Header Ads Widget

WALIOKUWA WATUMISHI TPA WASOMEWA MASHTAKA MATANO, KESI YAAHIRISHWA


WASHTAKIWA watatu ambao walikuwa watumishi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) leo Oktoba 12, 2020 wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Kigoma na kusomewa mashtaka matano yanayowakabili.

Watu hao ambao ni Eliya Stefano Ntinyako, Morris Charles Mchindiuza (aliyekuwa Meneja wa Bandari ya Kigoma), Herman Ntiboto Shimbe (aliyekuwa afisa uhasibu TPA Kigoma) na Lusabilo Anosisye Mwakyusa (aliyekuwa ofisa rasilimali watu TPA Kigoma) walifikishwa mahakamani hapo na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa makosa ya rushwa na uhujumu uchumi.

 Ambapo katika taarifa ya TAKUKURU mapema leo, ilisema kuwa watuhumiwa hao wanne wanakabiliwa na makosa ya rushwa, uhujumu uchumi, kuisababishia hasara ya Sh 619, 278, 260.52 Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) pamoja na ukwepaji kodi unaofikia jumla ya Sh 37, 837, 409.26.

Kesi hiyo ya Uhujumu Uchumi namba 5 ya mwaka 2020 imesomwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Kigoma mbele ya Hakimu Keneth Mtembei na washtakiwa kusomewa mashtaka matano yanayowakabili.

Shtaka la kwanza ni kuongoza genge la uharifu kinyume na aya ya 4(1)(d) ya jedwali la kwanza likisomwa pamoja na vifungu vya 57(1) na 60(2) vya Sheria ya Uhujumu Uchumi sura ya 200 kama ambavyo imefanyiwa marejeo mwaka 2002.

Katika Shtaka la pili, watu hao wanakabiliwa na kosa la ufujaji na ubadhirifu kinyume na kifungu cha 28 (1) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa No.11/2007. 

Kosa la tatu ni kuisababishia mamlaka hasara kinyume na aya ya 10(1) ya jedwali la kwanza likisomwa pamoja na kifungu cha 57(1) na 60(2) vya Sheria ya Uhujumu Uchumi, Sura ya 200 kama ambavyo imefanyiwa marejeo mwaka 2002. 

Shtaka la nne ni kushindwa kulipa kodi kinyume na kifungu cha 83(a) cha Sheria ya Usimamizi wa Kodi Namba 10 ya Mwaka 2015. 

Shtaka la tano ni kutakatisha fedha kinyume na kifungu cha 12(a) na 13(a) cha Sheria ya Kuzuia Utakatishaji Fedha No. 12 ya Mwaka 2006 ikisomwa pamoja na aya ya 22 ya jedwali la kwanza la vifungu vya 57(1) na 60(2) vya Sheria ya Uhujumu Uchumi Sura ya 200 kama ambavyo imefanyiwa marejeo Mwaka 2002.

Hata hivyo kesi hiyo imehairishwa ambapo italetwa tena mahakamani hapo kwa ajili ya kutajwa mnamo Oktoba 26, mwaka huu.


Post a Comment

0 Comments