Header Ads Widget

UONGOZI WA SERIKALI KITONGOJI CHA KANGOI, WAWAPELEKA WATOTO SHULE, WALIOZUIWA NA WAZAZI.

 

UONGOZI WA SERIKALI KITONGOJI CHA KANGOI, WAWAPELEKA WATOTO SHULE, WALIOZUIWA NA WAZAZI.


 Na Mutayoba Arbogast ,Bukoba

 Ni alfajiri moja tulivu ya ya mwezi huu wa Machi 2024, shule ya msingi Kanyigo, iliyoko kata ya Kanyigo, wilayani Missenyi, mkoani Kagera, inapokea wageni wawili wa ghafla ambao hawakutarajiwa.

Robert Kolugendo, mwenyekiti wa kitongoji Kangoi, katika kijiji cha Bugombe iliko shule hiyo anawaongoza wageni hao katika ofisi ya mwalimu mkuu wa shule hiyo.

Wageni hao wawili si wengine bali watoto ambao umri wao umefika kwenda shule lakini hawajasajiliwa kwa kuwa wazazi hawakuwa tayari kuwaandikisha.

Watoto hao mmoja wa kike umri miaka 9, na mdogo wake wa kiume, umri miaka 7 (majina yao yanahifadhiwa), wanaonesha tabasamu lenye matumaini ya kupenda shule, ingawa ndoto zao zingezimwa kabisa kama uongozi wa kitongoji usingechukua hatua ya nguvu kuwalazimisha wazazi watoto hao wapelekwe shule.

Uwezekano wa kisa hiki kutokea maeneo mengine ya Tanzania ni mkubwa  kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kutokuwepo elimu ya kutosha kuhusu haki za watoto miongoni mwa wazazi na wanajamii kwa jumla.

Wazazi wa watoto hao, Mawazo Jacob  Mgenyi (35) ambaye ni mzaliwa wa wilaya ya Ngara mkoani Kagera, na mkewe Sesilia Monica James (30) mzaliwa wa wilaya ya Geita na mkoa wa Geita, walifika kata ya Kanyigo miaka mitano iliyopita, wakiwa wanahamia hapa na pale wakifanya shughuli za vibarua, na wamehamia kitongojini hapo mwanzoni mwa mwaka huu.

Familia hiyo inao watoto wanne  wanaofuatana kwa karibu, ba wale wadogo wawili wa mwisho, wanastahili kuwa wanahudhuria kliniki kwa kigezo cha umri wao, lakini bado hawapelekwi, na uongozi wa kitongoji umeanza kuchukua hatua.stahiki pia. 

Majirani wamshauri mama mzazi, ageuka mbogo; baba haonekani                                             

 Baadhi ya majirani wa familia hiyo inayoishi kwenye nyumba waliyoomba kujihifadhi, wamemweleza mwandishi wa habari hii, jinsi kwa nyakati tofauti  walivyomshauri mama wa watoto hao, kuwaandikisha shule, na pia kuwapeleka hao watoto wadogo kupata huduma za afya, lakini kila mara wamekuwa akiwajia juu kwa maneno makali makali kuwa waache kujishughulisha na mambo ya watoto wake.

 Baadhi ya majirani hao, Kasimu Kalyomunda na Fauzia Mohamed wameelezea kusikitishwa na kauli za mama na kusema kuwa Watoto hawapati malezi bora kwani  kutowafanyiwa usafi wa mwili, kumesababisha kushambuliwa sana na wadudu funza. 

 Majirani wameeleza pia kuwa baba wa watoto hao huwa haonekani mara kwa mara  hivyo mzazi pekee ambaye yuko karibu na watoto ni mama yao na ndio maana wakachukua jukumu la kumkabili mama huyo kumueleza jukumu la malezi bora ya watoto japo kuwa wanaelewa kuwa Watoto wanahitaji malezi ya wazazi wote .

"Kwa siku kama nne hivi nilimtafuta baba mzazi wa watoto hao bila kumpata ili nimpe ushauri kuhusu watoto kutokwenda shule, nikamgeukia mama watoto, katika hali ya kushangaza na kuonesha kukata tamaa, alinikasirikia akisema hayo hayamhusu", amesema jirani Kasimu Kalyomunda. 

Naye  Fauzia Mohamed ambaye ni jirani yao anasema, "Nmemshauri mara kadhaa huyu mama kuwapeleka watoto kliniki, na pia usafi wa mwli wa watoto, lakini akisema ana msongo wa mawazo kutokana na mumewe kutomsaidia katika malezi na matunzo ya familia". 

