Header Ads Widget

NAIBU WAZIRI WA MAJI AKAGUA MIRADI MWANZA, ATOA ONYO KWA WAKANDARASI WATAKAOCHELEWESHA MIRADI

Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Maryprisca Mahundi (wa kwanza kulia) akishuka kwenye ngazi wakati wa ziara yake kwenye mradi wa tenki la maji la Buswelu Wilayani Ilemela mkoa wa Mwanza.

Na Mohamed Saif, Mwanza
SERIKALI haitowaongezea muda wakandarasi watakaoshindwa kukamilisha miradi ya maji kwa wakati na badala yake watanyang’anywa na itatekelezwa na wataalam wa ndani.

Rai hiyo imetolewa leo Februari 24, 2021 na Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Maryprisca Mahundi  kwa nyakati tofauti wakati wa ziara yake ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maji kwenye Wilaya za Nyamagana na Ilemela mkoani Mwanza.

“Wakandarasi ambao wanachelewesha miradi tutafuatilia ukomo wa mikataba yao na hatutaruhusu muda wa nyongeza labda tu kuwe na sababu za msingi zilizosababisha mradi kuchelewa,” amesisitiza Naibu Waziri Mahundi.

Amesema kwamba Serikali haitomvumilia mkandarasi yoyote mzembe na kwamba miradi itakayoshindwa kukamilika kwa wakati kama ilivyo kwenye mkataba itakamilishwa kwa utaratibu wa force account.

“Bahati nzuri tunao wataalam wazuri sasa mkandarasi atakayekwenda kinyume na mkataba ikiwa ni pamoja na kushindwa kukamilisha mradi kwa wakati, tunampokonya mradi na tunatekeleza wenyewe,” ameeleza.

Mhandisi Mahundi amesema kuwa inasikitisha kuona mkandarasi anashindwa kukamilisha mradi aliyokabidhiwa licha ya kwamba amepewa fedha kama ilivyo kwenye mikataba ya utekelezaji wake na alisisitiza kwamba Serikali ya Awamu ya Tano haipo tayari kuendelea kufanya kazi na mkandarasi wa namna hiyo.

“Serikali hii ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli ni ya vitendo, suala la mkandarasi kuongezewa muda bila sababu ya msingi hiyo haikubaliki, kwanini mkandarasi uwe kikwazo kwenye kutekeleza miradi licha ya kwamba unalipwa fedha yako kwa wakati, hii sio sawa,” amesisitiza Naibu Waziri huyo.

Aidha, Naibu Waziri Mahundi amebainisha kwamba Serikali imeazimia ifikapo mwaka 2025 upatikanaji wa majisafi na salama maeneo ya mijini uwe zaidi ya asilimia 95 na maeneo ya vijijini uwe zaidi ya asilimia 85.

Amesisitiza kwamba dhamira ni kumtua mama ndoo kichwani na kwamba hilo litafanyika kwa kuhakikisha huduma ya maji inafikishwa katika kila kaya na siyo kuishia kwenye vituo vya kuchotea maji maarufu kama vioski.

“Serikali ya Dkt. John Pombe Magufuli imejipambanua katika kumkomboa mwanamke na hili litafanyika kwa kuhakikisha tunamtua mama ndoo kichwani kwa kumfikishia bomba la maji nyumbani kwake,” amesema.

Akizungumzia miradi ambayo kwa muda mrefu imekua ikisuasua ama miradi kichefuchefu hususan kwenye maeneo ya pembezoni ambayo ilikabidhiwa kwa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), Mhandisi Mahundi alithibitisha kuwa utekelezwaji wake unakwenda vizuri na baadhi yake itakazinduliwa mnamo mwezi Machi mwaka huu wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Maji.

Aidha, Naibu Waziri Mahundi aliipongeza ushirikiano baina ya Serikali za Wilaya za Nyamagana na Ilemela na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA) na RUWASA Mkoa wa Mwanza na kuzitaka taasisi zingine kwenye Sekta ya Maji kuiga mfano huo.

“Lazima wataalam Sekta ya Maji tuwe na utamaduni wa kujenga mahusiano na Ofisi za Serikali kwenye maeneo ya miradi. Ushirikiano niliyouona hapa umenifurahisha na wengine muige kutoka hapa,” ameeleza.

Naibu Waziri Mahundi yupo Mkoani Mwanza kwa ziara ya siku mbili ya kukagua ujenzi wa miradi ya maji na ametembelea ujenzi wa mradi wa tenki wa Sahwa, Wilayani Nyamagana na mradi wa ujenzi wa tenki wa Buswelu Wilayani Ilemela ili kujidhirisha na hatua iliyofikiwa sambamba na kuzungumza na wasimamizi wake.

Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Maryprisca Mahundi (katikati) wakati wa ziara yake kwenye mradi wa tenki la maji la Sahwa, Wilayani Nyamagana.
Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Maryprisca Mahundi (katikati) akielekeza jambo wakati wa ziara yake kwenye mradi wa tenki la maji Sahwa, Wilayani Nyamagana.
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Dkt. Phillis Nyimbi akizungumza wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Maryprisca Mahundi (katikati) kwenye mradi wa tenki la maji Sahwa, Wilayani Nyamagana.
Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Mwanza (MWAUWASA), Mhandisi Leonard Msenyele (kulia) akizungumza wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Maryprisca Mahundi (katikati) kwenye mradi wa ujenzi wa tenki la maji la Buswelu, Wilayani Ilemela. Kushoto ni Mkuu wa wilaya hiyo, Dkt. Severine Lalika
Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Maryprisca Mahundi (wa pili kushoto) wakati wa ziara yake kwenye mradi wa tenki la maji la Buswelu, Wilayani Ilemela.
Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Maryprisca Mahundi (katikati) wakati wa ziara yake kwenye mradi wa tenki la maji la Buswelu, Wilayani Ilemela.



Post a Comment

0 Comments