Header Ads Widget

WAELIMISHA JAMII WAPATIWA MAFUNZO YA KUPAMBANA NA UKATILI KUTOKA SHIRIKA LA WEADO

 

 Mkurugenzi  wa Shirika  lisilo la kiserikali linalotetea haki za wanawake na watoto  la Women Elderly Advocacy and Development Organization (WEADO) Eliasenya Nnko  akitoa mafunzo kwa waelimisha jamii kutoka kata ya Masengwa.


Anna Nchenye kutoka shirika la WEADO akitoa mafunzo kwa waelimisha jamii.

Suzy Butondo.

WAELIMISHA jamii juu ya kupambana na ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na Watoto kutoka kata ya Masengwa halmashauri ya Shinyanga  wamepatiwa mafunzo ya kwenda kuelimisha jamii, ili iweze kuachana na matukio ya ukatili.

Akitoa mafunzo hayo Mkurugenzi  wa Shirika  lisilo la kiserikali linalotetea haki za wanawake na watoto  la Women Elderly Advocacy and Development Organization (WEADO) Eliasenya Nnko yaliyofanyika  katika kata ya Masengwa  halmashauri hiyo, amesema lengo la mafunzo hayo ni kupunguza matukio ya ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto katika kata hiyo.

Nnko amesema ili jamii iweze kuishi kwa amani na utulivu bila ya kufanyiana vitendo vya ukatili ni lazima wananchi wapewe elimu, kwani kuna baadhi ya wazazi, walezi na wanaume wanawafanyia ukatili watoto, wenza wao bila kujua, lakini wakipatiwa mafunzo watakuwa na uelewa.

"Utafiti uliofanyika ulionesha matukio mengi ya ukatili yanatokea Majumbani pamoja na Shuleni, na mengi yamekuwa yakifanywa na watu wa karibu na familia, hivyo waelimishaji wetu wanatakiwa waelimishe jamii ili jamii iwe na uelewa na kuachana na ukatili ikiwezekana kuuondoa kabisa na kubaki amani"amesema  Nnko.

" Pia nawaomba sana wawezeshaji wote tuliowapa mafunzo mkatoe elimu hii kwa jamii ili iweze kuwa na uelewa kwani wengi wao hawaelewi nini maana ya ukatili, lakini tukielimisha jamii tunaamini itaelewa kwamba  mtu akifanyiwa ukatili atapata madhara gani, ikiwa na uelewa matukio ya kijinsia yatapungua "ameongeza.

Kwa upande wake , Mtendaji wa Kata ya Masengwa wilayani humo Hussein Majaliwa, wakati akifungua mafunzo hayo amewataka waelimisha jamii wasikilize kwa makini ili wakatoe elimu kwa jamii inayowazunguka ili kupunguza ama kuondoa kabisa ukatili katika kata ya Masengwa.

Baadhi ya waelimisha jamii juu ya ukatili Mayenga Mabula na Sarah Charles wakazi wa kata ya Masengwa, wamesema elimu wameipata wataenda kuelimisha jamii na wanaamini matukio ya kijinsia yatapungua.

Mafunzo hayo yameandaliwa na shirika la WEADO  la mkoani Shinyanga kwa ufadhili wa mfuko wa Ruzuku wa wanawake Tanzania (WFT) wenye thamani ya Sh.milioni 12.4.ambao utakoma March 2022, ambapo wamepewa mafunzo waelimishaji nane, kitongoji Cha Ilobashi watu wawili, Ikonda watu wawili, Bubale watu wawili.

Pia shirika hilo lilitoa elimu kwenye vijiwe vya kahawa vilivyopo katika kata hiyo katika vijiji vya Ilobashi, Ikonda, Bubale na Masengwa, ambapo baadhi ya wazee walisema hawajui maana ya ukatili, hivyo walielimishwa na kuelewa, nao wakaahidi wataenda kuelimisha kwa mtu mmoja mmoja ili kuondokana na matukio hayo.

Baadhi ya wazee na vijana waliokuwa kwenye vijiwe vya kahawa Magembe Kija na Juma Shilinde ambaye ni Mwenyekiti wa kitongoji cha  Nyati walisema kuna matukio ya ukatili yalikuwa yakifanyika katika kijiji hicho wanaona ni kawada tu, baada ya kupewa elimu wameelewa kuwa kumbe vitu vingi vinavyofanywa na baadhi yao ni ukatili.

"Tunawashukuru sana shirika la WEADO kwa kutuletea elimu hii kwani tulikuwa hatujui kama usipomnunulia mtoto mavazi, viatu, kukutana ma mama bila idhini yake, na kutompeleka shule mtoto,ni ukatili, tutaifikisha hii elimu hata kwa wenzetu ambao hawapo hapa tunaimani jamii ya hapa Masengwa itabadilika"amesema Shilinde.
 
Emmanuel Samson mkazi wa kata ya Masengwa alipokuwa akizungumza na mwandishi wa Shinyanga press club blog kuhusu masuala ya ukatili wa jinsia.
 

 Wanaume wakiwa katika vijiwe vya kahawa wakipatiwa elimu ya ukatili wa kijinsia kutoka Shirika la WEADO katika kata ya Masengwa,Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga.

 Waelimisha jamii walioshiriki mafunzo ya ukatili wa kijinsia kutoka shirika la WEADO
 
 
 

Picha ya pamoja baina ya waelimisha jamii na watendaji wa shirika la WEADO kutoka kata ya Masegwa.

 

TUTUMIE HABARI,PICHA,MATUKIO AU TANGAZO LAKO TUKUWEKEE KWENYE SHINYANGA PRESS CLUB BLOG,WASILIANA NASI KWA Email : shinyapress@gmail.com Simu/WhatsApp 0756472807