` WANANCHI KISHAPU WASISITIZWA KUHIFADHI MAZINGIRA KWA VITENDO

WANANCHI KISHAPU WASISITIZWA KUHIFADHI MAZINGIRA KWA VITENDO

 

Mwakilishi wa Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga na mgeni rasmi Severini Musyangi kwenye maadhimisho ya siku ya mazingira duniani yaliyofanyika kiwilaya katika Kijiji cha Mwigumbi Kata ya Mondo Wilayani humo Juni,5,2025.Picha na Sumai Salum

Na Sumai Salum-Kishapu

Katika kuadhimisha Siku ya Mazingira Duniani, jamii ya Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga imetakiwa kuchukua hatua za dhati katika kulinda mazingira ikiwemo kupanda miti na kufanya usafi kwenye maeneo ya makazi na huduma za kijamii.

Maadhimisho hayo yalifanyika Juni 5,2025 katika Kijiji cha Mwigumbi, Kata ya Mondo, yakiongozwa na Severini Musyangi, Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu ambaye pia alikuwa mgeni rasmi wa tukio hilo.

Akizungumza na wananchi na wanafunzi wa Shule ya Msingi na Sekondari Mwigumbi Musyangi amesisitiza kuwa kila mwananchi ana wajibu wa moja kwa moja katika kulinda mazingira, huku akipendekeza mpango wa kila mwanafunzi kupanda mti mmoja kila mwanzo wa mwaka na kuuhudumia hadi unakomaa.

“Kila mwanafunzi anapaswa kupanda mti mmoja na kuuhudumia. Vivyo hivyo, kila mwananchi ahakikishe anapanda miti katika maeneo yake ya makazi na si kusubiria serikali ama mashirika yasiyokuwa ya serikali kupanda ” amesema Musyangi .

Afisa Mazingira wa Halmashauri ya Kishapu Charles Kanwakabo amesema maadhimisho ya mwaka huu yamefanyika katika eneo la Mwigumbi kutokana na wingi wa watu, hali inayochochea uwezekano wa uharibifu wa mazingira ikiwa hakuna elimu na usimamizi thabiti.

“Tumechagua Mwigumbi kwa sababu kuna msongamano wa watu Tumeweza kupanda miti 300 ya matunda na ya kivuli sambamba na kufanya usafi katika maeneo mbalimbali ya umma hivyo tunaamini kupitia ushirikiano wa jamii na maafisa wetu wa afya kuanzia ngazi ya Kijiji hadi Wilaya elimu hii itasaidia kudhibiti uharibifu wa mazingira,” amesema Kanwakabo.

Maadhimisho hayo yalihusisha ushiriki wa wananchi, viongozi wa Vijiji, wanafunzi, watumishi wa Halmashauri pamoja na wadau wa mazingira, ambapo shughuli mbalimbali za kijamii kama upandaji miti na kampeni ya kupinga matumizi ya plastiki zilifanyika.

Akizungumza kwa niaba ya wanafunzi Lidya Boniphace mwanafunzi wa darasa la saba katika Shule ya Msingi Ng’wigumbi amesema kuwa wanafundishwa masomo kuhusu mazingira shuleni ikiwa ni sehemu ya kuandaa kizazi kinachojali na kuhifadhi mazingira.

“Tumejifunza namna ya kupanda miti, nyasi na pia kuepuka matumizi ya plastiki tunajua ni jukumu letu kutunza mazingira ya sasa na ya baadaye,” amesema Lidya.

Kaulimbiu ya Mwaka 2025: “Rekebisha Ardhi kwa Mustakabali Endelevu” ikilenga kurejesha uoto wa asili, kuboresha matumizi ya ardhi, na kuhimiza jamii duniani kote kuchukua hatua za kuzuia mmomonyoko wa ardhi na mabadiliko ya tabianchi hivyo Wilaya ya Kishapu imedhihirisha kuwa kwa kutumia elimu na ushiriki wa wananchi, malengo haya yanaweza kufikiwa kwa vitendo.

Kishapu ni miongoni mwa maeneo yanayokabiliwa na changamoto ya ukame, mmomonyoko wa ardhi, na ukataji miti hovyo kwa matumizi ya kuni. Kwa hivyo, hatua ya kuhamasisha kila mwanafunzi kupanda mti ni ya kimkakati inalenga kujenga mazoea mapema ya kuhifadhi mazingira.

Aidha msisitizo kwenye elimu mashuleni kuhusu mazingira na kushirikisha jamii nzima ni hatua endelevu itakayosaidia kulinda vyanzo vya maji, kuimarisha hali ya hewa na kuzuia athari za mabadiliko ya tabianchi ambazo zimeanza kushuhudiwa pia katika mkoa wa Shinyanga.

Maadhimisho hayo yameambatana na Mgeni rasmi kutoa vyeti vya pongezi kwa wadau wa mazingira wakiwemo Wdl,Tcrs,Sinohydro, Daniel Xu, Nmb Kishapu pamoja na Crdb banc Maganzo.
Afisa mazingira wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga Charles Kanwakabo akizungumza kwenye maadhimisho ya siku ya mazingira duniani ngazi ya Wilaya yaliyofanyika Kijiji cha Mwigumbi Kata ya Mondo Wilayani humo Juni 5,2025
Baadhi ya wanafunzi wa Shule ya msingi Mwigumbi Wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga wakifanya usafi kwenye Zahati ya Kijiji hicho kwenye maadhimisho ya siku ya mazingira duniani yaliyofanyika Juni,5,2025 ngazi ya Wilaya

Baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari Mwigumbi
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464