` CPA. MAKALLA AIPONGEZA SERIKALI KWA MAENDELEO KISHAPU

CPA. MAKALLA AIPONGEZA SERIKALI KWA MAENDELEO KISHAPU


Na Sumai Salum – Kishapu

Katibu wa NEC - Itikadi, Uenezi na Mafunzo CCM Taifa, CPA. Amos Makalla ameipongeza Serikali kwa kuendelea kusogeza huduma muhimu za kijamii kwa wananchi wa Wilaya ya Kishapu, mkoani Shinyanga.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika Mei 23, 2025, katika Kata ya Maganzo wakati wa ziara ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Cpa. Makalla amesema kuwa Serikali imetekeleza kwa vitendo ahadi zake kwa wananchi wa Kishapu, hususan katika sekta ya maji.

“Nilipokuwa Naibu Waziri wa Maji, nilipokea kilio kikubwa kutoka kwa wananchi wa Kishapu kuhusu changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama.

Leo hii Serikali imetenga mabilioni ya fedha kutatua changamoto hiyo jambo linaloleta matumaini na maendeleo kwa wananchi,” amesema Makalla.

Ameongeza kuwa Wilaya ya Kishapu imeendelea kuimarika kimaendeleo kwa kasi kubwa na kwamba wananchi wake wanaonesha bidii ya dhati katika kuchangia maendeleo yao.
“Kishapu niliyoiona miaka michache iliyopita siyo hii ya leo. Mji wa Maganzo umekua, watu wameongezeka, na shughuli za kiuchumi na biashara zimeimarika sana,” amesema.

Katika kuonesha kutambua mchango wa wananchi CPA. Makalla amewataka waendelee kuiamini Serikali na kujitokeza kwa wingi katika uchaguzi mkuu ujao mwezi Oktoba kwani ni haki yao ya kikatiba.

Mbunge wa Jimbo la Kishapu Mhe. Boniface Butondo ameeleza mafanikio yaliyopatikana katika sekta mbalimbali ndani ya kipindi cha miaka minne akisisitiza kuwa Serikali imewekeza zaidi ya shilingi bilioni 3 katika elimu ambapo zaidi ya madarasa 210 yamejengwa katika shule za msingi na yote yamewekewa madawati.

“Katika Kata ya Maganzo tumefanikisha ujenzi wa kituo cha watoto wenye mahitaji maalum kwa gharama ya zaidi ya shilingi milioni 220, na kituo hicho kinaendelea kutoa huduma kwa mafanikio makubwa,” amesema Mhe.Butondo.
Akizungumzia huduma ya maji, Mhe. Butondo amesema kuwa mwaka 2021 ni Kata 3 tu kati ya 29 zilikuwa na huduma ya maji, lakini sasa ni jumla ya Kata 21 zina huduma hiyo kupitia miradi ya Ziwa Victoria na visima.

“Katika bajeti ijayo tumeidhinishiwa zaidi ya shilingi bilioni 16.5 kwa ajili ya kukamilisha usambazaji wa maji katika Kata za Mondo, Busangwa, Mwasubi, Bunambiyu na Sekebugolo,” ameongeza.

Kwa upande wa miundombinu amesema kuwa mtandao wa barabara umeongezeka kutoka kilomita 675 mwaka 2021 hadi kufikia kilomita 1,100 mwaka huu, huku bajeti ya barabara ikiongezeka kutoka milioni 900 hadi bilioni 2.5.

Aidha, amesema idadi ya vijiji vilivyopata umeme imeongezeka kutoka 48 hadi 117, jambo linaloonesha dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuwaletea wananchi maendeleo ya kweli.

Mbunge huyo amempongeza Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Mhe. Peter Masindi, kwa utendaji bora wa kazi na uongozi wa karibu na wananchi, huku akisisitiza kuwa mafanikio ya Halmashauri hiyo yanatokana pia na usimamizi mzuri wa Mkurugenzi Mtendaji, Bw. Emmanuel Johnson.

“Mkurugenzi wetu Bw. Emmanuel Johnson ametufikisha mbali kwa kuboresha ukusanyaji wa mapato kutoka shilingi bilioni 1.5 hadi bilioni 3.4. Tunaomba aendelee kupewa nafasi ya kuwatumikia wananchi wetu wa Wilaya ya Kishapu kwani amekuwa chachu ya maendeleo katika Halmashauri hii", amesema Mbunge Butondo.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464