Header Ads Widget

RAIS MSTAAFU KIKWETE MGENI RASMI 'WIKI YA MWANANCHI' YANGA


Rais Mstaafu wa awamu ya nne, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete

Na Shinyanga Press Club Blog
Agosti 30, 2020 ndiyo kilele cha tamasha la timu ya Yanga maarufu 'Wiki ya Mwananchi' ambayo ni maalum kuwakutanisha mashabiki na wapenzi wa klabu hiyo, kutambulisha wachezaji, benchi la ufundi na jezi zitakazotumika kwa msimu mpya wa kimashindano unaoanza Septemba 6, 2020.

Katika tamasha hilo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais Mstaafu wa awamu ya nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete na litafanyika katika uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam, ambapo Wana Jangwani watakipiga na timu ya Aigle Noir ya Burundi.
'Wiki ya Mwananchi' itafanyika Jumapili ya wiki hii zikiwa zimepita siku 8 tangu Watani wao wa jadi, Wekundu wa Msimbazi wafanye tamasha lao la Simba Day Agosti 22, 2020 na Azam FC wafanikishe tamasha lao la 'Azam Festival 2020' mnamo Agosti 23.

Wakati Diamond Platinumz akinogesha tamasha la Simba Day na Alikiba akipagawisha kwenye Azam Festival, Konde Boy 'Harmonize' yeye atatumbuiza kwenye 'Wiki ya Mwananchi' akiambatana na wasanii wengine kama Madee na Chege.