Header Ads Widget

WADAU, SERIKALI WAWEKA MAAZIMIO KUPUNGUZA VIFO VYA WAJAWAZITO, WATOTO WACHANGA SHINYANGA




Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga, Albert Msovela akifungua kikao cha mashauriano namna ya kudhibiti vifo vya wajawazito na watoto wachanga mkoani humo.

Na Damian Masyenene – Shinyanga Press Club Blog

IDADI ya vifo vitokanavyo na uzazi kwa akina mama wajawazito na watoto wachanga hususan wanaofariki ndani ya siku saba tangu kuzaliwa kwao wanaozaliwa wakiwa wamekufa, vimezidi kuongezeka mkoani Shinyanga, hali ambayo imewaibua wadau mbalimbali ambao wamekutana na kuweka mikakati ya kupunguza changamoto hiyo.

Wadau hao wakiwemo Waganga wa tiba mbadala, waandishi wa habari, wataalamu wa afya, wazee na makundi maalum ya watu wenye ualbino na viziwi pamoja na wawakilishi kutoka Wizara ya Afya – Idara ya Kinga kitengo cha elimu ya afya kwa umma wamekutana leo Julai 2, 2020 mkoani hapa katika kikao kazi cha tathimini na mashauriano namna ya kumaliza vifo hivyo.

Akizungumza wakati wa kufungua kikao hicho, Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga, Albert Msovela amesema bado vifo vya wazazi na watoto ni vingi hususan katika kipindi hiki cha ugonjwa wa COVID-19, ambapo wadau wanatakiwa kujipanga upya namna ya kukabiliana nalo. 


 Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga, Albert Msovela akizungumza wakati wa kufungua kikao hicho.

Msovela amesema katika mkoa huo, mwaka huu tayari vifo 15 vya wajawazito vimeripotiwa, huku 50 vikiripotiwa mwaka jana na 56 mwaka 2018, ambapo kwa mwaka huu pekee tayari vifo 322 vya watoto wachanga vinavyotokana na matatizo ya uzazi vimetokea.

“Tusichukulie sana kwamba ni kwa sababu ya Corona bali tuangalie changamoto ni nini na tutafute ufumbuzi, takwimu hizi zinaonyesha bado vifo ni vingi na vinatokea kwa sababu ya mila tulizonazo kwa akina mama kutohudhuria kliniki vizuri ama kutokwenda kujifungulia huko.

“Lakini pia akina mama kutofuata maelekezo ya kutumia dawa mfano kutomeza vidonge vya kuongeza damu, pia takwimu zinaonyesha vifo vingi vinatokea wakati mama amepungukiwa damu wakati wa kujifungua na hii inasababishwa na kutohudhuria kliniki hivyo kushindwa kubainika tatizo lake mapema,” amesema.

Kwa upande wake Mratibu wa huduma za elimu ya afya mkoa wa Shinyanga, Halima Khamis, amebainisha kuwa kwa kipindi cha Januari-Machi, 2020 tayari vifo 11 vimetokea vya watoto wachanga waliozaliwa wakafariki ndani ya siku saba au kuzaliwa wamekufa, huku kukiwa na matukio kama hayo 16 kwa mwaka jana.

Ameongeza kwa kuelezea kuwa kwa kipindi cha Oktoba-Desemba, 2019 walitegemea kupata akina mama 18,500 wanaohudhuria kliniki lakini wakapatikana 15,900, huku Januari-Machi,2020 wakitegemea 19,000 lakini waliojitokeza ni 17,000.  

Mratibu wa huduma za elimu ya afya mkoa wa Shinyanga, Halima Khamis akiwasilisha hoja.
Halima alivitaja visababishi vya matatizo ya vifo vitokanavyo na uzazi kuwa ni akina mama kupoteza damu nyingi kabla na baada ya kujifungua, kifafa cha mimba, upungufu wa damu kutokana na lishe ama mgonjwa Kuugua malaria, kupasuka kwa mfuko wa mimba na maumbile ya mtoto akiwa tumboni.

