Header Ads Widget

CHUO CHA UONGOZI WA MAHAKAMA LUSHOTO CHAPONGEZWA KUWA NI KISIMA CHA UTOAJI MAFUNZO KWA WATUMISHI WA MAHAKAMA


Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani akifungua mafunzo elekezi ya siku tano yanayowashirikisha Naibu Wasajili na Watendaji wa Mahakama ambayo yanafanyika katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA).
 Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akisistiza jambo alipokuwa anatoa mada katika mafunzo hayo.
Kaimu Mkuu wa Chuo, Prof. Fatihiya Massawe, ambaye pia ni Naibu Mkuu wa IJA, Mipango, Fedha na Utawala akitoa neno la ukaribisho kabla ya ufunguzi wa mafunzo ya siku tano yanayowashirikisha Naibu Wasajili na Watendaji wa Mahakama ambayo yanafanyika katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA). ,Mafunzo hayo yamefunguliwa leo tarehe 29 Novemba, 2021 na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani.
Sehemu ya Naibu Wasajili na Watendaji wa Mahakama ya Tanzania wakifuatilia mada iliyokuwa inatolewa na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel.
***

Na Faustine Kapama na Rosena Suka, Mahakama-Lushoto

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani leo tarehe 29 Novemba, 2021 amefungua mafunzo elekezi ya siku tano kwa Naibu Wasajili na Watendaji wa Mahakama ambapo amekisisifia Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) kwa mchango mkubwa kinachofanya na kujenga taaluma bora kwa watumishi wa Mahakama na wananchi wengine kwa ujumla.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo ya siku tano yanayowashirikisha viongozi hao, Mhe. Siyani amebainisha kuwa Chuo kwa kushirikiana na Kitengo cha mafunzo cha Mahakama ya Tanzania wamekuwa wakifanya kazi nzuri kwa kutoa mafunzo mbalimbali elekezi na endelevu kwa watumishi wa Mahakama ya Tanzania.

“Kama ilivyo kwa wengine, mimi nina imani kuwa chuo hiki kweli ni kitovu na kisima cha elimu bora. Kimsingi, chuo hili kina uwezo wa kujenga taaluma na kufanya leo hii tuna Wasajili ambao kesho ni Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania. Kwa hiyo, mimi niwapongeze sana na nifikishie salamu zangu kwa Mkuu wa Chuo,” Jaji Kiongozi alimweleza Kaimu Mkuu wa Chuo, Prof. Fatihiya Massawe, ambaye pia ni Naibu Mkuu wa IJA, Mipango, Fedha na Utawala.

Amesema kuwa mafanikio katika utoaji wa mafunzo elekezi ya awali na mafunzo endelevu ya kimahakama ni mojawapo ya matunda ya kazi nzuri yanayofanywa na IJA kwa kuzingatia Sera ya Mafunzo ya Mahakama ya mwaka 2019 ambayo inakitambua Chuo hicho kama kitovu au kisima cha utoaji mafunzo kwa watumishi wa Mahakama, lakini vile vile utafiti wenye lengo la kuongeza tija na kuboresha utendaji wa Mahakama ya Tanzania.

Jaji Kiongozi aliwakumbusha washiriki kuwa mafunzo ambayo yameandaliwa kwa ajili yao yamelenga kuwapa mbinu na nyenzo sahihi za kuweza kukabili changamoto mbalimbali za kiutendaji. “Hivyo muwe wazi kuuliza maswali na kuchangia uzoefu kila mmoja kwa namna ambayo mnaona italeta matokeo chanya katika utendaji kazi wenu. Shabaha ya kila mmoja wetu iwe ni utoaji wa haki na kuliletea maendeleo taifa letu na kutekeleza kwa vitendo Mkataba wa Huduma kwa Mteja,” amesema.

