Header Ads Widget

LIGI KUU BARA YAMALIZIKA, NDANDA, ALLIANCE, LIPULI NA SINGIDA ZASHUKA



Na Damian Masyenene
LIGI Kuu Tanzani Bara (VPL) msimu huu wa 2019/2020 imemalizika leo Julai 26, 2020 katika viwanja 10 nchini, huku timu 14 zitakazokuwepo msimu ujao, timu zitakazocheza mtoano (playoff) na nne zilizoshuka daraja zikijulikana.

Ambapo katika Msimu huu, Wekundu wa Msimbazi Simba SC ndiyo mabingwa baada ya kukusanya pointi 88 katika mechi 38, huku Wanajangwani Yanga SC wakimaliza katika nafasi ya pili na alama zao 72 na kusubiria matumaini ya kushiriki michuano ya kimataifa.

Matajiri wa Ice Cream, Azam FC wameambulia nafasi ya tatu kwa kufikisha pointi 70, huku Wageni katika ligi hiyo, Namungo FC ya mjini Ruangwa mkoa wa Lindi wakimaliza katika nafasi ya nne na pointi 64.

Timu mbili zitakazocheza hatua ya Mtoano (Playoff) kusaka nafasi ya kusalia kwenye ligi hiyo msimu ujao ni Mbeya City waliomaliza katika nafasi ya 16 na alama zao 45 licha ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 katika mchezo wao wa mwisho dhidi ya KMC.

Vile vile, Wabishi wa Kanda ya Ziwa, Mbao FC nao watalazimika kucheza Play off baada ya kushika nafasi ya 15 wakikusanya alama 45 licha ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 leo dhidi ya Ndanda FC ya Mtwara.

Timu nne zilizothibitishwa kushuka rasmi daraja leo ni Singida United iliyomaliza ligi katika nafasi ya mwisho wakikusanya alama 18 pekee kwenye michezo 38, Ndanda FC waliomaliza wa 19 na alamna zao 41, pia Lipuli FC iliyomaliza katika nafasi ya 18 na pointi zao 44 na Alliance FC ya Mwanza iliyoshika nafasi ya 17 na alama 45.

Mshambuliaji wa Simba, Meddie Kagere amemaliza ligi akiwa kinara wa upachikaji mabao baada ya kufunga magoli 22, huku kiungo wa timu hiyo, Clatous Chama akiwa kinara wa pasi za mabao na mlinda mlango, Aishi Manula akiongoza takwimu za kutoruhusu mabao mengi.

Matokeo ya mechi za mwisho zilizochezwa leo Julai 26, 2020 ni Polisi Tanzania 1-2 Simba SC, Lipuli FC 0-1 Yanga, Tanzania Prisons 2-2 Azam FC, Mbao FC 2-0 Ndanda FC na KMC 0-3 Mbeya City.

Mengine ni Alliance FC 3-2 Namungo FC, Mtibwa Sugar 2-1 Ruvu Shooting, Coastal Union 0-1 JKT Tanzania, Singida United0-2 Biashara United na Mwadui FC 2-1 Kagera Sugar.