Header Ads Widget

WATU WATANO WA FAMILIA MOJA MBEYA WAKAMATWA KWA TUHUMA ZA MAUAJI



JESHI la Polisi Mkoani Mbeya linawashikilia watu watano wa familia moja akiwemo mke wa marehemu kwa tuhuma za kumuua, Ally Mazinge (66) mkazi wa Ubaruku wilayani Mbarali.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo, Kamanda wa Polisi Mkoani hapa, Ulrich Matei amesema tukio hilo limetokea Juni 26, mwaka huu saa 00.40 usiku katika kitongoji cha Mbuyuni katika kijiji cha mpakani Kata ya Ubaruku.

Kamanda Matei amesema watuhumiwa hao walimvizia marehemu akiwa amelala kisha kumkata kwa panga sehemu ya shavu la kulia pamoja na kidevuni.

Aidha Matei amewataja watuhumiwa hao kuwa ni, Chausiku Mahmod (50) ambaye ni mke wa marehemu, Idrisa Ally (20), Hawa Ally (20),Salima Ally (19) na Jumanne Ally (30).

Akielezea zaidi Kamanda Matei alisema chanzo cha tukio hilo kuwa ni tamaa ya mali, kwani mke na watoto wa marehemu walipanga kuuza eneo wanaloishi ambalo mnunuzi alipanga kujenga kituo cha mafuta.

Amesema wakati wa uhai wake marehemu aliwakatalia kuuza eneo hilo kwa sababu sehemu ya eneo hilo kuna nyumba ambayo wanaishi, hivyo marehemu alionekana ni kikwazo katika mipango yao. Alisema upelelezi wa shauri hilo unaendelea na mara baada ya kukamilika watuhumiwa watafikishwa mahakamani.