Header Ads Widget

CHANGAMOTO YA KUPATA TAARIFA KUTOKA TAASISI ZA UMMA


Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Haki ya kupata taarifa nchini Tanzania imeainishwa, kusisitizwa na kulindwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 pamoja na Sheria ya Kupata Taarifa ya mwaka 2016 na Kanuni zake. Kwa mujibu wa sheria hizi, kila Mtanzania anayo haki ya kupokea na kutoa taarifa zinazoathiri maisha yake ya kila siku.

Haki ya kupata taarifa inahusisha uhuru wa raia kupata taarifa zenye maslahi kwa umma kutoka wizara, idara na taasisi za umma. Taarifa zenye maslahi kwa umma zinajumuisha taarifa kuhusu huduma mbalimbali za kijamii zinazoathiri haki, ustawi na maendeleo ya raia katika maeneo ya utawala bora, afya, elimu, miundombinu, na upatikanaji wa haki.

Ripoti mbalimbali zinaonesha uwepo wa changamoto ya kutafuta na kupata taarifa zenye maslahi kwa umma kutoka kwenye vyombo vya serikali na taasisi za umma nchini Tanzania (MISA, 2020; MCT, 2019). Tafiti zilizofanyika zinaonyesha kwamba maombi ya wananchi wengi ya kupata taarifa kutoka taasisi za serikali hayakujibiwa na/au kukataliwa. Mfano. Utafiti uliofanywa na MISA Tanzania mwaka 2020 uliohusisha wizara na taasisi 14 nchini Tanzania umeonesha vikwazo mbalimbali vinavyokwamisha wananchi kupata taarifa zinazohodhiwa na taasisi husika.

Ingawa wananchi wengi wana mwamko wa kutafuta na kupata taarifa kutoka taasisi za umma pamoja na kuongezeka kwa vyanzo vya utoaji taarifa ikiwemo tovuti na mitandao ya kijamii, bado upatikanaji wa taarifa imeendelea kuwa kikwazo. Mojawapo ya changamoto hizo zilizoainishwa kwenye ripoti ya utafiti wa MISA Tanzania zinahusisha kukosekana kwa afisa anayeshughulikia maombi ya taarifa, ucheleweshaji wa utoaji mrejesho na/au kutotolewa mrejesho wa maombi ya kupata taarifa.

Kwa kiasi kikubwa, ukuaji wa sekta ya mawasiliano nchini Tanzania kunakochochewa na maendeleo ya teknolojia ya mawasiliano hususan matumizi ya simu za kiganjani na upatikanaji wa intaneti umerahisisha utafutaji na upatikanaji wa taarifa kutoka taasisi za serikali. 

Kwa mujibu wa ripoti ya MISA Tanzania, wizara zote za serikali na taasisi za umma zinatoa taarifa zake kupitia tovuti na mitandao ya kijamii. Matumizi ya mitandao ya kijamii hususan Facebook, Instagram, Twitter na YouTube katika kutoa taarifa mpya kwa wananchi yameongezeka miongoni mwa taasisi husika na hivyo kuongeza uelewa kuhusu taasisi na/au wizara husika.

Hata hivyo, ripoti imebaini kwamba pamoja na uwepo wa vyanzo hivyo vya taarifa bado kuna changamoto ya kukosekana kwa taarifa muhimu na ucheleweshaji wa kuweka taarifa mpya katika tovuti bado kikwazo kwa wananchi kupata taarifa za taasisi za serikali na umma.

Kwa upande mwingine, haki ya wananchi kupata taarifa imeathiriwa na uelewa hafifu wa aina ya taarifa zinazotafutwa, vyanzo vya kupata taarifa husika, taratibu za kupata taarifa na namna sahihi ya matumizi ya taarifa inayoombwa.

 Aidha, uwepo wa vifungu vya sheria na kanuni vinavyozuia wananchi na wanahabari kupata na kutoa taarifa zenye maslahi kwa umma. Sheria ambazo asasi za kiraia na haki za binadamu, mashirika yasiyo ya kiserikali na wananchi wanapaza sauti kutaka vifungu vyake vifanyiwe marekebisho ni pamoja na Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari, 2016; Sheria ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania, 2003; Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (Maudhui ya Mtandaoni na Utangazaji) 2016; na Sheria ya Makosa ya Mtandao, 2015. Mabadiliko ya sheria hizi na nyinginezo sio tu ni muhimu katika kuhimiza uwazi, demokrasia na utawala bora lakini pia italinda haki ya kikatiba ya kila raia wa Tanzania ya kupata na kutoa taarifa zenye maslahi kwa umma.

Post a Comment

0 Comments