakati wa uandikishaji wa wapiga kura, ambapo mwitikio ulikuwa mkubwa.
Ziara ya RC Mhita katika wilaya ya Msalala ni mwendelezo wa dhamira yake ya kufuatilia utekelezaji wa majukumu ya serikali katika halmashauri zote na kuhakikisha huduma kwa wananchi zinaimarika.
Baada ya kikao hicho Mhe. RC Mhita alifanya ziara ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa katika halmashauri hiyo.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464