Header Ads Widget

LICHA YA UZALISHAJI MWINGI WA CHAKULA, WAZIRI HASUNGA ASHANGAZWA WATOTO MILIONI 3 KUWA NA UDUMAVU



Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga

Na Damian Masyenene- Shinyanga Press Club Blog 
WATOTO takribani Milioni 3 nchini wametajwa kuwa na udumavu unaotokana na lishe duni, ambapo mikoa inayoongoza kwa uzalishaji mwingi wa chakula imebainika kuwa ndiyo yenye idadi kubwa ya watoto walio na udumavu huo.
Jambo hilo limemshangaza Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga, ambaye ametoa maelekezo kwa mikoa hiyo kufanya jitihada za makusudi kuondoa tatizo hilo, pia kuitekeleza kwa vitendo miongozo miwili ya lishe iliyozinduliwa juu ya uboreshaji wa lishe nchini.
Hayo yamebainika leo Agosti 1, 2020 katika uzinduzi wa maonesho ya Nane Nane kitaifa yaliyofanyika katika Viwanja vya Nyakabindi mkoani Simiyu yakihudhuriwa na Makamu wa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.
 Waziri Hasunga aliitaja mikoa hiyo kuwa ni Njombe yenye udumavu wa asilimia 53.6, Rukwa asilimia 47.9, Iringa asilimia 47.1, Songwe 43.3, Kigoma 42.3 na mkoa ulioongoza kwa uzalishaji wa chakula mwaka jana na mwaka huu, Ruvuma ukiwa na asilimia 42.2. 
"Watoto takribani milioni tatu wana udumavu nchini na mikoa ambayo inaongoza kwa uzalishaji wa chakula nchini ndiyo inayoongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya watu wenye udumavu kutokana na lishe duni. 
 
"Wananchi waeleimishwe namna ya kuboresha lishe zao ili tuwe na watu ambao wana lishe bora, wananchi watumie miongozo hiyo ili kuimarisha afya na lishe zao. " amesema.

Katika hatua nyingine Waziri Hasunga amesema wizara imeweka mikakati kadhaa ikiwemo kuhakikisha kuwa panakuwepo na chakula cha kutosha na malighafi kwa viwanda,ambapo kwa kipindi cha miaka mitano taifa limekuwa na utoshelevu wachakula kwa asilimia 120.

 "Tumedhamiria kuoboresha zaidi sekta ya uvuvi kwa kuongeza ufugaji wa samaki wenye tija ili kuongeza uzalishaji wa samaki kwa wingi zaidi.

"Usajili wa wakulima ili kupata takwimu sahihi na kuboresha huduma zao, k
ufanya mapitio sera ya kilimo ya mwaka 2013, kutoka kilimo cha kujikimu hadi kilimo cha biashara na tuna matumaini itakamilika kabla ya mwaka huu kuisha," amesema Waziri Hasunga.