Header Ads Widget

DC- KAHAMA ASISITIZA WATOTO UMRI CHINI YA MIAKA MITANO WAFIKIWE NA CHANJO YA POLIO


 Mkuu wa wilaya ya Kahama Festo Kiswaga  ambaye anasisitiza suala la chanjo  ya polio katika wilaya yake.

Na  Kareny  Masasy, Kahama

MKUU wa wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga Festo Kiswaga amesema  watumike mabalozi  wa nyumba kumi kwenye mitaa,vitongoji na vijiji katika zoezi la utoaji chanjo  ya  kinga ya polio kwa watoto chini ya umri wa miaka mitano.

Kiswaga amesema hayo leo tarehe 1/12/2022 kwenye  kikao kazi cha kujadiliana utoaji wa chanjo  ya kinga ya Polio kwa awamu zilizopita  na awamu ya nne.

 Kikao hicho kilikutanisha  wataalamu  kutoka idara ya afya,lishe na maendeleo ya jamii wanaosimamia zoezi la chanjo katika halmashauri za Ushetu,Msalala na manispaa ya Kahama.

Kiswaga amesema wilaya ya Kahama inachukua nusu ya mkoa wa Shinyanga imepata idadi ya chanjo  304,600  ambazo zitatoa  kuanzia leo kwa watoto chini ya umri wa miaka mitano nakusisitiza  mafaniko zaidi.

“Sipendi mlegee kwenye tukio hili muendelee kuonyesha mfano…. Kama mlivyofanya utoaji wa chanjo kwa awamu zilizopita”amesema  Kiswaga.

Mratibu wa chanjo kutoka halmashauri ya Ushetu Ramadhani  Kabuhu akisoma taarifa kwa niaba ya halmashauri zote amesema   zoezi la utoaji chanjo litaanza tarehe 1 hadi 4 Desemba/2022.

Maandalizi ya utoaji chanjo awamu ya nne kwa halmashauri za Msalala,Ushetu na  Kahama yamekamilika  wanatarajia kuwafikia  watoto chini ya umri wa miaka mitano (walengwa) 284,495 na chanjo ya polio iliyopokelewa ni 304,600.

Kabuhu amesema halmashauri ya Ushetu wamepokea chanjo 98600,Msalala chanjo 107,000 na Manispaa Kahama chanjo 99,000.

"Kuna  timu ya wataalam 549 na maboresho yaliyofanyika kuongezwa kwa timu ya  watu 20 ya utoaji chanjo kwa kila halmashauri kuweza kuwafikia watoto wote"amesema  Kabuhu.

Wataalamu wote wamekiri mbele ya mkuu wa wilaya  maandalizi yako vizuri wataalamu wamejiandaa kufanya zoezi hilo kwa kuwafikia watoto kila kona  pamoja na kuwafuata shambani.

Hata hivyo mkoa wa Shinyanga unatarajia kutoa  chanjo kwa watoto chini ya umri wa miaka mitano  521,025 na kupokea  dozi  ya chanjo  614,800 ikiwa wataalamu 1,021.

Wizara ya afya kwa kushirikiana  na wadau wa sekta ya afya  imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kukabiliana na tishio la mlipuko wa ugonjwa wa polio hapa nchini.

Ugonjwa wa polio ni ugonjwa  unaosababishwa na kirusi ambacho  huambukizwa kutoka kwa mtu  aliyeathirika kwenda kwa mwingine  kwa kula au kunywa kitu kilichochafuliwa na kinyesi chenye virusi vya polio.

 vinapoingia katika mwilini  huathiri  mfumo wa fahamu na kusababisha  madhara ya kiafya ikiwemo kupooza  kwa ghafla viungo vya mwili.


Post a Comment

0 Comments