Header Ads Widget

WAFANYABIASHARA KAHAMA WAMKUMBUKA HAYATI MKAPA, WAELEZA ALIVYOSAIDIA BIASHARA KUKUA



Na Ali Lityawi - Kahama
KIFO cha Rais wa awamu ya tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Benjamin William Mkapa aliyefariki usiku wa kuamkia Julai 24, 2020 kimeendelea kuwagusa Watanzania ambao wanaomboleza na kukumbuka mchango wake mkubwa katika maendeleo ya taifa.

Sehemu ya Watanzania hao ni kundi la wafanyabiashara wilayani Kahama mkoa wa Shinyanga, ambao wameeleza kuwa hawa hawatamsahau Hayati Benjamini Mkapa kutokana na jitihada kubwa alizozifanya za kuimarisha uchumi na kutengeneza mazingira rafiki kwa wafanyabiashara kuendesha shughuli zao ikiwemo kusafirisha bidhaa.

Mmoja wa Wafanyabiashara hao aliyezungumza na Shinyanga Press Club Blog ni Charles Daud maarufu kwa jina la 'Chale Hardware', ambaye amesema atamkumbuka Hayati Mkapa kwa juhudi zake za kuweka miundombinu ya barabara iliyoleta mafanikio ya kuimarisha biashara ya kimataifa na nchi jirani.

Mfanyabiashara Charles Daud

Daud amesema katika baadhi ya Mikoa ya Kanda ya Ziwa inayopakana na nchi jirani za Burundi, Rwanda, Congo DR, Sudani ya Kusini na Uganda, biashara imekua kwa kiasi kikubwa kutokana na miundombinu ya barabara iliyojengwa katika utawala wa Rais Mkapa.

Daud ambaye ni mfanyabiashara maarufu Mjini Kahama amesema kuwa awali kulikuwa na changamoto ya ukosefu wa barabara, hali ambayo ilisababisha kuchelewa kwa bidhaa kuwafikia wateja pindi wanapoagiza kutoka bandarini.

"Kutokana na hali hiyo wafanyabiashara tulikuwa tuatumia siku zaidi ya tatu kupata mahitaji na mizigo ambayo tuliagiza wakati huo tukiwa tumetumia gharama kubwa," amesema.

Aidha Daud amesema kuwa kutokana na kuimarika kwa miundombinu tangu kipindi cha awamu ya tatu kumekuwa na ushindani wa kibiashara na kutoa fursa kwa vijana kuchangamkia fursa mbalimbali za biashara hali iliyosababisha kukua kwa biashara na kuongezeka kwa ushindani baina yao.

Aliendelea kusema kuwa biashara kwa sasa imekuwa kubwa huku wafanyabiashara wakielewa majukumu yao kwa kulipa kodi kwa wakati bila kusukumwa.

“Sisi kama Wafanyabiashara wa Kahama hatutamsahahu Rais wa awamu ya tatu Benajmin Mkapa kutokana na kuimarisha miundombinu ya barabara Kanda ya Ziwa kwani imeturahisishia kuimarika kwa uchumi wetu na kurahisisha utendaji kazi katika kipindi cha utawala wake hadi kufikia sasa, amesema Daud.

Wafanyabiashara wengine akiwemo Dan William na Mwajuma Athuman wamesema kuwa katika kipindi cha utawala wa hayati Mkapa, mazao ya biashara yalikuwa yakizalishwa kwa wingi na kwamba sehemu kubwa ya wananchi walipata mitaji kutokana na kufanya kazi kwa juhudi kubwa na nidhamu.