` TAF, GLOBAL FUND FOR WOMEN WANUFAISHA 300+ TAMASHA LA HEDHI VINGUNGUTI

TAF, GLOBAL FUND FOR WOMEN WANUFAISHA 300+ TAMASHA LA HEDHI VINGUNGUTI

 

Zaidi ya wananchi 300, wakiwemo vijana na wazazi, wamehudhuria na kunufaika na tamasha la wazi lililoandaliwa na shirika la Theatre Arts Feminists kwa msaada kutoka Global Fund for Women, katika viwanja vya Sinai, Vingunguti – Wilaya ya Ilala Jijini Dar es salaam, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Hedhi Duniani.

Tamasha hilo limeambatana na burudani ya ngoma za asili, mechi ya mpira wa miguu kwa wasichana ambapo jezi zilitolewa, pamoja na igizo la jukwaani lililobeba ujumbe mzito kuhusu afya ya uzazi na usafi wa hedhi. Igizo hilo lilizua mijadala ya wazi na ya kina miongoni mwa washiriki kuhusu changamoto zinazowakabili wasichana na wanawake, ikiwemo mimba za utotoni na hatari ya utoaji mimba usio salama.

Lengo kuu la tamasha hilo lilikuwa kuelimisha jamii kuhusu ongezeko la mimba za utotoni na kuhamasisha mazungumzo ya wazi kuhusu usafi wa hedhi na afya ya uzazi. Kupitia sanaa, washiriki walielezwa kuhusu chanzo cha changamoto hizo – kama vile unyanyapaa, upungufu wa elimu sahihi, na shinikizo la kijamii linalowakumba vijana.

“Tumejifunza mengi kuhusu afya ya uzazi na umuhimu wa kuzungumza masuala haya majumbani mwetu. Tukio hili limefungua macho ya wengi,” amesema mmoja wa wazazi waliokuwepo.

Tamasha hilo pia lilipambwa na uwepo wa viongozi wa mtaa akiwemo Mwenyekiti na Afisa Mtendaji ambao walionesha kuunga mkono kwa dhati jitihada hizi zinazochochea mabadiliko chanya katika jamii.

Mradi huu ni sehemu ya juhudi endelevu za Theatre Arts Feminists kupitia kampeni yao ya “Sanaa na Uzazi Salama”, inayotumia nguvu ya sanaa kama chombo cha mabadiliko ya kijamii, hasa katika masuala yanayowahusu wasichana na wanawake.

#SikuYaHedhiDuniani #AfyaYaUzaziKwaWote #MimbaZaUtotoni #HedhiSalama #SanaaNaUzaziSalama #TheatreArtsFeminists #SanaaKwaMabadiliko
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464