` BAISKELI: NJIA YA MAENDELEO SHINYANGA NA AFRIKA- AFYA, ELIMU NA UKOMBOZI WA JAMII

BAISKELI: NJIA YA MAENDELEO SHINYANGA NA AFRIKA- AFYA, ELIMU NA UKOMBOZI WA JAMII

 



                                                                          Na mwandishi wetu

Usafiri wa baiskeli umeendelea kuwa chaguo maarufu kwa watu wengi barani Afrika, hususan katika mkoa wa Shinyanga, kutokana na sababu mbalimbali za kijamii, kiuchumi, na kimazingira. Uchunguzi na tafiti mbalimbali zimebainisha faida na sababu zinazowafanya watu kupendelea kutumia baiskeli kama njia kudu ya usafiri.

Siku ya Baiskeli Duniani ilitangazwa rasmi na Umoja wa Mataifa mwaka 2018 kwa kutambua mchango mkubwa wa baiskeli kama chombo muhimu cha usafiri salama, rafiki wa mazingira, na nafuu kwa watu wa matabaka yote duniani.

 Baiskeli imejidhihirisha kuwa nyenzo ya maendeleo endelevu kwa kusaidia watu wengi kufikia huduma za afya, kupata elimu kwa wakati, kufanya biashara ndogondogo, na kuimarisha uhusiano wa kijamii hasa katika maeneo ya vijijini. 

Kwa sababu hiyo, siku hii huadhimishwa kila mwaka tarehe 3 Juni kwa lengo la kuhamasisha matumizi ya baiskeli kama suluhisho la changamoto za kijamii, kiuchumi, na kimazingira duniani kote.

Sababu za watu kupendelea usafiri wa baiskeli.

Gharama Nafuu na Upatikanaji Rahisi
Baiskeli imeendelea kuwa chaguo linalopendwa sana kutokana na unafuu wake katika ununuzi na uendeshaji. Tofauti na magari au pikipiki, baiskeli haihitaji mafuta wala bima, na vipuri vyake hupatikana kwa urahisi sokoni kwa bei ndogo. Watu wengi pia wana ujuzi wa kuzitengeneza wenyewe, jambo linaloongeza ushawishi wa kutumia chombo hiki, hasa kwa familia zenye kipato cha chini na cha kati.

Ufikiaji rahisi wa maeneo ya Vijijini
Katika mkoa wa Shinyanga, ambao una maeneo mengi ya vijijini yenye barabara zisizopitika kirahisi, baiskeli imekuwa suluhisho madhubuti. Kwa uwezo wake wa kupenya katika barabara za vumbi, matope, na hata milima midogo, wananchi wameweza kufika kwa haraka kwenye masoko, zahanati, au shule bila kutegemea usafiri wa magari, ambao si rahisi kupatikana kila wakati.

Chombo cha kujikwamua kiuchumi
Kwa wakazi wa Shinyanga na maeneo mengine ya Afrika, baiskeli si tu usafiri bali ni zana ya kujipatia kipato. Inatumika kubeba mazao kutoka shambani hadi sokoni, kusambaza bidhaa za biashara ndogondogo, au kama boda-boda za miguu kwa abiria. Hii imewasaidia wakazi wengi kuanzisha shughuli za kujiajiri, kuongeza mapato na kuboresha maisha yao ya kila siku.

 Kuwezesha elimu, afya na utunzaji wa Mazingira
Kupitia miradi Bike2School, wanafunzi—hasa wasichana—wamewezeshwa kupata baiskeli, jambo lililopunguza muda wa kwenda shule, kuongeza usalama na kuboresha mahudhurio. Aidha, kuendesha baiskeli ni zoezi bora la mwili, linalosaidia afya na kupunguza magonjwa yasiyoambukiza. Kwa upande wa mazingira, baiskeli hazitoi moshi wala kelele, hivyo huchangia katika kupunguza uchafuzi wa hewa mijini na vijijini.

