Header Ads Widget

NYUMBA YA MBUNGE KATAMBI YANUSURIKA KUCHOMWA MOTO, WANNE WAKAMATWA, MAKAMBA NAYE AHUSISHWA


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, ACP Debora Magiligimba

Na Damian Masyenene, Shinyanga 
WATU wanne wanashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga kwa tuhuma za kuhusika na tukio la kutaka kuchoma moto nyumbani kwao na Mbunge Mteule wa Jimbo la Shinyanga Mjini, Patrobas Katambi (CCM). 

Ambapo Jeshi hilo linafanya uchunguzi kuhusiana na tukio hilo la kuchoma nyumba moto lililotokea Mtaa wa Ushirika ndani ya Manispaa ya Shinyanga nyumbani kwao na Mbunge Mteule, Katambi. 

Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari leo Oktoba 30, 2020 mjini Shinyanga, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, ACP Debora Magiligimba, amesema kuwa tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia Ijumaa Oktoba 30, mwaka huu majira ya saa 6:45 usiku, mbunge huyo akiwa amelala nyumbani na ndugu zake walisikia kishindo juu ya paa la choo cha nje amacho kipo katika eneo la uzio wa nyumba hiyo ndipo walipotoka nje na kuona moto ukiwaka juu ya paa hilo pamoja na dumu lenye mafuta aina ya petrol. 

Kamanda Magiligimba ameeleza kuwa, wakati wakiendelea kuzima moto huo waliona gari aina ya Toyota Klugger lenye rangi ya silver likikimbiliwa na watu wawili na kisha watu wale waliingia ndani ya gari lile na kutoweka, baada ya kufanikiwa kuzima moto huo waliona gari lile likipita barabara ya lami ya Shinyanga-Mwanza ndipo walipoamua kulifuatilia. 

“Dereva baada ya kugundua kuwa wanafuatiliwa aliamua kuingia hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga na kuliacha gari hilo kasha kukimbia. Wakati wa kuwaweka chini ya ulinzi watu hao ilitokea prukushani ndani ya uzio wa hospitali na gari ya polisi iliyokuwa doria ilifika mapema na kufanikiwa kuwakamata watu wawili,” amesema. 

ACP Magiligimba amewataja watu waliokamatwa wakiwa ndani ya gari hilo kuwa ni Wilson Mhando Suluti (30) na Jackson Raphael Peter (27) wote wakazi wa Bugweto wakiwa kwenye gari hilo lenye namba za usajili T 729 DFP aina ya Toyota Klugger rangi ya silver mali ya Salome Makamba aliyekuwa Mgombea Ubunge Jimbo la Shinyanga Mjini Kupitia CHADEMA, ambao ilibainika kuwa ndiyo waliokuwa eneo la tukio kulingana na mavazi waliyovaa. 

“Baada ya mahojiano watu hao walikiri kuwa gari hilo ni la Salome Makamba na dereva aliyetoroka ni Timoth Makamba ambaye ni mdogo wake mmiliki wa gari hilo. Polisi walifika nyumbani kwa Salome Makamba na kufanya upekuzi kasha kuwakamata watu wengine wawili,” ameeleza ACP Magiligimba. 

Amewataja watu hao waliokutwa kwenye nyumba ya Salome Makamba baada ya upekuzi, kuwa ni Justin Owesiga (35) mfanyabiashara na mkazi wa kata ya Ndala mjini Shinyanga pamoja na Gibson Mkongwa (31) mkazi wa Iringa. 

Kamanda huyo wa Polisi amesema kuwa juhudi za kuwatafuta na kuwakamata Salome Makamba na Timoth Makamba ambaye ndiye dereva wa gari lililotelekezwa hospitalini zinaendelea, ambapo gari husika linashikiliwa pamoja na watuhumiwa hao wane na watafikishwa mahakamani upelelezi utakapokamilika. 

“Natoa wito kwa wanasiasa na wafuasi wao kuacha mihemko ya kisiasa inayopelekea uvunjifu wa amani, badala yake wafuate sheria, kanuni na taratibu za uchaguzi, na jeshi la polisi halitasita kamwe kuchukua hatua kali za kisheria kwa mtu au watu na kikundi chochote chenye nia ya kuvuruga amani nchini,” amesisitiza. 

Ikumbukwe kuwa, Salome Makamba alikuwa mahabusu baada ya kukamatwa na Jeshi la Polisi usiku wa Oktoba 28, 2020 kwa kosa la kumshambulia, kumpiga na kumuumiza msimamizi wa uchaguzi kituo cha Bugweto manispaa ya Shinyanga, ambapo jana (Alhamisi) Oktoba 29, mwaka huu aliachiwa kwa dhamana majira ya saa 9 Alasiri.
Aliyekuwa Mgombea Ubunge Jimbo la Shinyanga Mjini kupitia Chadema, Salome Makamba
Mbunge Mteule wa Jimbo la Shinyanga Mjini, Patrobas Katambi

Post a Comment

0 Comments