“Kwahiyo ni vyema wakahamasishwa kuhudhuria kliniki kupata huduma stahiki na kwa wakati tangu wakiwa na ujauzito chini ya wiki 12 ili tatizo ligundulike na kuzuilika mapema….Bado vifo vya watoto wachanga vipo na vinatishia tuwasaidie akina mama wapate huduma mapema,” amesema.

Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Nuru Mpuya amewataka waganga wa tiba mbadala kuacha kuwapa dawa za kuongeza uchungu akina mama wajawazito kwani husababisha kupasuka kwa mfuko wa uzazi, huku pia akiwasihi wanaume kuhudhuria kliniki na wenza wao ili kusaidia kulea ujauzito katika njia sahihi.

Naye Ofisa Programu wa Wizara ya Afya idara ya Kinga kitengo cha elimu ya afya kwa umma, Yuda John amesema kutokana na Virusi vya Corona, huduma za afya ziliathirika hadi wajawazito kuhofia kwenda kliniki, huku akieleza kuwa mbali na changamoto hiyo lakini bado jamii haijahamasishwa vya kutosha kwenda kupata huduma za afya. 

Afisa Program Wizara Idara ya Kinga kitengo cha elimu ya afya kwa umma, Yuda John akizungumza na wawakilishi wa makundi mbalimbali mkoani Shinyanga.

Yuda amewataka wadau kwa kila mmoja katika nafasi yake kushiriki kuhamasisha jamii kuendelea kupata huduma za mama na mtoto, ambapo nguvu ya ushiriki, uhamasishaji, elimu na kuwa pamoja itasaidia kupunguza tatizo hilo.

Baadhi ya washirika wa kikao hicho akiwemo Mwakilishi wa Wazee Halmashauri ya Shinyanga, Boniphace Boaz ameshauri kampeni zifanyike zikiwashirikisha viongozi ngazi za mitaa kufanya uhamasishaji na ufuatiliaji.
Naye Mwakilishi wa wanawake Kata ya Masangwa, Kastian Kazimoto amehimiza mabaraza ya wazee katika vitongoji na kata kutumika kuwapa elimu na hamasa akina mama wajawazito kuhudhuria kliniki, huku wahudumu wa afya wakitakiwa kufika vijijini kutoa elimu hiyo.

Kikao hicho kilimalizika kwa kufikia maazimio matatu ya namna ya kukabiliana na tatizo hilo, ambapo maazimio hayo ni kila mwakilishi wa kundi kutumia nafasi yake na majukwaa kuelimisha na kuleta hamasa kwa wajawazito kwenda kliniki mapema na kujifungulia hospitali.

Mengine ni kila Mshiriki kuwa mfano katika jamii kwa kuleta mabadiliko chanya kufuata huduma za afya sehemu zinazoshauriwa na wataalamu wa afya, pia kushirikiana kikamilifu katika kupunguza vifo vya mama wajawazito na watoto wachanga katika maeneo yao.

 Mratibu wa Huduma za elimu ya afya mkoa wa Shinyanga, Halima Khamis akizungumza na washiriki.

 Baadhi ya wawikilishi wa kundi la wazee ambao walihudhuria kikao hicho wakifuatilia mada kwa umakini mkubwa.

 Baadhi ya wawakilishi wa idara ya afya nao wakifuatilia kikao hicho.

 
 Baadhi ya wawakilishi kutoka kundi la waandishi wa habari nao wakifuatilia hoja katika kikao hicho.

 Viongozi wa dini nao walifika kuwasilisha hoja na ushauri wao.

 Baadhi ya wawakilishi wa makundi maalum ikiwemo wenye ulemavu wa kusikia (Viziwi) nao walifika.

 Baadhi ya wadau hao wakisikiliza mada katika kikao hicho.

  wadau mbalimbali waliohudhuria kikao hicho wakifuatilia hoja zilizowasilishwa.

Picha zote na Marco Maduhu