Mhe. Siyani alitumia nafasi hiyo kuwakumbusha washiriki wa mafunzo hayo kuwa wapo katika kipindi cha mapinduzi ya nne ya viwanda na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amekuwa akisisitiza watumishi wa Mahakama kujinoa zaidi kwenye eneo la TEHAMA ili waweze kuendana na kasi ya mabadiliko ya kidunia hivi sasa.

Amebainisha kuwa miongoni mwa mada zitakazotolewa katika mafunzo hayo inahusu TEHAMA, hivyo ni imani yake kupitia mada hiyo washiriki wote watapata nafasi ya kujifunza juu ya nafazi zao katika usimamizi wa mashauri kwa njia za kielektroniki. Aliwaomba kutumia fursa hiyo kupata kitu cha nyongeza katika eneo hilo na kwamba kila mmoja wao awe mfuasi wa karibu wa TEHAMA kama dunia inavyowataka hivi sasa.

“Tambueni kwamba tunakoelekea hakutakuwa na nafasi kwa Msajili au Mtendaji asiye na uelewa wa TEHAMA katika Mahakama yetu. Hiyo ni dhahiri kwa sababu ninyi ni wasimamizi wa mifumo ikiwemo ya TEHEMA na bila shaka msimamizi bora ni yule anayefahamu anachokisimamia,” aliwaambia viongozi hao wa Mahakama ya Tanzania.

Awali akitoa neno la ukaribisho, Kaimu Mkuu wa Chuo, Prof. Fatihiya Massawe alisema kuwa mafunzo yanayotolewa kwa Naibu Wasajili na Watendaji wa Mahakama siyo ya kwanza kutolewa hapo Chuoni, kwani IJA imekuwa ikitoa mafunzo elekezi (Induction) kwa wahesimiwa Majaji wote wapya wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania na mafunzo ya awali na elekezi kwa Majaji wote wapya wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Zanzibar wanapoteuliwa kwenye wadhifa huo na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzani pamoja na Rais wa Zanzibar.

Kwa mujibu wa Prof. Massawe, vilevile IJA imekuwa ikiendesha mafunzo elekezi kwa Mahakimu wote mara wanapoajiriwa kujiunga kwa mara ya kwanza na utumishi wa Mahakama kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kutenda haki kwa wote na kwa wakati kwa kuzingatia misingi ya sheria na uadilifu.

“Hii ni mara ya kwanza mafunzo ya namna hii yametolewa kwa Naibu Wasajili na hata kwa Watendaji. Tunapenda kuipongeza Mahakama ya Tanzania kwa kulisimamia hili. Tunaamini mafunzo haya elekezi ni mwanzo tu wa mafunzo endelevu ambayo washiriki hawa wataendelea kupata kama watumishi wa Mahakama. Chuo kinaahidi kitaendelea kutayarisha programu za mafunzo kulingana na uhitaji kadri watakavyoendelea kutekeleza majukumu yao na kubaini changamoto katika maeneo ya uhitaji wa mafunzo,” alisema.

Katika mafunzo hayo, mada mbalimbali zitawasilishwa na waezeshaji waliobobea katika maeneo mbalimbali, akiwemo Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma, Jaji Mkuu Mstaafu ,Mohamed Chande Othman, Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufani, Mhe. January Msoffe, Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Katarina Revocati na watendaji wengine waandamizi wa Mahakama.

Miongoni mwa mada zitakazowasilishwa kwenye mafunzo hayo zinajumuisha Uongozi wa Kimkakati, Stadi za Uongozi na Uwezo wa Kukabili Mabadiliko, Wajibu wa Mahakama, Utamaduni wake na Uhusiano wake na Mihimili Mingine ya Dola, Sheria ya Uendeshaji wa Mahakama na Uboreshaji unaofanywa na Mahakama, Maadili ya Watumishi wa Umma na Maadili ya Kimahakama, Usimamizi wa fedha na Manunuzi ya Umma pamoja na Usimamizi wa Nyaraka.


Post a Comment

0 Comments