Header Ads Widget

DC MBONEKO AKERWA KUKITHIRI UCHAFU MACHINJIO YA MANISPAA, ATOA MAAGIZO….ALIYEPIGA MHURI NYAMA ISIYOFAA ASAKWE


 Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko akizungumza na baadhi ya watendaji wa serikali wanaosimamia machinjio ya manispaa ya Shinyanga iliyopo eneo la Nguzo Nane.
 
Na Damian Masyenene, Shinyanga
MKUU wa Wilaya ya Shinyanga mkoani hapa, Jasinta Mboneko ameonyesha kukerwa na kusikitshwa na hali ya kukithiri kwa uchafu na mazingira yasyo ya kuridhisha katika machinjio ya Manispaa ya Shinyanga, hivyo kulazimika kutoa maagizo kwa wasimamizi kuhakikisha kuwa ifikapo kesho Januari 26, mwaka huu usafi uwe umefanyika.

DC Mboneko ametoa maagizo hayo leo alipotembelea machinjio hiyo ikiwa ni ufuatiliaji wa sakata la nyama ya ng’ombe isiyo halali iliyoingizwa kwenye machinjio hiyo kinyume na taratibu.

Akiwa katika machinjio hiyo akizungumza na viongozi mbalimbali akiwemo afisa mifugo wa wilaya, mkaguzi mkuu wa nyama manispaa ya Shinyanga, Verani Mwaluko, Mwenyekiti wa Mtaa wa Majengo Kata ya Kambarage, Majjid Ally na afisa afya kata ya Kambarage, Costancia Michael, Mkuu huyo wa wilaya amesema kuwa eneo la machinjio ni chafu kuliko maelezo na mazingira yanasikitisha na kunuka sana, hali ambayo itawafanya walaji kupata magonjwa.

“Lazima pawe pasafi na kesho nitapita hapa nikute mabadiliko hapa. Muda ambao watu hawafanyi uchinjaji muutumie kufanya usafi, muwabane watu wafanye usafi kabla ya kuchinja ama baada ya kuchinja,” ameagiza.

Akizungumzia sakata la nyama ya ng’ombe inayodhaniwa kuwa kibudu iliyoingizwa katika machinjio hiyo kinyume na utaratibu, DC Mboneko amepiga marufuku mnyama aliyekufa kuletwa buchani na marufuku kusafirisha nyama kuleta buchani kwa pikipiki ikiwa imebebwa kwenye sandarusi.

“Mifugo isiyo halali isiingie kwenye machinjio yetu, likijirudia tena hili basi mtaadhibiwa vikali idara ya mifugo. Hili lisijirudie tena. Tunaomba sana, wale wanaochinja wazingatie taratibu za uchinjaji.

Tunataka nyama yote inayoingia kwenye bucha zetu iwe ni halali, aliyeleta na aliyepokea na kugonga mhuri tunawataka tuwawajibishe. Wauza nyama zingatieni taratibu za afya, na msipokee nyama isiyoeleweka na uongozi wa wafanyabiashara wa nyama katika soko la Nguzo Nane usimamie vyema usafi na kutoingizwa nyama isiyo halali,” amesema.

Kwa upande wake, Mkaguzi Mkuu wa Nyama Manispaa ya Shinyanga, Verani Mwaluko ameahidi kuyatekeleza maagizo yote kuhusu usafi na ukaguzi katika machinjio hiyo, huku akibainisha kuwa ubebaji nyama kwenye sandarusi na bodaboda (pikipiki) umepigwa marufuku na watakaoendeea basi watashughulikiwa.

Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa Majengo Kata ya Kambarage ilipo machinjio hiyo, Majjid Issa Ally amesema uongozi wa mtaa umeyapokea maagizo hayo na utaingia kazini kuyafanyia kazi, huku Afisa Afya Kata ya Kambarage, Costancia Michael akieleza kuwa uchukuaji nyama kiholela kutoka kwenye machinjio hiyo hauruhusiwi na kuwataka wasimamizi wakiwemo maafisa mifugo waruhusu magari yaliyosajiliwa kisheria kwa ajili ya kubeba nyama.

Mhasibu wa Umoja wa Wafanyabiashara wa Nyama Manispaa ya Shinyanga, Ngassa Mashema amesema suala la nyama isiyo halali kuingizwa sokoni linasababishwa na wafanya biashara wengi kuendeshwa na tamaa na kutaka ng'ombe wa bei rahisi, ambapo ameahidi kuyafanyia kazi maagizo ya Serikali na kwamba suala hilo halitojitokeza tena.

