` RC MBONI ARIDHISHWA NA UTEKELEZAJI WA MIRADI YA MAENDELEO HALMASHAURI YA USHETU, WILAYANI KAHAMA

RC MBONI ARIDHISHWA NA UTEKELEZAJI WA MIRADI YA MAENDELEO HALMASHAURI YA USHETU, WILAYANI KAHAMA

MKUU WA MKOA WA SHINYANGA ARIDHISHWA NA UTEKELEZAJI WA MIRADI YA MAENDELEO HALMASHAURI YA USHETU, WILAYANI KAHAMA

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, ameendelea na ziara yake ya kikazi katika wilaya za mkoa huo kwa lengo la kujionea hatua ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo, ambapo ametembelea Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu na kupongeza juhudi kubwa zinazofanywa katika kusimamia miradi inayogusa maisha ya wananchi moja kwa moja.

Katika ziara hiyo, Mhe Mboni ametembelea miradi kadhaa ikiwemo ujenzi wa Shule ya Msingi Igwamanoni inayolenga kupunguza msongamano wa wanafunzi na kuongeza upatikanaji wa elimu bora kwa watoto wa vijijini. Aidha, alikagua ujenzi wa mashine za kuchakata mazao ya kilimo ikiwa ni hatua ya kuwawezesha wakulima kuongeza thamani ya mazao yao na kukuza uchumi wa kaya.

Vilevile, Mkuu huyo wa Mkoa alitembelea Kituo cha Afya Bulugwa ambako ujenzi wa wodi ya wazazi unaendelea. Mradi huo unatarajiwa kuboresha huduma za afya ya mama na mtoto kwa kupunguza umbali wa kufuata huduma hizo. Miradi mingine ni pamoja na upandaji miti kwa ajili ya uhifadhi wa mazingira, ujenzi wa tanki kubwa la maji na mtandao wa usambazaji maji safi na salama katika maeneo ya vijijini, pamoja na ujenzi wa shule mpya ya Amali ambayo itasaidia kuwapa vijana elimu ya ufundi na kuwajengea uwezo wa kujiajiri.

Akizungumza baada ya kutembelea miradi hiyo, Mhe. Mboni amesema ameridhishwa na kasi ya utekelezaji wa miradi hiyo, usimamizi wake na jinsi inavyolenga kuboresha maisha ya wananchi. Amewapongeza viongozi na watendaji wa halmashauri ya Ushetu kwa kushirikiana na wananchi kuhakikisha miradi hiyo inatekelezwa kwa viwango na ndani ya muda.

Aidha, Mhe. Mboni amehimiza usimamizi madhubuti wa miradi yote ya serikali ili kuhakikisha rasilimali zinazotolewa zinatumika kwa uaminifu na kuleta tija kwa wananchi. Ameongeza kuwa ni muhimu kwa wananchi kushiriki kikamilifu katika kutunza miundombinu hiyo ili idumu na kuendelea kutoa huduma kwa vizazi vijavyo.

“Mkoa wa Shinyanga una fursa kubwa ya maendeleo, ni wajibu wetu wote kuhakikisha tunazitumia kikamilifu. Halmashauri ya Ushetu imeonyesha mfano mzuri kwa usimamizi wa miradi, tunataka kuona kila halmashauri inakwenda kwa kasi hii,” amesema Mhe Mboni.

Ziara ya mkuu huyo wa mkoa ni sehemu ya utaratibu wa kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuhimiza uwajibikaji kwa watendaji wa serikali ili kufanikisha ajenda ya maendeleo ya Taifa.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464