Na Neema Nkumbi - Kahama
Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Mhe. Mboni Mhita, amefungua Kongamano la Kitaifa la Afya ya Akili linalofanyika kwa siku mbili katika Manispaa ya Kahama, mkoani Shinyanga, likilenga kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa afya ya akili na kuweka mikakati madhubuti ya kuboresha huduma hizo nchini.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kongamano hilo leo Mei 30, 2025, Mhe. Mhita ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kuitambua Wilaya ya Kahama kama mwenyeji wa kongamano hilo muhimu.
Amesema kuwa fursa hiyo itasaidia wataalamu, watunga sera na wadau mbalimbali kujadili kwa kina changamoto na fursa zilizopo katika sekta ya afya ya akili nchini.
"Elimu ya afya ya akili ni muhimu sana katika jamii. Natoa rai kwa washiriki kuhakikisha kuwa baada ya kongamano hili, elimu hiyo inaendelea kutolewa kwa wananchi katika ngazi ya familia na jamii kwa ujumla," amesema Mhe. Mhita.
Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Mhe. Mboni Mhita
Amebainisha kuwa Mkoa wa Shinyanga kupitia Wilaya ya Kahama tayari umeanza ujenzi wa jengo maalumu kwa ajili ya kuwasaidia waraibu wa dawa za kulevya na watu wenye matatizo ya afya ya akili.
Ameongeza kuwa mkoa huo tayari una vituo viwili jumuishi (One Stop Center) vinavyotoa huduma hizo, vyote vikiwa katika Wilaya ya Kahama.
Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Afya, Jenista Mhagama, Mhe. Mhita amesema serikali imetenga Shilingi milioni 300 kwa ajili ya ujenzi wa kituo maalum cha kusaidia waraibu wa dawa za kulevya ambao ni sehemu kubwa ya waathirika wa matatizo ya afya ya akili.
Mkurugenzi wa Shirika la WAYDS Charles Deogratius
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Shirika la Women and Youth Development Solution (WAYDS), Charles Deogratius – ambaye pia ni Mratibu wa kongamano hilo kwa mwaka 2025 amesema kuwa afya ya akili ni nguzo muhimu ya maendeleo ya binadamu na kwamba bila ustawi wa akili hakuna maendeleo ya taifa.
“Afya ya akili ni msingi wa maendeleo. Hatutaweza kufikia maendeleo hayo bila sera bora, takwimu sahihi na ushirikiano wa pamoja kutoka kwa wadau wote,” amesema Deogratius.
Kamishna Msaidizi kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watu Wenye Ulemavu, Bi. Tulo Masanja, alisema kuwa majanga kama mafuriko, ajali na migogoro ya kifamilia huathiri sana afya ya akili. Alisema wizara yake kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu inaandaa miongozo ya kitaifa ya kutoa huduma za afya ya akili wakati wa majanga.
“Tunahakikisha kila mwananchi anapata msaada wa haraka na kwa mujibu wa sheria za taifa katika kipindi cha majanga,” amesisitiza Tulo.
Dkt. Yudas Ndungile
Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dkt. Yudas Ndungile, amehimiza jamii kujitokeza kupata elimu na ushauri wa kisaikolojia ili kusaidia kupunguza matukio ya kujiua, mauaji na matumizi ya dawa za kulevya – sababu kuu za matatizo ya akili.
Afisa Habari wa Hospitali ya Mirembe, Christian Elias, ameeleza kuwa vijana wenye umri wa miaka 18 hadi 35 ndio waathirika wakuu wa matatizo ya afya ya akili kutokana na msongo wa mawazo, changamoto za kiuchumi, na matumizi ya dawa za kulevya.
Katika ushuhuda wa kusisimua, kijana Rehema Hussein amesimulia jinsi alivyokumbwa na ugonjwa wa akili baada ya manyanyaso ya ndoa, hali iliyomfikisha kwenye hatua ya kutaka kujiua pamoja na mtoto wake wa miezi minne.
“Nilipata msaada kutoka kwa dawati la jinsia polisi na baadaye vikundi vya vijana vilinisaidia kujitambua na kupona,” amesema kwa hisia.
Kongamano hilo linatarajiwa kutoa dira mpya ya kitaifa kuhusu afya ya akili na kuhamasisha uwekezaji wa rasilimali zaidi katika huduma za kisaikolojia, hasa kwa vijana ambao ndio kundi kubwa lililo hatarini.