Akizungumza baada ya kulalamikiwa na wafanyabiashara wengi kuwa anauza nyama bei rahisi na kumaliza mapema akihusishwa na uuzaji wa nyama isiyo halali na kumlazimu Mkuu wa Wilaya kumfuata nyumbani kwake kufahamu undani wa jambo hilo, Mwenyekiti Wafanyabiashara wa Nyama Manispaa ya Shinyanga, Abdi Kidodi amekanusha tuhuma hizo na kueleza ng’ombe wote anawachinjia kwenye machinjio ya manispaa na wanakaguliwa na wataalam wa afya.

“Sakata hili na hizi lawama zinakuja kwa sababu kulizuka mgogoro wa bei ya nyama wapo waliotaka tuuze kilo moja Sh 7,000 sisi tukakataa na kujiengua tukaunda umoja wetu tukabaki na kilo moja Sh 6,000, kwahiyo kuna mgawanyiko wa makundi mawili na hapo ndipo kunatengenezwa hizi tuhuma zisizo za kweli,” amefafanua.

Akitolea ufafanuzi suala la kupanda kwa bei ya nyama ya ng’ombe katika manispaa ya Shinyanga, Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko amesema kuwa tayari amepokea malalamiko ya maandishi kutoka kwa wananchi juu ya jambo hilo na amekwishawaagiza maofisa biashara na mifugo kukaa na wafanyabiashara waweke bei moja ambayo ipo kila mahali.

"Kwanini sisi Shinyanga ambako mifugo inatoka ndiko bei iko juu, alafu hawa ng'ombe wanaenda mikoa mingine lakini wao hawajapandisha bei. Kwahiyo tuangalie bei ambayo ipo, tusiwaumize wananchi,” ameagiza.

NYAMA YA NGURUWE

Akizungumzia mlipuko wa ugonjwa wa homa ya Nguruwe ulioanzia katika wilaya ya Kahama, DC Mboneko amekazia maelekezo ya serikali ya marufuku ya biashara ya nyama ya nguruwe (Kitimoto), huku akiwataka maofisa mifugo kupita kwenye bucha kukagua na kutoa taarifa, pia kuwatembelea wafugaji kuwaelimisha na kufanya ukaguzi kuhakikisha biashara hiyo haifanyiki.

“Mfike kwa wafugaji na wafanyabiashara muwaambie, mkague pia maeneo yote ya nyama choma. Maafisa mifugo wa halmashauri na Kata wapite kukagua mifugo na wabainishe dalili za ugonjwa huo ili wafugaji wazifahamu, vilevile mpite kwenye yombo vya habari kuelimisha, muwafute wafugaji kuwapa maelekezo na kufanya ukaguzi.

“Kila mtu anayefuga nguruwe ahakikishe anatoa taarifa haraka kwa mamlaka za serikali hatua ziweze kuchukuliwa kunusuru wananchi. Atakayekutwa anafanya biashara hii na kukiuka maagizo ya serikali atachukuliwa hatua,” ameagiza.

Akieleza dalili za ugonjwa huo, Mkaguzi Mkuu wa Nyama Manispaa ya Shinyanga, Verani Mwaluko amesema kuwa homa ya nguruwe husababishwa na virusi vinavyotoka kwenye nguruwe wa porini na kusambazwa na vitu vingi (mwingiliano wa wahudumu zizini, mabaki ya chakula cha nguruwe) kwenda kwenye nguruwe wanaofugwa nyumbani.

Amesema dalili zake ni sehemu za masikio, mkia na tumboni zinakuwa nyekundu sana na nguruwe kutetemeka na kukaa chini. 


Muonekano wa hali ilivyo katika machinjio ya Manispaa ya Shinyanga iliyopo eneo la Nguzo Nane kata ya Kambarage
 
 
 
 
DC Mboneko akiendelea na ukaguzi katika machinjio hiyo




Baadhi ya maeneo ya machinjio hiyo ambazo zimeonekana kuwa chafu na kulalamikiwa na Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko na kutaka wasimamizi wafanye usafi haraka
 
DC Mboneko (kulia) akizungumza na wafanyabaishara wa nyama katika soko la Nguzo Nane
 
 
 
DC Mboneko (kulia) na Mkaguzi Mkuu wa Nyama Manispaa ya Shinyanga, Verani Mwaluko wakilitazama vazi la muuza nyama ambalo limeonekana kuwa chafu kukithiri, hivyo aawataka wauza nyama kuwa wasafi
 
Mkaguzi Mkuu wa Nyama Manispaa ya Shinyanga, Verani Mwaluko
Mwenyekiti wa Mtaa wa Majengo Kata ya Kambarage, Majjid Issa Ally

Afisa Afya wa Kata ya Kambarage, Costancia Michael
 
Mwenyekiti wa Wafanyabiashara wa Nyama Manispaa ya Shinyanga, Abdi Kidodo

Muonekano wa machinjio ya Manispaa ya Shinyanga lililopo eneo la Nguzo Nane





Post a Comment

0 Comments