Header Ads Widget

POLEPOLE AMALIZA UTATA HOJA YA JPM KUONGEZEWA MUDA

Humphrey Polepole akiwa bungeni leo

Mbunge wa kuteuliwa, Humphrey Polepole leo Jumanne Februari 9, 2021 amelieleza Bunge kuwa Rais wa Tanzania, John Magufuli hana mpango wa kuongeza muda wa kukaa madarakani.

Hata hivyo, amesema hawezi kuzuia mijadala ya wabunge kwa kuwa ni haki yao kusema kile wanachokiamini ndani ya Bunge.

Polepole ambaye ni katibu wa itikadi na uenezi wa CCM amesema ndani ya chama chao walishaelezwa hivyo na itabaki hivyo bila kubadilika.

Ametoa taarifa hiyo leo baada ya kuomba taarifa kufuatia kauli ya mbunge wa Konde (ACT-Wazalendo), Khatibu Said Haji kumtaja Polepole kwamba alitumwa na Rais kusema juu ya kutogombea lakini amekaa kimya.

Khatibu amesema kitendo cha kukaa kimya kinawafanya wabunge kuendelea kumtaka Rais Magufuli avunje Katiba wakati aliapa kuilinda.

"Rais hataongeza muda sisi ndani ya chama tulishaelezana na yeye (Rais) ndiyo msemaji mkuu, lakini humu bungeni haizuii wao kutoa maoni yao," amesema Polepole.

Katika michango ya wabunge, Deo Sanga (Makambako) na Joseph Msukuma (Geita Vijijini) waliibua hoja iliyoanzia Bunge la 11 wakimtaka Rais Magufuli kufikiria namna ya kuongeza muda wa kuwa madarakani.

Post a Comment

0 Comments