Mama watoto aeleza yanayomsibu,

 Wakihojiwa na uongozi wa kitongoji, kwa nini watoto hawapelekwi shule wala kliniki, na kudhoofika kwa watoto, Sesilia alijitetea kuwa yeye daima yuko kwenye kibarua cha kuhemea chakula na fedha ya kujikimu, hivyo asingeweza kukabiliana na michango ya shule, na anaogopa kuwapeleka watoto kliniki kwani hawana nguo  nzuri, maana baba yao amekalia ulevi tu.

 Baba wa Watoto hao, Mawazo,  alipoulizwa amekiri udhaifu wa kulewa na kutoitunza familia yake na ameahidi kubadilika ili kuleta ustawi  katika familia yake. 

"Ukweli nilikuwa nimekengeukia mno, pombe zilinitawala kupita kiasi, ila kiukweli kuona nasakwa na uongozi kama digidigi imenifedhehesha sana, Nikajiuliza mara mbilimbili, hivi kwa nini nakuwa hivi. Nimeamua kubadilika na nitajitahidi kuhakikisha naitunza familia na watoto nawatimizia mahitaji yao". 

 Mwalimu mkuu awapokea watoto hao, aipongeza jamii kwa kuguswa 

Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Kanyigo, Edwin Mugomba, amekiri kuwapokea na kuwasajili watoto  wawili wa miaka 9 na7, ingawa muda wa usajili umekwishapita na huyo mmoja yuko mbele kwa miaka miwili. 

Amewashukuru wanajamii walioguswa na watoto hao hadi kuweka msukumo wa kuletwa shuleni. 

Kwa mujibu wa kifungu cha 35 (1) cha Sheria ya Elimu ya mwaka 1978,  ilivyofanyiwa marekebisho, kila mtoto anayefikisha miaka saba na hazidi miaka 13 ni lazima aandikishwe darasa la kwanza.

Hata hivyo Maboresho ya mtaala mpya katika Sera ya elimu, kuanzia mwaka 2027 mtoto  darasa la awali akiwa na miaka 5 ( kama ilivyo sasa) na darasa la  kwanza miaka sita badala ya saba ya sasa.

Lakini bado watoto wengi nchini Tanzania, kama walivyo hao wanaozungumziwa hapo juu bado hawako shuleni kutokana na umaskini, miundombinu , kutelekezwa na wazazii nk

 Kwa mujibu wa takwimu za EMIS (Education Management Information Systems) mwaka 2016 watoto milioni 1.33(14.4%) wenye umri wa miaka saba hadi 13 na walistahili kuwa wameandikishwa shule ya msingi, hawakuwa shuleni, na Benki ya dunia (WB) inaonesha kwa mwaka 2022 wanafunzi 2,024 waliotakiwa kuwa shule ya msingi, hawakuwa shuleni.

 Pamoja na uwekezaji mkubwa wa serikali na wadau wa mendeleo katika sekta ya elimu, serikali inajitahidi kupunguza tatizo hili kadri inavyowezekana ili walengwa wafaidike na kuleta tija kwa taifa miaka ya baadaye.

  Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT-MMMAM)

Miongoni mwa hatua chanya zinazochukuliwa na serikali kwa kushirikiana na wadau, ni kuweka sheria na miongozo inayosimamiwa na kutekelezwa, kama vile Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJTMMMAM) iliyozinduliwa  mwaka 2021/22 ikitarajiwa kukamilika mwaka 2025/26.

Utekelezaji PJT-MMMAM unawaleta pamoja wadau wote wa elimu, afya, lishe, ulinzi na malezi yenye kuitikia mahitaji ya mtoto, ili kuhakikisha watoto wote kuanzia miaka 0 hadi 8 wanakua kwa utimilifu wao ili waweze kutimiza ndoto zao. Kipengele vipengele vikuu vitano vinayo leta ukuaji timilifu kwa Watoto. Na kupitia PJT-MMMAM jamii kwa ujumla inawajibika kwenye ulezi wa watoto na wanajamii wa Kanyigo wameonyesha mfano bora.

Baadhi ya watoto kutokana na sababu mbalimbali kutokana na kutowajibika,mifarakano katika ndoa, umaskini, miundombinu , kutelekezwa na wazazi nk hukosa fursa ya kuandikishwa shule kujumuika na wenzo kama hawa, shule ya msingi mojawapo wilayani Missenyi (picha kwa hisani ya mdau wa maendeleo ya elimu

 


Post a Comment

0 Comments