Header Ads Widget

WAZAZI NA WALEZI WATAKIWA KUWAPELEKA WATOTO KWENYE CHANJO YA POLIO

WAZAZI NA WALEZI WATAKIWA KUWAPELEKA WATOTO KWENYE CHANJO YA POLIO


Mkuu wa wilaya ya Shinyanga jasinta Mboneko akizungumza kwenye  kikao cha kamati ya afya wilaya ya Shinyanga


Mwenyekiti wa halmashauri ya Shinyanga Ngassa Mboje akizungumza jambo kuhusu chanjo ya polio.Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Shinyanga David Rwazo ambaye pia ni afisa utumishi wa halmashauri ya Shinyanga.


Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga Getruda Gisema ambaye pia ni afisa utumishi wa manispaa ya Shinyanga


.Kaimu afisa chanjo wilaya ya Shinyanga Said Mankiligo ambaye pia ni afisa afya wa Shinyanga.
Mratibu wa Chanjo Manispaa ya Shinyanga, John Alphonce Sakwa akitoa ufafanuzi juu ya chanjo ya polio
Wajumbe wa kamati ya afya wakiwa kwenye kikao cha kamati hiyo

 Suzy Butondo, Shinyanga 

Wazazi na walezi wenye watoto waliochini ya miaka mitano wametakiwa kuwapeleka  watoto wao kwenda kupatiwa chanjo ya kuzuia ugonjwa wa polio ambao ukimpata mtoto unaweza kusababisha ugonjwa wa kupooza, ulemavu hadi kifo.

Licha ya wazazi hao pia viongozi wa dini na viongozi wote kuanzia mitaa vitongoji na kata wametakiwa kuhamasisha na kutoa elimu kwa wananchi ili waweze kuwa na uelewa wa chanjo hiyo ambayo inasaidia kukinga ugonjwa wa polio kwa watoto hao.

Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko kwenye kikao cha kamati ya afya wilaya ya Shinyanga, ambaye amesema yeye na kamati yake wamejipanga kikamilifu kuhakikisha wanafanikisha Kampeni ya Chanjo ya Polio kwa awamu ya tatu ambayo inaanza  Septemba 1 hadi 4 ,2022 itakayofanyika nyumba kwa nyumba kwa watoto wote walio chini ya miaka mitano.

Mboneko amesema wananchi wakihamasika kikamilifu zoezi la chanjo litafanyika kwa wakati na lengo litafikiwa ili kuhakikisha watoto wa umri huo wanakuwa salama na wanategemea awamu ya tatu matokeo yatakuwa makubwa zaidi baada ya kufanya vizuri kwenye awamu ya pili iliyopita ambapo walikuwa wa kwanza. 

"Ugonjwa huu ni mbaya sana, hivyo tusifanye masihara, kwani watoto wetu wakipata chanjo ya matone watakuwa salama, wataepuka magonjwa kwa sababu watakuwa na kinga ya kutosha hawatayumbishwa na ugonjwa huo hata kama walipata chanjo awamu ya kwanza na ya pili haina madhara yoyote wachanjwe tu”, amesema Mboneko.

Malengo yetu tuliyojiwekea ya Walengwa 88,376 kwa Halmashauri ya Shinyanga na Manispaa ya Shinyanga ni 44,013 naomba  isipungue, tuone  namba imeongezeka, na tuwafikie watoto wote wenye umri wa chini ya miaka mitano, na naomba wawepo wataalamu wa kutosha, kwenye maeneo ambayo kuna changamoto wataalamu waongezwe ili kuweza kufanikisha zoezi hili”,amesema Mboneko.

Kwa upande wake afisa Mipango wa Taifa wa Chanjo kutoka Wizara ya Afya, Immaculate Dotto amesema lengo la Kampeni ya Chanjo ya Polio awamu ya tatu ni kukinga watoto walio chini ya miaka mitano ili wasipatwe na virusi vya ugonjwa huo, ambao unaambukizwa kwa njia ya vinyesi vinavyozagaa ovyo.

" Ili tufanikishe lengo hili ni vizuri kila kiongozi mtendaji aelimishe jamii na kuwaeleza faida za Chanjo ya Polio, kampeni hii itafanyika kwa siku nne kuanzia Septemba 1 hadi 4,2022, ugonjwa huu unasababishwa na Virusi vya Polio vinavyosababisha kupooza na kusababisha ulemavu  hatimaye kifo kabisa, kwani  virusi hivi huingia mwilini kwa njia ya mdomo,kwa kunywa maji au chakula kilichochafuliwa na kinyesi kutoka kwa mtu aliyeambukizwa virusi na hauna tiba, lakini unaweza kuzuiliwa tu kwa kupata chanjo ya matone ya polio”,amesema Dotto.

Naye mratibu wa Chanjo Manispaa ya Shinyanga, John Alphonce Sakwa amesema walengwa wa kampeni ya chanjo ya Polio katika halmashauri ya wilaya ya Shinyanga ni 88,376 na Manispaa ya Shinyanga 44,013 huku akieleza kuwa Chanjo itafanyika nyumba kwa nyumba na itaendelea pia kwenye vituo vya kutolea huduma za afya.

“Sambamba na uchanjaji huduma zingine zitatolewa ikiwemo elimu ya chanjo kwa jamii, kuimarisha huduma za chanjo katika vituo vya kutolea chanjo pamoja na kuwatafuta na kuwafuatilia watoto wote wenye umri chini ya miaka 15 ambao wamepata ulemavu ghafla tepetepe (washukiwa wa ugonjwa polio) na kutoa taarifa vituo vya karibu kwa uchunguzi na kubaini ugonjwa huu wa polio”,amesema Sakwa.

Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga Getruda Gisema na Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Shinyanga David Rwazo wamesema wamejipanga vizuri kuhakikisha wanafanikisha vizuri kampeni hiyo ikiwa ni pamoja na kuwa na takwimu sahihi.

Kaimu afisa chanjo wilaya ya Shinyanga Said Mankiligo amesema uzinduzi wa chanjo utafanyika katika kijiji cha Nindo ambapo tayari wameshaanza kuhamasisha,  na manispaa utafanyika katika zahanati ya Chamaguha manispaa ya Shinyanga.

Post a Comment

0 Comments