Meneja Mkuu wa Mgodi wa Barrick Bulyanhulu,Cheick Sangare, akiongea wakati wa hafla ya kusaini mkataba wa makubaliano na viongozi wa Halmashauri ya wilaya ya Nywang’hwale ya kutekeleza miradi ya kijamii katika wilaya hiyo kupitia fedha za uwajibikaji wa jamii katika hafla iliyofanyika mgodi hapo mwishoni mwa wiki, kushoto ni Meneja wa Meneja uhusiano wa jamii wa mgodi huo Agapiti Paul.
Meneja Mkuu wa Mgodi wa Barrick Bulyanhulu,Cheick Sangare (Kushoto) akibadilishana nyaraka za makubaliano na Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Nyang’hwale, Bw.John Isaac John muda mfupi baada ya kusaini mkataba wa makubaliano katika hafla iliyofanyika katika Mgodi wa Bulyanhulu.
Meneja Mkuu wa Mgodi wa Barrick Bulyanhulu,Cheick Sangare (Kulia) akibadilishana nyaraka za mkataba wa makubaliano na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Nyang’hwale,Bw.Majagi Maiga ambapo mgodi huo utatoa kiasi cha shilingi milioni 989 kwa ajili ya kufankisha miradi ya kijamii kupitia fedha za mfuko wa uwajibikaji kwa jamii katika kipindi cha mwaka huu.
Kaimu Mwenyekiti wa mfuko wa maendeleo wa halmashauri ya wilaya ya Nyang’hwale,Bw.Patrick Athanas akiongea katika hafla hiyo iliyofanyika mwishoni mwa wiki katika mgodi wa Bulyanhulu.
Diwani wa kata ya Kharumwa iliyopo katika halmashauri ya Nyang’hwale akiongea wakati wa hafla hiyo.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Nyang’hwale,Bw. Majagi Maiga (kushoto) na Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Nyang’hwale, Bw.John Isaac John wakisaini mkataba wa makubaliano ya utekelezaji wa miradi ya kijamii kutumia fedha za uwajibikaji kwa jamii zitakazotolewa na Barrick Bulyanhulu mwaka huu.
Meneja Mkuu wa Mgodi wa Barrick Bulyanhulu,Cheick Sangare (kushoto) na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Nyang’hwale,Bw. Majagi Maiga (kulia) wakisaini mkataba wa makubaliano ya utekelezaji wa miradi ya kijamii kutumia fedha za uwajibikaji kwa jamii zitakazotolewa na Barrick Bulyanhulu mwaka huu.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Nyang’hwale,Bw.Majagi Maiga akiongea wakati wa hafla hiyo
Wafanyakazi wa Barrick Bulyanhulu na wageni waalikwa katika hafla hiyo fupi wakifuatilia matukio ya kusainiwa kwa mkataba wa makubaliano baina ya Mgodi na Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale.
Picha ya pamoja ya Wafanyakazi wa Barrick Bulyanhulu na viongozi wa Serikali wa Halmashauri ya wilaya ya Nyang’hwale iliyopo mkoani Geita baada ya kusaini mkataba wa makubaliano ya utekelezaji wa miradi ya kijamii kutumia fedha za uwajibikaji kwa jamii zitakazotolewa na Barrick Bulyanhulu mwaka huu.
***
Mgodi wa Barrick Bulyanhulu, uliopo wilayani Msalala mkoani Geita unazidi kuboresha maisha ya Wananchi wanaoishi katika Halmashauri ya Nyang’hwale kupitia miradi mbalimbali inayotekelezwa kupitia fedha za uwajibikaji kwa jamii ambapo mwishoni mwa wiki viongozi wa Mgodi huo na halmashauri hiyo walisaini mkataba wa makubaliano wa kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo yenye thamani ya milioni 989,000,000/- katika kipindi cha mwaka 2023.
Akiongea katika hafla hiyo iliyofanyika katika Mgodi wa Bulyanhulu na kuhudhuriwa na viongozi wa Halmashauri ya Nyang’hwale na wafanyakazi wa Barrick, Meneja wa Barrick Bulyanhulu, Cheick Sangare, alisema kampuni itaendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha inafanikisha miradi ya kuboresha jamii zinazozunguka katika maeneo ya migodi yake kwa mujibu wa sera za nchi kupitia fedha za Uwajibikaji kwa jamii (CSR).
