Majeruhi Ajali Mgodi wa Mwakitolyo akatwa Mguu,RC Macha aonya upotoshaji utoaji taarifa juu ya tukio hilo
Na Marco Maduhu,SHINYANGA
Mmoja wa majeruhi katika Ajali ya Mgodi wa Mwakitolyo namba 8 wilayani Shinyanga Nkwabi Bugisi,amekatwa Mguu wake wa kulia kutokana na kuumia vibaya katika Ajali hiyo,huku Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha akionya upotoshaji wa taarifa za tukio hilo.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa mkoani Shinyanga Dk.Luzila John, akizungumza leo Mei 20 na Waandishi wa habari Hospitalini hapo, amesema kwamba Mei 18 majira ya saa 8 usiku, alipokea majeruhi 7 wa ajali hiyo na kuwapatia matibabu.
Amesema kwamba, Majeruhi Wanne baada ya kupatiwa matibabu waliruhusiwa kutoka Hospitali kutokana na hali zao kuwa nzuri,huku Mgonjwa Mmoja wakimpatia Rufaa ya kwenda kutibiwa Bugando Jijiji Mwanza, na Mgonjwa Mmoja Nkwabi Bugisi akikatwa Mguu.
“Sasa hivi hapa Hospitali ya Mkoa wa Shinyanga tumebaki na Wagonjwa wawili tu,na Mmoja amekatwa Mguu na wanaendelea na matibabu,”amesema Dk.Luzila.
Mmoja wa Majeruhi hao Zacharia Bachangwana, amesema kuwa siku ya tukio hilo wakati wakiendelea na shughuli za utafutaji madini, kwa kuokota mawe yadhaniwayo kuwa na dhahabu,ndipo gema la mgodi huo likaanguka na kuwafunika.
Amesimulia kuwa, baada ya kufunikiwa na gema hilo,ndipo kila mmoja akaanza kutafuta kujiokoa,huku wengine wakiwa wamekandamizwa na mawe mazito akiwamo yeye mwenyewe, na kusababisha kuumia zaidi.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha,ameonya utolewaji wa taarifa za upotoshaji juu ya tukio hilo,na kwamba masuala yanayohusu maisha ya watu siyo ya kufanyia mzaha.
Amefafanua kuwa,katika tukio hilo watu waliofukiwa katika Mgodi huo walikuwa 17,ambapo watu Sita ndiyo waliofariki dunia na kupatikana majeruhi 11, na siyo watu 150 waliofukiwa kama ilivyoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari.
Aidha,amewataja watu Sita waliofariki katika ajali hiyo, kuwa ni Ntemi Costantine,Agnes Zabroni, Mponeja Sabato,Patrick Kanizio na Haji Juma, huku mwanaume mmoja amesema hajafahamika jina lake.
Amesema kuwa Miili Mitano ya Marehemu tayari imeshatambuliwa na ndugu zao, na wameshachukuliwa kwa ajili ya mazishi kasoro mwili mmoja ambao haujatambuliwa.
Aidha,Mei 17 mwaka huu katika Mgodi wa Mwakitolyo namba 8 wilayani Shinyanga,kulitokea Maafa ya Watu 17 kufukiwa na gema la Mgodi huo na wakati wakiendelea na kushughuli za utafutaji madini, na kusababisha vifo vya watu Sita na Majeruhi 11.
TAZAMA PICHA👇👇
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha,akizungumza na waandishi wa habari.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa Shinyanga Dk.Luzila John akizungumza na waandishi wa habari.
Majeruhi Zacharia Bachangwana akizungumzia ajali hiyo.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464