Header Ads Widget

DC MBONEKO AUFUNGA MNADA WA ZAMANI TINDE, AUHAMISHIA ENEO JIPYA, ATOA ONYO KWA WAFANYABIASHARA

 Wananchi wakiwa katika mnada wa Tinde wilayani Shinyanga kwa ajili ya kuuza na kununua bidhaa mbalimbali

Na Shinyanga Press Club Blog
Serikali ya Wilaya ya Shinyanga imeufunga mnada wa Tinde ulioko katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga na kuuhamishia katika eneo lingine lenye ukubwa wa zaidi ya ekari 30, lengo likiwa ni kutatua changamoto ufinyu wa eneo na mrundikano wa watu unaoweza kusababisha magonjwa ya mlipuko, huku eneo likiloachwa wazi likitarajiwa kutumika kwa shughuli zingine za kijamii ikiwa ni pamoja na stendi ya mabasi. 

Shinyanga Press Club Blog imefika katika eneo hilo jipya la mnada na kukuta wananchi wakiendelea na shughuli za kibiashara kama kawaida baadhi wakiwa wameridhika, lakini wengine wakilalamikia changamoto mbalimbali ikiwemo baadhi ya wafanyabiashara kivuruga utaratibu waliowekewa na kupanga bidhaa pembezoni mwa barabara kuu ya kielekea kahama hali ambayo imeonekana kuwanyima riziki walioko ndani ya mnada. 

Mmoja wa wafanyabiashara wa nguo katika emnada huo, Gerald Mchau amesema kuhamishiwa mnada katika eneo hilo imewasaidia kupunguza mbanano uliokuwepo katika mnada wa awali lakini hofu yake ni wakati wa mvua kwakuwa eneo hilo lilikuwa na majaruba ya mpuna. 

Aidha wafanyabiashara wengine wameishukuru Serikali ya Wilaya ya Shinyanga pamoja na halmashauri kutoa eneo hilo bure hali ambayo imetoa nafasi pana kwa baadhi ya wajasiriamali kujiendeleza kiuchumi. 

Kufuatia hali hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko akapiga marufuku wafanyabiashara kupanga bidhaa zao na kufanya biashara pembezoni mwa barabara kuu na kuwaagiza viongozi wa mnada kushirikiana na polisi kusimamia kikamilifu hali hiyo isijirudie tena. 

Nao baadhi ya viongozi na wasimamizi wa mnada huo akiwemo Christopher Malengo ambaye ni msimamizi wa minada kutoka halmashauri ya wilaya ya Shinyanga wamesema mnada huo kwa sasa utaingiza mapato makubwa kwasababu umewekwa katika eneo zuri ambalo linamvutia kila anayepita katika maeneo hayo. 

Wakati huo huo, Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko amepiga marufuku magari ya abiria kushusha na kupakia pembezoni mwa barabara kuu na kuwataka madereva kuingia ndani katika eneo likilotengwa kwa ajili ya kupakia abiria na mizigo ili kuondoa hatari inayoweza kujitokeza barabarani. 

Amesema Serikali ina nia njema kwa wananchi na kudai kuwa damira yake ni kuhakikisha kila mwananchi anakuwa na maisha yenye tija huku akiwataka wajasiriamali wote wa mnada huo kuwa na viongozi katika kila kundi kulingana na biashara zao akitaja baadhi ya makundi kuwa ni wafanya biashara wa nguo za mtumba, viatu vya mtumba na spesho, mama lishe, wauza ng'ombe,mbuzi, wauza dawa za asili, mboga mboga, nafaka nakadhalika. 
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko akizungumza baada ya kuuzindua mnada wa Tinde katika eneo jipya

DC Mboneko akitazama bidhaa mbalimbali katika mnada huo
DC Mboneko akisisitiza jambo ambapo amepiga marufuku magari ya abiria kupakia pembezoni mwa barabara na wafanyabiashara katika mnada huo kujiepusha kupanga bidhaa zao pembezoni mwa barabara kwani ni hatari endapo ajali itatokea.
DC Mboneko akiendelea na ukaguzi katika mnada huo
Mfanyabiashara akiuza mbuzi kwenye mnada wa Tinde
Akina mama wakiuza vyombo  vya ndani katika mnada huo
Shughuli zikiendelea katika mnada wa Tinde

Biashara ya nyama choma ikiendelea
Mmoja wa wafanyabiashara akina mama katika mnada huo akiwauzia samaki wateja waliofika mnadani hapo
Mmoja wa wakazi wa Tinde akinunua nyanya katika mnada huo
Mfanyabiashara akisubiria wateja kununua bidhaa
Biashara ya Ng'ombe mnadani hapo ikiendelea
Msimamizi wa minada kutoka halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, Christopher Malengo akitoa ufafanuzi wa mambo mbalimbali 


Baadhi ya wafanyabiashara katika mnada huo wakizungumzia hatua iliyochukuliwa na Serikali ya Wilaya ya Shinyanga kuufunga mnada wa zamani na kuuhamishia eneo jipya lenye ukubwa wa kutosha, ambao wamepongeza hatua hiyo.


 Kiongozi wa wafanyabiashara wa vyombo vya ndani mnadani hapo akielezea mambo mbalimbaliPost a Comment

0 Comments