Header Ads Widget

BUTONDO ACHANGIA SH. MILIONI 42.6 KUKAMILISHA MADARASA, MAABARA NA OFISI YA POLISI KISHAPU


Mbunge wa Jimbo la Kishapu mkoani Shinyanga, Boniface Butondo (anayezungumza) akiwashukuru wananchi wa Kata ya Talaga wilayani Kishapu baada ya kuonyesha uzalendo wakuchangia fedha za ujenzi wa vyumba vya madarasa

Na Suzy Luhende , Kishapu
Mbunge wa Jimbo la Kishapu mkoani Shinyanga, Boniface Butondo (CCM), amechangia jumla ya Shilingi Milioni 42.6 kutoka kwenye mfuko wa jimbo kwa ajili ya kukamilisha miradi 15 ya maendeleo iliyopo wilayani humo yakiwemo madarasa na maabara yanayojengwa kwa nguvu za wananchi ikiwa ni pamoja na ofisi ya Jeshi la polisi ya wilaya inayosimamiwa na wananchi.

Pia Butondo amewataka wasimamizi wa miradi hiyo wasimamie ipasavyo iweze kujengwa kwa kiwango kinachotakiwa ili iweze kudumu muda mrefu, huku akikemea tabia ya watendaji wa vijiji na kata ambao hawasomi taarifa za mapato na matumizi kwa wananchi, kwani kufanya hivyo kunasababisha kuwakatisha tamaa na kutokuwa na imani na viongozi wao,

Akizungumza na wananchi ambao walijitokeza kwenye miradi aliyokuwa akiikagua kwenye ziara yake ya siku mbili ya kutembelea miradi mbalimbali iliyoko wilayani humo, alisema lengo lake ni kutekeleza agizo la Waziri Mkuu, Kasim Majaliwa la kuhakikisha wanafunzi wote waliofaulu kidato cha kwanza ifikapo Februari mwaka huu wawe wameshaanza masomo bila kukosa.

"Fedha hizi zitakamilisha kujengea madarasa, maabara na ofisi ya jeshi la polisi wilayani humo inayojengwa kwa nguvu za wananchi, kwa kuwa serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ina malengo makubwa ya kuondoa ujinga na maladhi hivyo itasaidia elimu bure bila malipo kwa wanafunzi wote," amesema Butondo.

"Nawaomba sana viongozi wote msiache kuwasomea mapato na matumizi wananchi kwani mkifanya hivyo mtawarejeshea imani na watawaamini na kuwaondolea mashaka," ameongeza Butondo.

Aidha aliwapongeza wananchi wa wilaya hiyo kwa kujitolea kuchangia katika miradi ya maendeleo kwa kuchangia fedha na nguvu kazi zao katika kutekeleza miradi, hivyo amewataka waendelee kujitoa kwa sababu Kishapu itajengwa na wanakishapu wenyewe.

"Nimewapongeza sana wananchi wangu kwa kujitoa kuchangia miradi nawaomba muendelee kuwa na moyo huo huo usikubali mtu awakatishe tamaa kwani nimetembelea miradi yenu mko vizuri sana na mimi nimeona niwasapoti katika kupauwa baadhi ya majengo yenu, nawashukuru sana tukaze mwendo ili tuweze kufanya makubwa zaidi," amesema Butondo.

Akiwa katika ziara yake Butondo aliwashukuru wananchi kwa kumchagua kuwa mbunge wao na madiwani na pia kumchagua Rais Jonh Pombe Magufuli kuwa Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania, hivyo wataendelea kushirikiana kwa pamoja ili kuhakikisha wanaleta maendeleo katika jimbo la Kishapu.

Baadhi ya wananchi wa Kata ya Talaga wilayani humo Kabanga Lubaliji na Masanja Kija walimpongeza mbunge huyo kwa kuchangia na kuunga mkono juhudi zilizoanzishwa na wananchi wake, huku wakishukuru pia kwa mkakati wake wa kuchangia fedha zingine kwenye hatua za upauaji wa vyumba vya madarasa.

"Tunakushukuru sana mbunge wetu Boneface Butondo kwa kutuletea fedha ili tufanye maendeleo, zamani tulikuwa hatuambiwi hivi tulikuwa tukisikia tu lakini kwa sasa kuna uwazi, tumefurahi sana, hivyo tu Mungu aendelee kukulinda ili uweze kuleta mabadiliko katika jimbo letu tupo bega kwa bega na wewe," alisema Ubaliji.

Aidha wakiwa katika ziara hizo walizindua kamati ya jimbo kwa jimbo kwa ajili ya kutambulisha wajumbe wa mfuko wa jimbo wapya ambapo waliazimia kusapoti miradi ya ujenzi wa madarasa na maabara na miradi mbalimbali wilayani humo.


Mbunge Butondo akikagua maendeleo ya ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule ya sekondari Isoso.

Mbunge wa Kishapu, Boneface Butondo akifanya kazi na wananchi wa kata ya Talaga wilayani humo wanaoendelea na ujenzi wa madarasa

Mbunge Butondo akishiriki katika ujenzi huo kwa kumimina zege kwenye msingi wa jengo la darasa
Mbunge Butondo akishiriki kwenye ujenzi huo kwa kumimina mchanga kwa kutumia koleo
Mbunge Butondo akitoa maelekezo kwa Diwani wa kata ya Kishapu, Joel Ndetoson (katikati) jinsi ya kusimamia ujenzi wa madarasa na maabara katika shule ya sekondari Isoso.
Mbunge Butondo akitoa maelekezo kwa Diwani wa kata ya Kishapu, Joel Ndetoson (katikati) jinsi ya kusimamia ujenzi wa madarasa na maabara katika shule ya sekondari Isoso. 
Mbunge Butondo akitoa maelekezo kwa diwani wa kata ya Ukenyenge Underson Mandia ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kishapu mkoani Shinyanga kwa ajili ya kuongezea jengo la shule ya sekondari

Post a Comment

0 Comments