Header Ads Widget

MGEJA ALAANI UPOTOSHAJI,UPANDIKIZAJI CHUKI ZA UDINI NA UKABILA UWEKEZAJI BANDARI YA DAR ES SALAAM

Mwenyekiti wa Taasisi ya Mtanzania Mzalendo Foundation Hamis Mgeja

Na Marco Maduhu, SHINYANGA

MWENYEKITI wa Taasisi ya Mtanzania Mzalendo Foundation Hamis Mgeja, ambao wanajihusisha na masuala ya haki, demokrasia na utawala bora, amelaani kitendo cha baadhi ya watu kupitia mitandao ya kijamii kupotosha Umma suala la Mkataba wa uwekezaji Bandari ya Dar es salaam pamoja na kupandikiza chuki za udini na ukabila.

Amebainisha hayo jana wakati akizungumza na vyombo vya habari mkoani Shinyanga.

Amesema wao kama Taasisi ya Mtanzania Mzalendo Foundation, wamefanya uchambuzi wa kina pamoja na kufuatilia mijadala mbalimbali ikiwamo kusikiliza bunge, na wamejiridhisha pasipo shaka yoyote, kwamba mpango wa Serikali kuhusu uwekezaji wa Bandari ya Dar es salaam ni mzuri na wameunga mkono asilimia 100 kwa maslahi mapana ya Taifa, na kulaani upotoshaji na upandikizaji wa chuki.

“Taasisi ya Mtanzania Mzalendo Foundation tunaimani na Serikali haiwezi kupotosha umma wala kuuza maslahi ya nchi, tumeona Bunge limeridhia suala hili, na sisi kama Watanzania tumeona Jambo hili tulizungumze na kumuunga Mkono Rais Samia juu ya uwekezaji wa Bandari ya Dar es salaam baina ya Tanzania na Dubai,”amesema Mgeja

Aidha, amesema kuna mambo ambayo yamekuwa yakimkera kupitia mitandao ya kijamii, na kuamua kuyazungumza ili kuweka sawa hasa ya upotoshaji na upandikizaji wa chuki kwenye masuala ya udini na ukabila ambayo hayana afya na yanaweza kuligawa Taifa, na kuwaomba Watanzania wapuuze Propaganda hizo na kuunga mkono uwekezaji huo.

Amesema suala la kubinafsisha hali jaanza katika awamu ya Sita, na pale panapo onekana hakuna ufanisi, ni vyema wakatafutwa wawekezaji ili kuongeza ufanisi na kupata mapato mengi kwa mashali ya Taifa, na kuomba hata Bandari ya Bagamoyo, Tanga na Mtwara napo patafutwe wawekezaji.

“Kwenye suala hili la Bandari ya Dar e salaam tuna muomba Rais azibe masikio, hata kwenye Filamu ya Royal Tour napo kulikuwa na maneno mengi, leo tumeona faida yake fedha za kigeni zimeongezeka kutokana na Sekta ya Utalii, na hili jambo la uwekezaji wa Bandari mafanikio yake tutayaona na wanaopinga watakuja kusema tulichelewa,” amesema Mgeja.

Amesema kwa watu ambao bado wanapinga uwekezaji huo wa Bandari ya Dar es salaam, waje sasa na mbadala kwamba wao wanaweza kufanyanini, au kama hawakubaliani mtu mwenye dini flani au kabila flani waeleze wao wanataka mtu mwenye dini gani au kabila gani, na kusema kwamba wasiwe Mahodari wa upotoshaji bali waje na mawazo ya kujenga nchi na siyo kuleta chuki za kidini.

“Bandari ndiyo Sekta mama, mapato ambayo yanaweza kupatikana katika uwekezaji huu, tangia tupate uhuru hayataweza kupatikana kama yatakavyo patikana katika mpango huu, hivyo tuiunge mkono Serikali yetu”amesema Mgeja.

Aidha, Juni 16 mwaka huu Wazee, Viongozi wa Dini na Machifu mkoani Shinyanga, nao walitoa tamko la kumuunga mkono Rais Samia juu ya Mkataba wa uwekezaji wa Bandari ya Dar es salaam, na kulaani juu ya upotoshaji kwa baadhi ya watu ambao hawana nia njema na Taifa kusongambele kimaendeleo.

Post a Comment

0 Comments