Header Ads Widget

RC MNDEME AWEKA JIWE LA MSINGI UJENZI KITUO CHA AFYA BULIGE

RC MNDEME AWEKA JIWE LA MSINGI UJENZI KITUO CHA AFYA BULIGE

Na Marco Maduhu, KAHAMA

MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Christina Mndeme, ameweka jiwe la msingi katika ujenzi wa kituo cha Afya Bulige Halmashauri ya Msalala wilayani Kahama, huku akiagiza ujenzi huo hadi kufika Oktoba 30 mwaka huu uwe umeshakamilika na kuanza kutoa huduma za matibabu Novemba Mosi.

Ameweka jiwe hilo la msingi leo Septemba 19, 2023 ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake wilayani Kahama ya kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, pamoja na kusikiliza kero za wananchi na kuzitatua.
Akiwa katika ujenzi wa kituo hicho cha Afya Bulige, amesema hajaridhishwa na kasi ya ujenzi wake, na kuagiza iongezwe hadi kufikia Oktoba mwaka huu uwe umeshakamilika na mwezi Novemba wananchi waanze kupata huduma ya matibabu.

“Rais Samia ametoa fedha Sh,milioni 500 kujengwa kituo hiki cha Afya Bulige ili wananchi wapate huduma za matibabu karibu na makazi yao, hivyo hakuna ya kuchelewa kukimaliza sababu tupo nje ya muda, hadi kufikia Novemba Kituo hiki kikamilike na kutoa huduma ya matibabu,”amesema Mndeme.
“Wananchi zaidi ya Elfu 39 ni wengi sana ambao wanategea kupata matibabu katika Kituo hiki cha Afya Bulige, na kuagiza Mkuu wa wilaya shughulikia ujenzi huu ukamilike ili wananchi wapate huduma bora za matibabu,”ameongeza Mndeme.

Aidha, Mndeme ameagiza pia Halmashauri ya Msalala mara baada ya Kituo hicho kukamilika wafanye pia na upanuzi wa kuongeza majengo ya wodi za wagonjwa kupitia fedha za mapato ya ndani na kuboresha huduma bora za matibabu kwa wananchi.
Naye Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Bulige Dk. Catherine Peter, akisoma taarifa ya ujenzi wa kituo hicho cha Afya, amesema ulianza Februari mwaka huu na utahudumia wananchi wapatao 39,408, na sasa ujenzi wake upo katika hatua nzuri licha ya kuwa nje ya muda.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Msalala Hamis Katimba, amesema ujenzi huo ulipaswa ukamilike June huku akiahidi kutekeleza maagizo hayo ya Mkuu wa Mkoa kukamilisha ujenzi huo Oktoba 30 mwaka huu.
Nao baadhi ya wananchi wameishukuru Serikali kwa kuwajengea Kituo hicho cha Afya Bulige ambacho kitawasaidia kupata huduma ya matibabu karibu na makazi yao na kuacha tena kutembea umbali mrefu.
Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Bulige Dk. Catherine Peter.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Christina Mndeme akikagua ujenzi wa Kituo cha Afya Bulige, (kulia ni) Mkurugenzi wa Halmashauri ya Msalala Hamis Katimba.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Christina Mndeme akikagua ujenzi wa Kituo cha Afya Bulige.
Muonekano wa baadhi ya Majengo katika Kituo cha Afya Bulige.
Muonekano wa baadhi ya Majengo katika Kituo cha Afya Bulige.
Muonekano wa baadhi ya Majengo katika Kituo cha Afya Bulige.

Post a Comment

0 Comments