
Suzy Luhende Shinyanga blog
Baadhi ya wazazi wanaotelekeza watoto wao na wengine kuwaachia mabibi wametakiwa kuacha tabia hiyo kwani kufanya hivyo wanasababisha watoto wengi kuwa watoto wa mitaani na kukosa maadili kutokana na kukosa malezi bora ya baba na mama.
Agizo hilo limetolewa leo na kamati ya utekelezaji wa Jumuiya ya wazazi CCM wilaya ya Shinyanga mjini, wakati wakiwa kwenye ziara ya kukagua uhai wa Chama na Jumuiya zake katika kata ya Ngokolo manispaa ya Shinyanga, ambapo ilielezwa baadhi ya wazazi wamekuwa wakiwatelekeza watoto wao na kwenda kusikojulikana na kuwaacha watoto wakihangaika na bibi zao.
Katibu wa Jumuiya ya wazazi CCM wilaya ya Shinyanga mjini Dorisi Kibabi ametoa agizo hilo baada ya kusikia taarifa ya kata ya Jumuiya hiyo ikitaja kuwa kuna watoto wanaoishi katika mazingira magumu ambao wametelekezwa na wazazi wao na kuachiwa mabibi ambao nao hawana uwezo.
Kibabi amesema wazazi wanaotelekeza watoto wao kwa mabibi wanafanya dhambi kubwa, kwani wao waliwalea na sasa hawana nguvu tena za kulea wajukuu, lakini wanalazimika kuanza kuwahangaikia watoto hao kwa kuwatafutia chakula hali ambayo ni kumfanya bibi huyo apate mateso ya kumuwazia mjukuu huyo anakula nini, anavaa nini.
"Niwaombe wanawake wenzangu tunaotelekeza watoto wetu tuache tabia hiyo kama tunawaacha watoto tuache na chakula ama tutoe matumizi kwa ajili ya watoto wetu,kuna wengine wanawaachia wanaenda kazini na wanarudi na chochote hapo sawa, lakini wanaotelekeza na kwenda mbali na kusahau kabisa kama wanawatoto wanafanya vibaya warudi kwa watoto wao wawalee,"amesema Kibabi.
"Pia niwaombe wazazi wote tunapoona mtoto anaharibikiwa na anaelekea kuwa na maadili yasiyofaa tutoe taarifa kwa wazazi tusiwaangalie tu wakaharibikiwa zaidi, tunatakiwa kurudisha upendo wa zamani tuone mtoto wa mwenzako kama mtoto wako, tukifanya hivyo tutaokoa vizazi vyetu na jamii itakuwa yenye maadili mema,"amesema Kibabi.
Kwa upande wake mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM wilaya ya Shinyanga mjini Fue Mrindoko amewahimiza wanachama wa Jumuia ya wazazi kuwa na upendo na mshikamano, ikiwa ni pamoja na kuendelea kusajili wanachama wapya katika kata hiyo, kwani Jumuiya hiyo inahitaji kuwa na wanachama wengi.
Pia amewaomba mabalozi kuandikisha idadi ya wazee waliopo katika mitaa yote mbalimbali ili waweze kuandikishwa bima ya afya, "naamini kufikia tarehe 28 zoezi hili litakuwa tayari kabisa,"amesema Mrindoko.
Naye katibu elimu, malezi na mazingira wa Jumuiya ya wazazi wilaya ya Shinyanga mjini Richard Mseti amesema watoto wanatakiwa kulelewa katika mazingira safi ili wawe na afya bora, ambapo kila familia inatakiwa kutunza mazingira kwa kupanda miti agizo ambalo linatekelezwa na ilani ya CCM
"Tuwaombe wazazi wote tuyapambe mazingira yetu kwa kupanda miti, tuwe wasafi, kwani miti inafaida kubwa kwa binadamu inatengeneza hewa safi, lakini uchafu unaleta Magonjwa,amesema Mseti.
Aidha mjumbe wa kamati ya Utekelezaji Joseph Ntabindi amewaomba wazazi waendelee kuchangia chakula kwa ajili ya watoto mashuleni, kwani wakishiba wanaelewa vizuri wanachofundishwa darasani .
Mjumbe wa kamati hiyo Piter Frank ameiomba jumuia ya wazazi kuwa wabunifu ili kuhakikisha wanafanya vizuri na waendelee kuwakusanya wanachama waliorudi nyuma warudi kundini na kama watakuwa hawana kadi wapatiwe kadi za Jumuiya na za Chama.














Katibu wa Mbunge wa jimbo la Shinyanga Samweli akitoa ufafanuzi juu ya maji




