KATAMBI AANZA KUTEKELEZA KERO ZA WANANCHI KWA VITENDO KUPITIA MIKUTANO YAKE YA HADHARA,AZINDUA ZOEZI LA USAMBAZAJI UMEME AZIMIO


KATAMBI AANZA KUTEKELEZA KERO ZA WANANCHI KWA VITENDO KUPITIA MIKUTANO YAKE YA HADHARA,AZINDUA ZOEZI LA USAMBAZAJI UMEME AZIMIO

Na Marco Maduhu,SHINYANGA

MBUNGE wa Jimbo la Shinyanga Mjini Patrobas Katambi,ambaye ni Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi,Vijana,Ajira na Watu wenye ulemavu, ameanza kutekeleza kero za wananchi kwa vitendo ambazo ziliwasilishwa kwenye mikutano yake ya hadhara ya Kata kwa Kata.
Katambi leo Marchi 4,2025 amezindua zoezi la usambazaji umeme katika Mtaa wa Azimio Kata ya Lubaga, ahadi ambayo aliahidi kupitia mkutano wa hadhara alioufanya juzi kwenye Kata hiyo ambapo wananchi wa Azimio walilalamikia kutokuwa na umeme.

Akizungumza kwenye Mkutano huo wa Lubaga (juzi)aliwahidi wananchi kwamba siku ya jumanne ambayo ni leo, kuwa nguzo za umeme zitaanza kusimikwa kwenye mtaa huo ili kusambaziwa umeme majumbani mwao.
Katambi akizungumza na wananchi wa Azimio leo,amesema serikali chini ya Rais Dk.Samia Suluhu Hassan ikiahidi inatekeleza kwa vitendo, na kuwaomba wananchi waendelee kukiamini Chama Cha Mapinduzi (CCM) sababu kipo kwa maslahi ya wananchi.

"Siku ya Jumapili tukiwa kwenye Mkutano wa hadhara hapa Lubaga wananchi wa Azimio waliomba umeme, nikawahidi kwamba siku ya jumanne nguzo zitaanza kusimikwa na leo nimekuja kuzindua usimikwaji huo wa nguzo ili kusambaza umeme,"amesema Katambi.
Aidha,amesema mtandao huo wa kusambazwa huduma ya umeme katika maeneo yote utakuwa wa awamu kwa awamu, na wananchi wote watafikiwa sababu serikali ipo kazini, pamoja na utatuzi wa changamoto zote ambazo zilisalia kutekelezwa.

Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Shinyanga Mjini Anord Makombe, amesema hakuamini kama Mbunge Katambi atatekeleza ahadi hiyo ya kusambaza umeme Mtaa wa Azimio siku ya leo jumanne,lakini ameshuhudia kwa macho yake,na kumsihi aendelee kuchapa kazi na kuwatumikia wananchi.
Diwani wa Lubaga Ruben Dotto, amemshukuru Katambi kwa kutekeleza Ahadi zake kwa vitendo,na kutatua changamoto ya ukosefu wa umeme kwa wananchi wa Mtaa wa Azimio.

"Katambi unafanya miujiza ya maendeleo,yani juzi tu umeahidi leo unatekeleza,sijawahi kuona Mbunge wa namna hii wewe ni kiboko,"amesema Rubeni.
Kaimu Meneja wa TANESCO Mkoa wa Shinyanga Mhandisi Anthony Tarimo, amesema katika mwaka wa fedha 2024/2025 zimetengwa sh.bilioni 1.2 kwa ajili ya kusambaza huduma ya umeme katika maeneo mbalimbali ya manispaa ya Shinyanga ambayo hayakuwa na umeme.

Amesema katika Mtaa huo wa Azimio zitumika sh.milioni 61 kwa ajili ya kusambaza huduma za umeme kwenye makazi ya wananchi, na sasa wanaanza na zoezi la usimikaji wa nguzo kwanza,huku akimshukuru Katambi kwa kuwa nao bega kwa bega kwenye uboreshaji wa huduma.
Nao baadhi ya Wananchi wa Azimio,wamemshukuru Katambi kwa kusikiliza kilio chao cha ukosefu wa umeme na sasa tatizo linakwenda kuisha,huku wakifarijika kuona nguzo za umeme.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464