
Suzy Luhende,Shinyanga press blog
Mwenyekiti wa Jumuiya ya wazazi Taifa Rajabu Maganya amezitaka Jumuiya za wazazi na Jumuiya zote za CCM kuwa na miradi mbalimbali kwa ajili ya kujipatia vitega uchumi na kuondokana na ombaomba pale zinapotokea shughuli za kijumuiya.
Hayo ameyasema leo wakati akiwa kwenye ziara ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo ya jumuiya ya wazazi ikiwemo kukagua eneo la heka 50 linalotarajiwa kujengwa hospitali ya wazazi Mkoa katika manispaa ya Kahama Mkoani hapa.
Maganya ameitaka Jumuiya hiyo na wanachama wote wa chama cha mapinduzi CCM Mkoa kushirikiana katika kujenga mradi wa hospitali hiyo ya Wazazi Mkoa ili iweze kuisha kwa wakati wananchi waweze kupata huduma.
"Tunaleta hospitali katika Mkoa wa Shinyanga, na hospitali hii itajengwa na wanashinyanga wenyewe,hivyo tushirikiane tu kujenga hiyo hospitali, mimi ni mbeba maono tu, pia niziombe na jumuia zingine, tuhakikishe tunakuwa na miradi mbalimbali ili kujipatia kipato katika Jumuiya zetu lazima tuwe na vitega uchuni,"amesema Maganya.
Aidha alimshukuru mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Christina Mndeme kwa kuhakikisha kiwanja cha Jumuiya kinapatikana kwa wakati, kinachotakiwa ni kuungana kwa pamoja na kuhakikisha mradi huo unatekelezwa kwa wakati.
"Tuna miradi mingi inaendelea kutekelezeka hapa nchini ila tusiogope, kuna viwanda vya matunda Mkoa wa Tanga kiwanda cha kusindika mikonge,viwanda vya nguo,hivyo naamini tutafanikiwa tunatakiwa kuwa na uthubutu tu ili tufanye vizuri," amesema Maganya.
Kwa upande wake mwenyekiti wa Jumuiya ya wazazi Mkoa wa Shinyanga John Siagi yeye na viongozi wenzake wanashukuru sana kwa kupatiwa hospitali katikaMkoa wa Shinyanga hivyo watahskikisha wanaisimamia hospitali hiyo kwa kushirikiana na wataonyesha imani kwa vitendo.
"Nikuhakikishie mwenyekiti wangu sisi wanashinyanga hatutakuangusha tutaonyesha imani kwa vitendo katika ujenzi wa hospitali yetu hivyo tutashirikiana na kuhakikisha mradi wetu unasimama,"amesema Siagi.
Kwa upande wake kaimu katibu wa Jumuiya ya wazazi Mkoa wa Shinyanga Doris Kibabi ambaye ni katibu wa Jumuiya ya wazazi wilaya ya Shinyanga ameshukuru kwa kupatiwa hospitali hiyo na kuahidi kushirikiana katika ujenzi wa hospitali hiyo.
Aidha mwenyekiti Maganya ameambatana na wajumbe wa kamati ya utekelezaji Jumuiya ya Wazazi Taifa Edwin Nkenyenge na Mgole Miraji katika ziara ya ukaguzi wa hospitali ya wazazi inayotarajiwa kujengwa Kahama.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya wazazi Taifa Rajabu Maganya akizungumza na viongozi wa Chama na Jumuiya zake Mkoani Shinyanga

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Shinyanga John Siagi akizungumza

Mjumbe wa kamati ya utekelezaji Jumuiya ya Wazazi Taifa aliyeambatana na mwenyekiti wa Jumuiya ya wazazi Taifa Mgole Miraji





Katibu muenezi wa Chama Cha Mapinduzi CCM Mkoa wa Shinyanga Richard Masele akizungumza





Mjumbe wa baraza la Jumuiya ya wazazi Mkoa wa Shinyanga Jimotoli Maduka akizungumza











