Header Ads Widget

FOMU ZA USPIKA, UMEYA KUANZA KUTOLEWA LEO


Aliyekuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai

FOMU za kuwania nafasi mbali mbali ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) zimeanza kutolea leo na kesho kuanzia saa mbili asubuhi hadi saa 10 jioni.

Taarifa ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole imesema wenye sifa stahiki kwa mujibu wa sheria na wanao omba wafikiriwe na Chama kwa nafasi ya Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Naibu Spika, Meya wa Halmashauri ya Jiji au Manispaa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya wajitokeze kuchukua fomu hizo.

“Sambamba na sifa stahiki kwa mujibu wa sheria za nchi, waombaji wote lazima wawe wanakidhi sifa za uongozi kwa mujibu wa wa katiba ya CCM ya mwaka 1977 toleo la mwaka 200 ikisomwa pamoja na kanuni ya maadili na uongozi toleo la mwaka 2017,” amesema Polepole na kuongeza

“Kwa nafasi za spika na naibu spika wa bunge, fomu zinapatikana katika Ofisi ya Makao Makuu ya CCM jijini Dodoma, Ofisi ndogo ya Makao Makuu, Lumumba jijini Dar es Salaam na Ofisi Kuu ya CCM - Kisiwandui Zanzibar.”

Amesema kwa nafasi ya Meya wa jiji au Manispaa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya fomu zinapatikana katika ofisi za CCM za Wilaya.

“Tarehe rasmi ya kuchukua na kurejesha fomu kwa nafasi zote tajwa hapo juu ni leo Novemba 2 na kesho kesho Novemba 3 saa 10 jioni,” amesema Polepole 

Aidha amesema taarifa iliyotolewa izingatiwe na vikao vya uongozi na uamuzi ngazi ya Mkoa na wilaya kwamba Novemba 4, 2020 ziketi Kamati za Siasa za Halmashauri Kuu za CCM za Wilaya na kutoa mapendekezo na Novemba 5 ziketi Kamati za siasa za Halmashauri Kuu za CCM Mkoa na kutoa mapendekezo

Amesema mapendekezo ya Kamati za Siasa za Wilaya na Mkoa yawe yamefika ofisini kwa Katibu Mkuu wa CCM jijini Dodoma si zaidi ya saa 10 jioni Novemba 6, 2020.

“Niwatakie kila la kheri katika kujitafakari, kujitathmini na kumtanguliza Mungu mbele kwa wale watakao omba kufikiriwa na Chama kwa dhamana tajwa, nitawakie utekelezaji wa haraka wa taarifa hii na maelekezo yaliyomo ndani yake,” Polepole.

 CHANZO: HABARI LEO

Post a Comment

0 Comments