Header Ads Widget

JAJI KIONGOZI WA MAHAKAMA KUU YA TANZANIA ATAJA USULUHISHI KUWA NJIA SAHIHI YA UTATUZI WA MIGOGORO

JAJI KIONGOZI ATAJA USULUHISHI KUWA NJIA SAHIHI YA UTATUZI WA MIGOGORO

· Awataka Mawakili kutumia mifumo iliyopo kisheria kuwasilisha malalamiko yao

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Mhe. Mustapher Siyani, akizungumza kwenye kikao hicho.

Mkutano ukiendelea.

Mkutano ukiendelea.

Mkutano ukiendelea.

Na Lydia Churi-Tume ya Utumishi wa Mahakama, Shinyanga

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Mhe. Mustapher Siyani amesema usuluhishi ni njia sahihi ya kutatua migogoro kwa kuwa inajenga na kukuza undugu na pia ni takwa la Katiba ya nchi.

Akizungumza na wadau wa utoaji haki katika Mkutano wa Tume ya Utumishi wa Mahakama jana mkoani Shinyanga, Jaji Siyani alisema njia hiyo ya utatuzi wa migogoro ina tija katika jamii kwa kuwa huwaacha watu wakiwa wamepatana badala ya kutekeleza amri zinazotolewa na Mahakama.

“Wakati mwingine ni bora hata pale unapofanyika vibaya lakini watu wamepatana ni bora zaidi kuliko amri zinazotolewa na Mahakama”, amesema Jaji Kiongozi.

Akitolea mfano wa nchi zilizoendelea, Jaji Siyani alisema kuwa katika nchi hizo, usuluhishi unamaliza kwa zaidi ya asilimia 90 migogoro inayofikishwa mahakamani. Aliongeza kuwa hali hiyo ni tofauti kwa nchi yetu licha ya kuwa zipo njia mbalimbali za usuluhishi hata kabla nchi haijapata uhuru.

Alisema ushahidi wa kwa nini Tanzania haitumii njia ya usuluhishi ni uwepo wa mashauri machache yaliyosikilizwa kwa njia hiyo. Alisema kati ya mwaka 2020 hadi 2021 Masjala za Mahakama Kuu ya Tanzania ziliamua mashauri 2,398 yenye asili ya madai na kati ya mashauri hayo, mashauri 182 tu ambayo ni sawa na asilimia nane ndiyo yaliyoamuliwa kwa njia ya usuluhishi.

Akizungumzia Mawakili, Jaji Kiongozi alisema wote wanao wajibu wa kuwaandaa wadaawa kushiriki kwenye hatua zote za usuluhishi na kuwa tayari kufikia uamuzi unaotokana na mapatano kwani kwa kufanya hivyo kutarahisisha kazi ya utoaji haki, kupunguza gharama na kuokoa muda.

“Usuluhishi utafanikiwa tu endapo kuna dhamira ya kusuluhisha na kufikia muafaka, lakini ikichukuliwa kuwa ni hatua ya lazima kisheria hautaweza kufanikiwa na italeta dhana kuwa hatua za usuluhishi zinapoteza muda”, alisema Mhe. Siyani.

Aidha, Jaji Kiongozi amevitaka vyombo vya habari nchini kutenga nafasi ya kuelimisha Umma umuhimu wa usuluhishi ili wananchi waelewe faida zake na kuitumia njia hiyo. Alisema kutumika kwa njia hiyo si tu kuwa itaongeza kasi ya usikilizwaji wa mashauri bali pia mshikamano na undugu wa jamii utaimarika zaidi.

Ametoa wito kwa Maafisa wa Mahakama hususani Mawakili kushiriki katika maboresho ya Mahakama kwa kutumia mifumo na vyombo vilivyopo kisheria badala ya kulalamika na kukosoa kupitia mitandao ya kijamii huduma zinazotolewa na Mahakama pamoja na watumishi wake.

“Katika zama tulizonazo, Wakili hatarajiwi tu kuisaidia Mahakama kufikia uamuzi wake bali pia anatarajiwa kuwa sehemu muhimu ya maboresho ya mifumo mbalimbali kivitendo ili kufikia lengo la Mahakama la kutoa haki kwa wakati”, amesisitiza Jaji Kiongozi.

Alisema Mawakili wanapaswa kufahamu kuwa kama suala linahusu maadili ya Jaji au Hakimu kuna kamati zilizoundwa kisheria zikiwemo Kamati za Maadili ya Maafisa wa Mahakama na nyinginezo hivyo wawasilishe malalamiko yao kwenye kamati hizo.

“Kumekuwepo na ongezeko la Maafisa wa Mahakama kuwa wakosoaji wa huduma za Mahakama na watumishi kupitia mitandao ya kijamii pekee hivyo matarajio ya Tume na Mahakama ni kuona wananchi na Maafisa wa Mahakama wanashiriki katika juhudi za kuboresha huduma kupitia mifumo na vyombo vilivyopo kisheria na si kulalamika kupitia mitandao, kuijadili na kuishia huko”, amesema.

Wajumbe wa Tume ya Utumishi wa Mahakama wanaendelea na ziara ya siku nne katika mikoa ya Shinyanga na Simiyu yenye leo la kutangaza shughuli za Tume hiyo na pia kukutana na wajumbe wa Kamati za Maadili ya Maafisa wa Mahakama ngazi ya Mkoa na wilaya pamoja na wadau wa utoaji haki.

Post a Comment

0 Comments