Header Ads Widget

POLISI MWANZA YAWASHIKILIA 4 TUHUMA ZA MAUAJI UKEREWE

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Jumanne Muliro

Na Shinyanga Press Club Blog
WATU wanne wanashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoani Mwanza kwa tuhuma za kupanga tukio la mauaji ya mtu mmoja wilayani Ukerewe mkoani humo.

Kwa mujibu wa taarifa ya jeshi hilo kwa vyombo vya habari jana Agosti 31, 2020 iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Jumanne Muliro ilisema kuwa watu hao wanashikiliwa wakihusishwa na tukio la Agosti 25, 2020.

Ambapo siku hiyo, majira ya 02:00 usiku usiku eneo la mission, Kata ya Nyamanga Kisiwa cha Ukara, Wilaya ya Ukerewe Mkoa wa Mwanza, Andrew Magai (48) ambaye ni Mkulima wa Kijiji cha Chibasi aliuawa kwa kupigwa sehemu mbalimbali za mwili na kukatwa na vitu vinavyodaiwa kuwa na ncha kali kwa madai kuwa marehemu kabla ya kifo chake aliwasafirisha watu ambao hawakutambulika kwenda kuvunja nyumba ya Magesa Simon. 

 Kwa mujibu wa jeshi hilo, chunguzi wa awali umebaini kuwa tukio la kuvunja nyumbani kwa Magesa Simon lilikua ni la kutengenezwa ili kuhalalisha mauaji yaliyotokea eneo hilo. 

Uchunguzi wa kina unaendelea ukihusisha wataalamu mbalimbali, ambapo mwili wa marehemu ulifanyiwa uchunguzi na daktari katika kituo cha afya Bwisya na kukabidhiwa kwa ndugu kwa mazishi. 

 Kamanda Muliro aliwataja waliofikishwa mahakamani leo (jana) Agosti 31, 2020 kuwa ni Magesa Simon (50),  Makanje Mgeta (28), Mkapa Magesa (24) na Selestini Datusi (22). 

 Watuhumiwa wote wamefikishwa mahakama ya Hakimu Mkazi kujibu tuhuma zinazowakabili. 

 "Jeshi la polisi mkoa wa Mwanza linawataka wananchi, wanasiasa wa vyama vyote kutojiingiza katika mambo ambayo yanaweza kuhamasisha uvunjaji wa sheria na kuvuruga amani na utulivu wa nchi, limeapa kuendelea kuchukua hatua kali kwa kila atakayekiuka sheria," amesema Kamanda Muliro.