Sangare, alisema Mgodi wa Bulyanhulu mwaka huu unatarajia kuzalisha karibia wakia 215,000 za dhahabu,ambapo kutokana na uzalishaji huu utatenga shilingi bilioni 2.9 kwa ajili ya miradi ya uwajibikaji kwa jamii iliyopendekezwa na wilaya husika ambapo kati ya fedha hizi zitaenda kwa halmashauri za wilaya za Msalala na Nyang’wale.
“Nawapongeza Kamati ya Maendeleo ya Halmashauri ya Nyang’hwale kwa kuchagua miradi yenye kugusa mahitaji ya Wananchi ikiwemo ya afya, maji na elimu sambamba na miradi mingine ya maendeleo, natumaini miradi hii itatekelezwa kama ilivyopangwa na kukamilika kwa wakati mwafaka uliopangwa na nawashauri katika siku za usoni mwendelee kupendekeza miradi endeelvu ambayo itaacha alama hata muda wa mgodi ukiisha” alisema Sangare.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Nyang’hwale, Bw .John Isack John, aliipongeza Barrick Bulyanhulu kwa mapinduzi makubwa ya maendeleo inayoendelea kufanya katika maeneo yanayozunguka mgodi kupitia fedha za uwajibikaji wa jamii (CSR) ambayo yanazidi kuboresha maisha ya wananchi na kuwafanya wajivunie kuwepo migodi katika eneo lao.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Nyang’hwale, Bw.Majagi Maiga, alishukuru Barrick Bulyanhulu, kwa kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika manispaa hiyo na aliahidi kuwa Serikali itahakikisha fedha zote zinatumika kwa lengo lililokusudiwa la kufanikisha miradi ya maendeleo kwa wananchi.
Baadhi ya miradi itakayotekelezwa kwa fedha za uwajibikaji kwa jamii za Barrick Bulyanhulu katika halmashauri ya Nyang’hwale katika kipindi cha mwaka huu ni kumalizia ujenzi wa wodi maalum katika hospitali ya Nyang’hwale (97,860,500/-),kumalizia ujenzi wa gereji katika kijiji cha Kharumwa (40,000,000),kumalizia ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa katika shule ya msingi Ikangala (11,625,000),kumalizia ujenzi wa vyumba bitatu katika shule ya msingi Samia Suluhu (18,833,000),ujenzi wa choo na sehemu maalum ya kuchoma taka katika zahanati ya Iyenze (14,279,250),kukamilisha ujenzi wa jingo la maabara katika sekondari ya Mwingiro (16,000,000),kumalizia jengo la utawala katika sekondari ya Kaboha (67,602,000),kukamilisha ujenzi wa bwalo la chakula katika shule ya msingi ya Kharumwa (60,000,000) na kukamilisha ujenzi wa vyumba 5 vya madarasa katika shule za msingi za Nyamikonze, Ngwasabuka,Iyenze na Kafita 62,500,000).
Miradi mingine ni kukamilisha jengo la utawala,maabara choo na mfumo wa maji katika shule ya sekondari ya Nyamtukuza (51,169,200),ujenzi wa kituo cha mabasi katika kijiji cha Ikangala (170,000,000),kukamilisha ujenzi wa zahanati ya Mwingiro (74,178,450),kukamilisha ujenzi wa jengo la dharura hospitali ya Mwingiro (69,250,000),kukamilisha ujenzi wa zahanati ya Nyijundu (45,885,000),mpango wa kuinua ufaulu wa wanafunzi mashuleni (25,000,000),matenki ya kuhifadhi maji na kujenga mfumo wa kuvuna maji ya mvua katia sekondari ya Mwingiro (6,000,000),ujenzi wa jengo la utawala katika shule ya msingi ya Kharumwa (60,086,225),kukamilisha ujenzi wa kituo cha polisi cha Kharumwa (17,931,375) na kununua jenereta kubwa na kuimarisha miundombinu ya hospitali ya wilaya ya Nyang’hwale (50,000,000).