WAFANYABIASHARA NDOGO SHINYANGA WAMETAKIWA KUCHANGAMKIA FURSA YA MIKOPO NAFUU YA SERIKALI
Na Marco Maduhu,SHINYANGA
Wafanyabiashara ndogo katika Manispaa ya Shinyanga wametakiwa kuchangamkia fursa ya mikopo yenye masharti nafuu na riba ndogo ya asilimia 7, inayotolewa na Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wanawake na Makundi Maalumu kwa kushirikiana na Benki ya NMB.
Wito huo umetolewa leo Mei 14, 2025, na Afisa wa Wizara hiyo, Ezekiel Philipo kutoka Kitengo cha Makundi Maalumu, wakati wa utoaji wa elimu kuhusu usajili na utambuzi wa wafanyabiashara ili waweze kupata vitambulisho vinavyowaruhusu kufaidika na mikopo hiyo.
Amesema ili kupata mikopo hiyo ambayo inatolewa na serikali,ni lazima kwanza wafanyabiashara wasajiliwe na kutambuliwa kwenye mifumo,ndipo wapate vitambulisho ambavyo vitawasaidia kupata mikopo kwa kufika Benki ya NMB na kuwekewa kwenye Akaunti zao.
“Tumefika Shinyanga kutoa elimu kwa wafanyabiashara ndogo ili wachangamkie mikopo ya serikali isiyo na dhamana, yenye riba nafuu ya asilimia 7. sharti pekee ni kuwa na kitambulisho kinachopatikana baada ya usajili rasmi,” amesema Philipo.
Aidha,amesema mara baada ya kutoa elimu hiyo ya kujisajili na kutambuliwa,kwamba wanategemea kuona idadi kubwa ya wafanyabiashara katika Manispaa ya Shinyanga wanaongezeka kupata mikopo hiyo sababu idadi bado ipo chini.
Kwa upande wake, Afisa Maendeleo ya Jamii Mkuu kutoka Wizara hiyo David Malebetho, amewataka wafanyabiashara hao kujitokeza kwa wingi kusajiliwa, akieleza kuwa hatua hiyo si tu itawasaidia kupata mikopo, bali pia itawezesha serikali kupata takwimu sahihi za wafanyabiashara ndogo kwa ajili ya kupanga maendeleo kikamilifu.
Naye Mratibu wa zoezi la usajili na utambuzi wa wafanyabiashara ndogo Mkoa wa Shinyanga Rose Tungu, ambaye pia ni Afisa Biashara wa Mkoa huo, amesema bado kuna mwitikio mdogo wa kuchangamkia mikopo hiyo licha ya kuwa na masharti rafiki.
“Serikali imeanzisha mikopo hii ili kuinua uchumi wa wafanyabiashara ndogo, lakini mwamko wa kuchukua mikopo bado ni mdogo hapa Shinyanga,” amesema Rose.
Naye Afisa kutoka Benki ya NMB Tawi la Manonga Manispaa ya Shinyanga Albini Mpona,ametaja idadi ya wafanyabiashara ndogo ambao mpaka sasa wamechangamkia mikopo hiyo na kupata pesa kuwa ni 15 tu.
Amesema mikopo hiyo inatolewa kuanzia sh.100,000 hadi Milioni 4 na hakuna dhamana.
Baadhi ya wafanyabiashara walioshiriki katika mafunzo hayo, akiwemo Tatu Ally, wameeleza kufurahishwa na elimu waliyopewa, huku wakiahidi kujisajili ili kufaidika na mikopo hiyo ya serikali, na kuondokana na mikopo yenye masharti magumu kutoka taasisi zisizo rasmi.
TAZAMA PICHA👇👇
Afisa Mipango kutoka Kitengo cha Makundi Maalumu Wizara ya Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wanawake na Makundi Maalumu Ezekiel Philipo akizungumza.
Afisa Maendeleo ya Jamii Mkuu kutoka kitengo cha Makundi Maalumu Wizara ya Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wanawake na Makundi Maalumu David Malebetho akizungumza.
Afisa Maendeleo ya Jamii kitengo cha Makundi Maalumu, Wizara ya Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wanawake na Makundi Maalumu Vaileth Mambosasa akizungumza.
Mratibu wa Usajili na utambuzi Wafanyabiashara ndogo kutoka Mkoa wa Shinyanga Rose Tungu akizungumza.
Mratibu wa Usajili na utambuzi Wafanyabiashara ndogo kutoka Mkoa wa Shinyanga Rose Tungu akizungumza.
Afisa kutoka Benki ya NMB Albini Mpona akizungumza.
Wafanyabiashara ndogo wakiwa kwenye elimu ya mikopo ya serikali yenye masharti nafuu na riba ya asilimia 7.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464