Mkoa wa Shinyanga kwa nyakati tofauti umenufaika kwa nguvu za wadau mbalimbali waliowezesha kutoa misaada ya baiskeli kwa ajili ya kusaidia makundi mbalimbali kwa malengo tofauti ikiwa ni pamoja na  :                   

Uwezeshaji wa Jamii Kupitia elimu na haki za watoto
Kupitia ufadhili wa Oxfam Tanzania, shirika la Kivulini lilitoa msaada wa baiskeli 50 na pikipiki 4 kwa taasisi mbalimbali za serikali katika halmashauri za Shinyanga na Kishapu. Msaada huo uliwalenga watendaji wa kata, Jeshi la Polisi (Dawati la Jinsia na Watoto), pamoja na Maafisa Maendeleo ya Jamii kwa lengo la kusaidia katika utoaji wa elimu na ufuatiliaji wa mashauri ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto, hususan mimba na ndoa za utotoni. Hii ni hatua muhimu katika kulinda haki za watoto na kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa sheria kwenye jamii.

Kuwezesha vijana kupambana na maambukizi ya VVU
Family Health International (FHI 360), kupitia mradi wake wa EPIC, ilitoa baiskeli 242 kwa wawezeshaji uchumi waliopo kwenye halmashauri tano za mkoa wa Shinyanga. Baiskeli hizo ziliwasaidia wawezeshaji hao kuwafikia wasichana balehe na wanawake vijana walioko maeneo ya mbali, kwa lengo la kuelimisha na kupunguza maambukizi ya VVU/UKIMWI. Msaada huu umechangia kwa kiasi kikubwa katika kampeni za afya ya jamii na kuhamasisha uelewa kuhusu afya ya uzazi.

Kuboreshwa kwa huduma za afya ngazi ya Jamii
World Vision Tanzania kwa kushirikiana na Kivulini, walitoa baiskeli 73 kwa watoa huduma za afya katika maeneo ya vijijini. Msaada huu uliwezesha wahudumu wa afya kuwafikia kwa urahisi watu walioko katika maeneo yaliyo mbali na vituo vya afya, hivyo kurahisisha utoaji wa huduma kama chanjo, ushauri wa lishe, na ufuatiliaji wa afya ya mama na mtoto. Hili limeongeza usawa wa upatikanaji wa huduma za afya kwa jamii zisizokuwa na miundombinu ya usafiri wa uhakika.

 Uwezeshaji kwa watu wenye ulemavu
Mbunge wa Shinyanga Mjini na Naibu Waziri Patrobas Katambi alitoa msaada wa baiskeli sita zenye magurudumu matatu, fimbo nyeupe 20, na magongo 16 kwa watu wenye ulemavu kupitia SHIVYAWATA. Lengo la msaada huu lilikuwa ni kuwawezesha watu wenye ulemavu kushiriki kikamilifu katika shughuli za kila siku, kujitegemea, na kupata fursa zaidi za kijamii na kiuchumi. Hii ni hatua ya kuimarisha ushirikishwaji wa watu wenye mahitaji maalum katika maendeleo ya jamii.

Hata hivyo ,zimekuwepo nukuu maarufu kuhusu usafiri wa baiskeli kwa muda mrefu kutokana  thamani na umuhimu wa chombo hiki .Baadhi ya nukuu ambazo za muda mrefu ni pamoja na

Baiskeli huchangia kuboresha maisha nchini Tanzania. Kwa baiskeli, watu wanakuwa na afya bora, wanatembea zaidi, wanapata elimu na kuunganishwa zaidi.”Hans Harrison, Meneja wa Arusha Bicycle Company

Baiskeli husaidia wasichana kwenda shule na kumaliza elimu yao. Hii huongeza nafasi zao za kuweza kuunda maisha yao wenyewe na kuyaongoza kwa uhuru.”
Marlen Reusser, mwanariadha na balozi wa Velafrica

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464